Na Deodatus Balile
Nimesoma kitabu alichokiandika Rais (mstaafu), Benjamin Mkapa kiitwacho Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais Mtanzania Akumbuka.”
Kitabu hiki kimekuwa gumzo. Sitanii, nilisikia Rais John Magufuli akiagiza kitabu hiki kitafsiriwe katika Kiswahili. Kitabu hiki kimenikumbusha vitabu vinne vya kizalendo; Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; A View of Kwame Nkrumah 1909 — 1972: An Interpretation (Mtazamo wa Kwame Nkrumah 1909 — 1972: Fasiri); The 48 Laws of Power (Sheria 48 za Mamlaka) cha Robert Green na The Art of War (Sayansi ya Vita) cha Mchina Sun Tzu (kimeandikwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita), kilichotafsiriwa na Thomas Cleary. Vitabu hivi vinaeleza jinsi ya kujenga nchi imara.
Najua kitabu cha The Art of War, wapo waliotamani nitafsiri Kiswahili chake kama “Sanaa ya Vita”, ila hiyo itakuwa ni tafsiri sisisi – isiyofaa. Maudhui ya kitabu hiki kinazungumzia mikakati ya kisayansi jinsi ya kuepuka vita.
Mkapa katika kitabu chake ameonyesha mashimo kila kona kwa nchi yetu. Ameonyesha umuhimu wa uhuru wa mawazo, haki za kisiasa, uhuru wa kukusanyika, umuhimu wa kuwezesha sekta binafsi serikali ikabaki kukusanya kodi tu na mengine mengi muhimu.
Sitanii, sitaingia katika mtego wa majivuno, ambao Mkapa ameeleza bayana kujifahamu katika hilo zaidi ya mara 10 ndani ya kitabu hiki, kuwa jamii inamchukulia kuwa ana majivuno, suala analolithibitisha kwa kuonyesha kudharau wanasiasa, wafanyabiashara, waandishi wa Tanzania na yeyote akiamini katika Wazungu na Wakenya, jambo ambalo ni bahati mbaya kwa rais aliyeongoza nchi kwa miaka 10 kuwa na mtazamo huo.
Nimpongeze kwa kuandika Dira ya Taifa: 2000 — 2025, kwani nchi haikuwa na Dira, ukiacha Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Na kwa kweli kama hatuna Dira au tunaipuuza Dira kutumbukia shimoni mchana kweupe ni haki yetu. Amejaribu kuzungumzia umuhimu wa kujenga mifumo rafiki kwa biashara na haki za binadamu. Ametetea haki za kisiasa, ingawa wakati wa utawala wake yalitokea mauaji Zanzibar na Tanzania ikazalisha wakimbizi kwa mara ya kwanza kwenda Shimoni, Kenya, huku polisi wake wakimvunja mkono Prof. Ibrahim Lipumba!
Sitanii, kichwa cha makala hii kinasema: “Mkapa amekiri jinai, Katiba inamlinda.” Rais Mkapa alikwenda mahakamani kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Balozi Prof. Costa Mahalu, akakiri kuwa yeye alifahamu kuwa nyumba iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka kwa mama wa Kitaliano ilikuwa na mikataba miwili.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, Mkapa katika kitabu chake ukurasa wa 204 na 205 anasema: “Hivyo, ununuzi ulifanywa kwa malipo mara mbili tofauti, ingawa ushahidi uko wazi kuwa kiasi chote kilitoka Hazina ya Tanzania, kiasi chote kikalipwa katika akaunti ya Ubalozi (Italia), ambako ziligawanywa na kulipwa katika akaunti ya benki Italia na Monaco (Ufaransa).” Anasisitiza kuwa alifahamu kila kitu na aliruhusu.
Ununuzi huu ulifanyika serikali ikifahamu dhahiri kuwa kulikuwa na udanganyifu. Waziri wa Mambo ya Nje (wakati huo jengo liliponunuliwa mwaka 2001/2002), Jakaya Kikwete alifahamu. Mthamini Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi aliyekwenda Rome Julai 15 hadi 26, 2001 akalithamini jengo na kusema kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh bilioni 6, alifahamu. Ripoti za uthamini wa jengo hilo; ile ya mama mwenye nyumba ilionyesha jengo hilo lilikuwa na thamani ya Sh bilioni 5.5 na ripoti ya uthamini iliyofanywa na Serikali ya Italia iliyoonyesha kuwa jengo lilikuwa na thamani ya Sh bilioni 11.117.
Kiuhalisia serikali yetu iliamua kutumia ripoti ya mama huyo iliyofahamu fika kuwa ni fojali, hivyo ikalipa Euro 2,065,827.60 (Sh bilioni 5), na bado ikashirikiana na mama huyo kukwepa kodi kwa kulipa sehemu ya fedha hizo Monaco, nchini Ufaransa, hali iliyoikosesha kodi Serikali ya Italia. Bado bila soni, Rais (mstaafu) Mkapa, Mei 6, 2012 akaenda mahakamani Kisutu kumtetea Prof. Mahalu. Mahalu akashinda kesi. Kiuhalisia hapa Mahalu alielekezwa, na kwa vyovyote hakuwa na namna ila kutekeleza maelekezo.
Sitanii, Katiba ya Tanzania (1977), Ibara ya 46 (3) inasema: “Isipokuwa kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na masharti ya ibara ya 46A (10), itakuwa ni marufuku kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote la jinai au la kumdai mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya kuacha madaraka hayo kutokana na jambo lolote alilofanya yeye kama Rais wakati alipokuwa bado anashika madaraka ya Rais kwa mujibu wa Katiba hii.”
Hiki ndicho kichaka kilichosaidia kuipotezea Italia kodi kwa kulipa sehemu ya fedha hizi Monaco. Hivi ninajiuliza, kama ingekuwa fedha hizi zinapaswa kulipwa na mlipa kodi wa Tanzania kupitia Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gains Tax), nchi yetu ingejisikiaje kusikia rais wa nchi nyingine anashiriki kutukosesha kodi?
Hii ingefanywa na mtu mwingine bila kinga hii ya kikatiba angeozea jela. Je, tunadhani ni sahihi kuendelea na kifungu hiki? Ikiwa Mkapa alishiriki kukwepa kodi kwa kufahamu ana kinga ya kifungu hiki, je, ni mangapi ambayo hatujayafahamu aliyoyafanya kwa kutumia kifungu hiki baada ya kupata uzoefu huu? Tafakari, chukua hatua.
Ends….