DODOMA
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Ukonga (CCM), Jerry Silaa, amelia bungeni wakati akihoji kwa nini Kampuni ya Syno Hydro inapewa zabuni za kujenga miradi mbalimbali ukiwamo wa barabara ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam huku mingine ikijenga chini ya kiwango.
Kauli hiyo ameitoa Mei 23, 2022 wakati akitoa mchango wake wa bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya mwaka wa fedha wa 2022/2023.
“Pale Dar es Salaam, serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa Usafiri wa Haraka wa Mabasi (BRT) awamu ya pili, ambayo ina urefu wa kilomita 19.3 kutoka Mbagala hadi Kariakoo, Kurasini hadi Magomeni. Mradi ule una mkandarasi wa sehemu ya kwanza na ya pili,” amesema na kuongeza:
“Desemba wakati Rais Samia Suluhu Hassan anazindua sehemu ya pili alisema maneno yafuatayo na naomba nimnukuu; Juni nadhani, nilifanya ziara ndani ya Wilaya ya Temeke lakini nikapita pia barabara hii ya BRT na nikakuta ubovu ambao waziri umeutaja na nikaelekeza hatua zichukuliwe na kama viongozi wasingesimama na kusema hapa ni pabovu mkandarasi angetujengea ubovu uleule.
“Kwa hiyo niombe sana viongozi wa wilaya, halmashauri mlioko huko muwe macho lakini wakati mwingine nao labda na sisi serikali tuna tatizo, kwa sababu unaweza kukuta mkandarasi mmoja ana kazi nne – tano kwa wakati mmoja.
“Syno Hydro utaikuta kwenye hydropower kule Nyerere, utaikuta katika BRT, iko Msalato, iko katika maji, sasa mkandarasi mmoja maeneo yote hayo lazima atavuruga. Kwa hiyo mnaotoa tenda hizi nanyi muwe makini kuangalia nani yuko tayari kujenga miradi tunayowapa.”
Silaa amesema wakati Rais Samia anasema hivyo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alikuwapo, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) alikuwapo na Syno Hydro nao walikuwapo.
“Wakati Rais Samia anasema nadhani wenzetu mioyoni walikuwa wanasema mama sema haraka umalize kwa sababu si kazi moja, nne au tano ila tunakwenda kumpa ya sita,” amesema na kuongeza:
“Syno Hydro amepewa kazi ya mradi wa BRT awamu ya tatu kutoka Gongo la Mboto hadi Kariakoo wenye urefu wa kilomita 23.6 kama ilivyoainishwa, mkandarasi huyo ambaye tayari kilomita 2.5 zimetinduka kule Mbagala, mkandarasi huyo asiyelipa wafanyakazi, mkandarasi huyo asiyelipa wazabuni amekwenda kuongezwa kazi nyingine.
“Kazi hii ya kilomita 23.6 inapatikana katika Ilani ya CCM ya uchaguzi ukurasa wa 69 na wala haikusema inakwenda kumpa Syno Hydro kujenga mradi wa BRT awamu ya tatu, bali ilisema inakwenda kutatua kero za Watanzania. Rais Samia ndiye Mwenyekiti wa CCM, amesema hadharani, ameonya lakini mnakwenda kutoa kazi ile.”
Silaa amesema Rais alisema kule Mbagala alikwenda Juni na alikwenda Desemba huku Barabara ya Nyerere akiwa anapita kila siku kwenda kutafuta fedha kwa ajili ya miradi kama hiyo na mkandarasi anakwenda kufanya vitendo vya namna hiyo.
“Spika, Bunge hili nawe ukiwa ni spika ndilo ambalo limesimamia bajeti hii inayokwenda kusimamia kero hii ambayo leo iko Mbagala, iko Temeke na sasa inakwenda kurejeshwa tena Gongo la Mboto na maeneo mengine, tunakuwa Bunge la namna gani?” amehoji.
Silaa amesema Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, amekwenda kusimamia haki za wananchi wanaonyanyaswa na Syno Hydro lakini Tanroads wakamwandikia barua asiingilie mikataba ya miradi ya ujenzi wanayoisimamia.
“Kuna mikataba inayosema mkandarasi asilipe wafanyakazi? Ndiyo Tanroads hii, halafu ukisema unaonekana una jambo lako binafsi, jambo gani binafsi? Hatuwezi kuacha watu hao wakaendelea kufanya kazi hiyo. Kuna jambo nimesema hapa, kuna watu wakafikiria vibaya.
“Haya mambo ya ‘single source’ si mbaya na zabuni za ushindani nazo siyo mbaya, ubaya ni uadilifu wa wanaosimamia kazi hizi. Mradi wa mwendo kasi wa awamu ya kwanza kutoka Kimara hadi Posta umejengwa na Strabag, leo mwaka wa sita – wa saba hata shimo moja halijatokea, hivi wangempa Strabag kwa ‘single source’ kwa ujenzi wa awamu ya pili na tatu kuna watu wangelalamika?” amehoji.
Silaa amesema Arusha kuna mradi wa Sh bilioni 520 una sehemu 13 na kati ya hizo 12 zimekamilika lakini sehemu moja inayojengwa na Syno Hydro hadi sasa haijakamilika na wananchi hawapati maji kwa sababu yake.
Amesema katika mradi huo vyanzo vya maji vimekamilika, matenki yamekamilika ila mtu mmoja anafanya kazi kwa utaratibu anaouona yeye ndio unafaa.
“Waziri akija kujibu hapa nitashika shilingi ya mshahara wake, nitashika shilingi ya fungu la Tanroads na ukiwauliza wanakujibu eti Benki ya Dunia (WB) walitoa ‘letter of no objection’, msituletee habari ya namna hiyo.
“Sheria ya ununuzi wa umma sura 410 ya mwaka 2011 na kanuni zake zinaitaja Tanroads kuwa ndiyo procuring entity, ndio wanaoandaa nyaraka za zabuni na ndio wanaoandaa sifa za mwombaji.
“Tanroads mmetunga mtihani wenyewe, mmempa majibu wenyewe na mmehakikisha ameshinda na Rais ametoa kauli na bado mnakwenda kumpa kazi, mnataka nchi iende namna gani? Sisi tunakwenda kwenye uchaguzi,” amesema na kuanza kulia na kisha kukaa kwenye kiti chake.
Katika hatua nyingine, chanzo kimoja cha habari (jina linahifadhiwa) kimeliambia Gazeti la JAMHURI kuwa kinajua nini kilicho nyuma ya Syno Hydro hadi inapata zabuni za miradi mbalimbali hapa nchini.
“Naijua Syno Hydro, naijua hiyo michezo yao, sijui nini kilikuwa nyuma ya Syno, yaani nini nguvu ya Syno? Tuna wasiwasi sana, kuna watu wako ndani ya nafasi ya uongozi wa juu, wengine sijui wastaafu wapo wanaisaidia Syno vibaya mno.
“Kwa sababu nikiangalia wamelalamikiwa mno hata Awamu ya Tano. Nakumbuka kuna wakati, achana na Jokate, bali Gondwe akiwa DC Temeke, alikwenda kule na bahati nzuri wakati ule ulikuwa huwezi kumjibu ovyo DC kama alivyojibiwa Jokate, kwa hiyo kulikuwa na malalamiko yamepelekwa chini chini,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:
“Ikapelekwa timu ya uchunguzi wakathibitisha malalamiko na Gondwe akapigiwa simu afuatilie ndipo akaenda, achana na hiyo ya Jokate alivyojibiwa na Tanroads, wakati ule Tanroads wasingeweza kujibu hivyo. Kwa hiyo Syno nawakumbuka katika mchezo mmoja wa uwanja wa Msalato Desemba, mwaka juzi walimwaga fedha pale Dodoma.
“Na mshindi wake wa zabuni ilionekana angepatikana kwa utata kutokana na kiasi kikubwa cha fedha, lakini walipoomba zabuni waliomba chini ya kiwango hicho cha fedha.”
Pia chanzo hicho kimedai kuwa Syno Hydro ni wasumbufu na hata hawajamaliza mkataba tayari wameshaandika hati za madai kudai fedha wakati makandarasi wengine wanafanya kazi kisha ndipo wanadai kulipwa fedha zao.
Taarifa ya Tanroads kwa PIC
Machi 26, 2022, Tanroads, imetoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu ujenzi wa miundombinu ya BRT awamu ya pili unaofanywa na Syno Hydro na kusema hadi sasa umefikia asilimia 50.07 ukilinganisha na asilimia 50.99 iliyopangwa.
Pia taarifa hiyo imesema ujenzi wa vituo vya mabasi na madaraja ya juu haukuanza kwa wakati kutokana na mabadiliko ya usanifu yaliyoletwa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kutoka Kampuni ya Logit ya Brazil ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji.
Imesema baada ya kufanya tathmini ya maombi ya mkandadarsi ya muda wa nyongeza, mhandisi mshauri akapendekeza miezi 11 iliyoridhiwa na Tanroads na mkandarasi na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Machi 27, 2023.
Vilevile taarifa hiyo imesema kulikuwapo na kasoro ya ubora wa kazi ya zege ya barabara uliobainika Julai, 2020 na sehemu kadhaa zilionekana nyufa kuanzia pale mkandarasi alipoendelea na kazi Juni, 2020 tangu alipopunguza kasi ya ujenzi Januari, 2020 kwa hofu ya mlipuko wa Covid-19.
Imesema uchunguzi wa kina ulifanywa na kubaini kuwa nyufa hizo zilitokana na kukosekana kwa umakini wa mkandarasi na hatua zilizochukuliwa na Tanroads kuhakikisha kuwa ubora wa kazi unafikiwa na kasi ya mradi inaongezeka.
Kutokana na nyufa hizo, taarifa hiyo imesema mkandarasi huyo aliagizwa kubomoa sehemu zote zenye kasoro na kujenga upya jumla ya kilomita 2.5 (upana mita 3.5) kwa viwango vinavyokubalika kwa gharama zake mwenyewe na hadi sasa anaendelea na kazi ya kubomoa na kuweka zege upya na Tanroads inasimamia kuhakikisha anatekeleza maagizo yote kama alivyoamriwa.
Pia imesema mikutano miwili ya ngazi za juu, ikihusisha Mtendaji Mkuu wa Tanroads na wakurugenzi wenye kampuni kutoka China imefanywa kwa lengo la kuwahimiza watekeleze wajibu wao kama mkataba unavyotaka.
Aidha, imesema Februari, 2021, viongozi watatu wa juu wa mkandarasi waliondolewa katika nafasi zao katika mradi huo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kutokana na kuchukuliwa kwa hatua hizo, imesema mkandarasi huyo ameongeza kasi ya utendaji na kufikia hatua ambayo kwa sasa inakaribiana na mpango kazi uliorejewa.