Dar es Salaam
Na Mwl. Paulo S. Mapunda
Tuendelee kutoka pale tulipoishia wiki iliyopita. Mungu anaangalia neno lake apate kulitimiza, hivyo utimilifu wa neno la Mungu unatokana na utekelezaji kikamilifu alichokiagiza.
Mungu anasema; ‘njoo tusemezane.’ Kwa hiyo anatoa fursa ya majadiliano, tupeleke hoja zetu zenye nguvu tupate haki yetu.
Alisitisha kafara ya damu kwa kuimwaga damu yake yeye mwenyewe (kumbuka damu ya Yesu inajulikana kama damu ya Mungu, Mdo 20:28), kwa tendo hilo alisitisha umwagikaji wa damu kwa ajili ya kafara (sadaka).
Shetani kwa kutambua nguvu iliyomo ndani ya damu, amelibeba jambo hilo na kulifanya kuwa kiini cha mafanikio kwa wafuasi wake ulimwenguni.
Kafara za damu za watu, zimekuwa na zinaendelea kuwa msingi mkuu (mhimili) wa mafanikio na kuinuliwa katika ulimwengu wa kishetani.
Kwa kushirikiana na mawakala wake (watu waliomkubali, kumpokea na kumfuata), ameendelea kutoa kafara za watu na kuifanya dunia ielee na kuogelea katika dimbwi la damu.
Kafara za damu za watu zinaambatana na matendo machafu yanayomchukiza Mungu kama ngono za jinsia moja, ngono kinyume cha maumbile, kuharibu mimba, uvunjifu wa ndoa, ongezeko la uzinzi na umalaya duniani, matumizi ya kondomu tofauti na kanuni za kiungu za kujamiiana, ambapo tupu ya kiume inapaswa kuingia kwenye tupu ya kike ili kuinua uzao na kuendeleza kizazi huku dunia ikijaa (Mwz. 1:28).
Ikumbuke dhambi ya Onani (mtoto wa kiume wa Yuda) aliyekuwa akiingia kwa Tamari anamwagia chini ili asimuinulie nduguye uzao (Mwz. 38:8-10).
Mungu anayaeleza haya yatokeayo kupitia kinywa cha Paulo Mtume katika Rumi 1:18-32. Juu ya hayo yote, Mungu anasema wameshapata thawabu yao, kwamba hesabu ya uovu wao iko mezani pa Mungu, naye ataitolea hukumu kwa wakati wake.
Katika kusimika utawala wake duniani ulio kinyume cha ule wa Mungu muumbaji wa vyote, shetani huchagua na kutumia wabeba hatima ya familia, taifa na dunia kwa ujumla.
Mathalani wazaliwa wa kwanza wabebao nguvu na limbuko la uhai wa mzazi, shetani alimchagua Kaini (mzaliwa wa kwanza wa Adamu), Nimrod (mzaliwa wa kwanza wa Kushi), Ismaili (mzaliwa wa kwanza wa Ibrahimu, japo kwa mama mwingine), Esau (mzaliwa wa kwanza wa Isaka), Ruben (mzaliwa wa kwanza wa Yakobo) orodha ni ndefu sana.
Halikadhalika hutumia watu wenye nguvu na mamlaka ili kurahisisha utekelezaji wa malengo na mipango yake, mfano aliwatumia Farao, Herode, makuhani (wakuu wa taasisi za kidini) kama Kayafa na Anasi, watoa uamuzi kama Ponsio Pilato, mashujaa kama Goliathi, hata wateule wa Mungu kama Sauli, Daudi, Selemani hawakubaki salama mbele ya kishindo cha shetani, aliwavuruga katika tawala zao na kwa nyakati tofauti walimkosea Mungu kwa kushiriki au kutenda ushetani katika tawala zao.
Hata Ibrahimu rafiki wa Mungu, ushawishi wa shetani haukumuacha aende kwa amani, bali kwa ushauri wa sara, mkewe alizini na mjakazi (Maandiko hayasemi ni mara ngapi alitenda tendo hilo) bali tujualo ni kuwa alisababisha kuzaliwa Ismaili, mtoto anayeleta shida si kwa Waebrania pekee wa uzao wa Isaka bali duniani kote.
Hata pale shetani alipotaka kumuangamiza Yesu, alimtumia Yuda Iskariote ambaye alikuwa waziri wa fedha (mbeba hazina) katika serikali ndogo ya Yesu hapa duniani.
Kwa hiyo shetani anamtengenezea mtu dhambi kulingana na matamaniao mtu aliyo nayo, ile dhambi inakuwa inamuwinda mtu kama simba awindavyo swala, ikitafuta upenyo iliipate kumnasa, hivyo kuandaa mazingira ya kumuangamiza.
Kumbuka Mungu alimwambia Kaini dhambi iko mlangoni inakuotea (inakuwinda) ili ipate kukunasa. Hii ni kanuni inayowakabili watu wote, bali rehema za Mungu zinatufanya tuishinde dhambi.
Yusufu na Ayubu ni mfano wa watu walioishinda dhambi, hata wewe na mimi tunaweza kuishinda dhambi na kuishi maisha matakatifu na yenye kumpendeza Mungu.
Watawala wengi wa dunia hii wanapata madaraka kwa mbinu za kishetani na kusuka mifumo inayonyonga haki katika tawala zao. Hata ikitokea mtu amepata madaraka kwa nguvu za Mungu, bado shetani atamuwinda ili apate kumteka.
Hilo limetokea kwa watawala wa kale (Sauli, Daudi, Selemani na wengine wengi) na bado lingalipo hata leo hii katika tawala za hapa duniani. Maandiko yanasema haki huinua taifa (Mithali 14:34a) kwa kuwa Mungu anafahamu kuwa watawala wanatweza haki katika tawala zao.
Mbinu zilizotumika tangu kale za kuwatumia wenye mamlaka, wasuka mifumo ya kifedha na utawala, mashujaa, watunga sheria na watoa uamuzi, ni mbinu ile ile itumikayo leo hii kufanikisha malengo ya kishetani.
Watu wenye ushawishi na wanaoheshimika katika jamii ndio wabeba ajenda za kishetani. Matajiri na wenye mamlaka wanatekeleza matakwa ya kishetani hasa kutokana na viapo, nafasi au utajiri walionao ambavyo wamepata kwa msaada na nguvu za kishetani.
Ikumbukwe kwamba Yesu hakukamatwa, kushitakiwa na kuhukumiwa na watu wa kawaida bali wenye mamlaka ambao walimuona kuwa tishio katika utekelezaji wa ajenda na mipango yao, walimuona kuwa mvurugaji anayewajanjarusha watu kwa kufichua yale yatendekayo sirini (usiku, nyuma ya pazia).
Katika hukumu ya Yesu, watu wa kawaida walikuwa wafuata mkumbo, washabikiao wasilolijua (uproar for the unknown), walipiga kelele ilhali hawakujua namna ya kuingia wala kutoka (walikuwa kama vimbora au mazombi).
Katika kuthibitisha kuwa Yesu alikuwa mhanga wa wenye mamlaka, hukumu ya kifo chake haikufanyika mchana bali usiku ikifanywa na kuhani mkuu, Kayafa, akishirikiana na Anasi (mkwewe).
Ni Kayafa aliyesema yapasa mtu mmoja afe kwa ajili ya wengine, kwa kauli tajwa akawa amepitisha hukumu maarufu zaidi duniani kwa zaidi ya miaka 2000.
Hata pale walipompeleka Yesu kwa Ponsio Pilato asubuhi ya siku iliyofuata ilikuwa ni kuhalalisha hukumu waliyokwisha kuitoa usiku wa hapo kabla.
Pilato alicheza mdundo uliopigwa na Kayafa (wenye mamlaka) kwa kutoa hukumu elekezi. Naye ameendelea kuwa mtu maarufu duniani kama hakimu aliyenyonga haki mchana kweupe, kwa sababu ya shinikizo la watawala waliolewa madaraka na kujifanya miungu watu. Hali hii bado ingalipo hata katika nyakati zetu.
Kwa hiyo Yesu aliposema ‘Jiwe (Yesu) walilolikataa waashi (mashetani) limekuwa jiwe kuu la pembeni, alikuwa anawaeleza wenye mamlaka watendao ushetani kwamba nguvu zake (Yesu) zinapita mbali mno nguvu za shetani wanaye mshabikia na kumfuata pasipo kujua kwamba shetani anawapepeta kama ngano ili apate kuwateka na kuwaangamiza. Hivyo, ni jina na damu ya Yesu pekee vitupatiavyo ushindi dhidi ya shetani. Hatuwezi kumshinda kwa nguvu zetu, bali neema ya Mungu inatushindia.
Kwa mantiki hii waitwao ni wengi bali wateule ni wachache, na barabara ni nyembamba na imesongwasongwa ielekeayo kwenye uzima wa milele bali barabara ni pana ielekeayo upotevuni na ni wengi waipitao na kwa sababu hiyo, ijara yao imefungwa.
Hivyo ingieni kupitia mlango mwembamba, asema Bwana Mungu wa Majeshi aliye Alfa na Omega, nanyi mtapata uzima nafsini mwenu.
Tuwasiliane: [email protected]; 0755 671 071.