Mnyukano wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 umeanza. Vyama 10 vya upinzani vimeandaa mkakati wa kisayansi kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutumia Sheria mpya ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2018.
Kwa upande wake, CCM imejigamba kuwa maisha ya vyama vya upinzani katika uwanja wa siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao nchini ni ‘mahututi’.
Gazeti la JAMHURI linafahamu kwamba vyama 10 vya upinzani nchini vimekuwa katika mazungumzo ya siri kuhusu namna ya kuiondoa madarakani CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka kesho.
Mkakati huo unasukwa kwa kuzingatia mafanikio na kasoro zilizojitokeza katika uliokuwa ushirikiano wa kisiasa wa vyama vinne katika Uchaguzi Mkuu uliopita, 2015 (Ukawa).
Katika uchaguzi huo wa 2015, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi viliingia katika ushirikiano wa kisiasa kwa wagombea wao wa ngazi mbalimbali za kisiasa kuachiana nafasi dhidi ya CCM, lakini hata hivyo, ushirikiano huo haukuwa wa kiwango cha kuridhisha, hasa katika ngazi za ubunge na udiwani huku unafuu ukijionyesha ngazi ya urais ambako mwanasiasa wa siku nyingi, Edward Lowassa, kutoka Chadema aligombea nafasi ya urais huku mgombea mwenza akiwa Juma Duni Haji akitokea Chama Cha Wananchi (CUF), ambaye ilibidi ajiunge na Chadema kwanza ili kukidhi matakwa ya kisheria ya wakati huo.
Kwa sasa Lowassa amerejea katika Chama chake cha awali, CCM, huku Juma Duni Haji akijiondoa CUF na kujiunga ACT-Wazalendo kama ilivyo kwa aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa akiungwa mkono na ushirikiano huo wa kisiasa kwenye mbio hizo za urais wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa (kama ilivyorekebishwa mwaka 2018), Kifungu cha 11A kinaruhusu vyama vya siasa vilivyosajiliwa kuungana na kusajili chama kipya kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, Kifungu cha 11A(3) kinasema chama kipya kitasajiliwa iwapo Msajili wa Vyama vya Siasa atajiridhisha juu ya maudhui ya mkataba ulioingiwa baina ya vyama.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameliambia JAMHURI kwamba mazungumzo ya ushirikiano huo yamekwishaanza na yanaendelea. Hata hivyo, alisema ni mapema kutaja orodha ya vyama vinavyoshiriki mazungumzo hayo, kwa kuhofia kuwa wasioutakia mema upinzani “wanaweza kutia mkono wakayavuruga.”
Kwa mujibu wa Zitto, vyama vya upinzani nchini vimeweka azima ya kushirikiana na katika kushirikiana huko watarejea uzoefu uliojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Tutakuwa na mgombea mmoja katika kila nafasi, kuanzia nafasi ya urais, ubunge na udiwani. Sisi ACT-Wazalendo tutakuwa mstari wa mbele katika hilo, kuna vyama 10 vya upinzani kwa sasa ambavyo tuko kwenye mazungumzo na kuainisha mikakati ya pamoja ili kufanikisha ushirikiano huo. Hatutafanya makosa ya kuacha kila chama kipambane kwa nafasi yake, ni lazima na muhimu sana kuunganisha nguvu kila jimbo, kila kata. Changamoto za UKAWA za mwaka 2015 zimekuwa darasa kubwa na muhimu sana,” amesema Zitto katika mahojiano na Gazeti la JAMHURI.
Katika mazungumzo hayo, Zitto pia aligusia kuhusu hofu iliyopo kwamba huenda wabunge wa upinzani wataanguka zaidi katika Uchaguzi Mkuu ujao, hivyo CCM kujiongezea viti vya ubunge.
Amefafanua hilo sambamba na kubainisha mikakati iliyopo baina ya viongozi wa upinzani akisema: “Hii ni hofu iliyojengwa zaidi katika siasa za Bara, si Zanzibar, kwamba Tanzania Bara viti vya ubunge katika upinzani vitapotea vingi. Hii si hoja inayozingatia hali halisi.
“Ukitazama takwimu rasmi utaona kuwa asilimia 65 ya wananchi wako katika umri wa chini ya miaka 40, yaani kati ya miaka 18 hadi 40. Kundi hili halina upande rasmi wa kisiasa (political base), wengi wao wanategemea hali ya kisiasa ilivyo na mwenendo wake, hasa mwenendo wa kampeni.
“Lakini pia kuna kundi la wapiga kura wapya. Hawa wamezaliwa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, yaani baada ya mwaka 1992, hawa ni takriban milioni 5.7. Kwa hiyo, kisiasa hii ina maana kubwa. Maana yake ili CCM ipate kura lazima ifanye mabadiliko makubwa ya mbinu na kiuongozi. Katika hali ya kawaida makundi haya ya vijana ni magumu kupata kura zao, vijana huwa hawapigii kura ‘status quo’ (mazoea), bali wanapigia kura mabadiliko.
“Utaona, kuna vijana milioni 16 wanaingia katika mtandao wa ‘instagram’ kila siku hapa nchini. Hii ni changamoto kubwa katika kuendesha siasa za kuliteka kundi hili. Nasema suala la eti wabunge wa upinzani kuanguka kwenye majimbo yao itategemea na namna vyama vyenyewe vitakavyojipanga,” amesema Zitto.
Lakini katika hatua nyingine, Zitto pia amezungumzia mtazamo wake kwa upande wa wabunge wa CCM na namna wanavyoweza kupata taabu kujinadi kuomba kura kwenye uchaguzi wa 2020.
Zitto amesema anachokiona ni kwamba wabunge wa CCM ndio watakaopata wakati mgumu katika kutafuta kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, na kwamba hali hiyo inatokana na mwenendo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo kwa mujibu wa maelezo yake, imejikita zaidi katika miradi mikubwa ya kitaifa na kusahau miradi midogo yenye kugusa wananchi moja kwa moja majimboni.
“Wabunge hawa hawana cha kuonyesha kwa wananchi. ‘Focus’ ya serikali hii imekuwa kwenye miradi mikubwa kama ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa na miradi mingine. Sasa unaweza kuzungumzia siasa za ujenzi wa reli Morogoro au ndege – Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na maeneo mengine wanakopanda ndege hizo. Unaweza kuzungumzia mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge kwingine lakini si Kigoma, maana yake ni kwamba miradi hii mikubwa itakuwa na maeneo mahususi ya kufanyia siasa si kila jimbo la ubunge hapa nchini.
“Ilichofanya serikali ni fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya miradi kupitia serikali za mitaa hazipelekwi kwa kiasi cha kutosha, pesa zinaelekezwa zaidi kwenye miradi mikubwa. Hali hii itawapa shida wabunge wengi wa CCM kujinadi kwa wananchi ambao hawaguswi moja kwa moja na miradi hiyo mikubwa,” amesema Zitto.
Baada ya kuulizwa kuwa kuna mradi wa uenezaji umeme vijijini (REA) ambao unagusa wananchi moja kwa moja, Zitto anajibu: “REA umeme unapita vijijini kwenye njia kuu, wanachi wanaona nguzo tu, wachache sana wanaopata huduma ya umeme, na kwa namna fulani mradi huo umezua misuguano katika baadhi ya maeneo nchini”.
Hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amesema kwa sasa umeme unawafikia Watanzania wapatao asilimia 97 kwa maeneo ya mijini na asilimia 49.5 kwa watu wa vijijini, ikilinganishwa na asilimia 20 ya mwaka 2015. Pia amesema kufikia mwaka 2020 vijijini umeme utakuwa umesambaa kwa asilimia 60.
Zitto amesema miradi hiyo ya kitaifa itaweza kumnufaisha kisiasa kwa kiasi fulani mgombea urais wa chama hicho, lakini si kundi kubwa la wabunge wa CCM. “Mbunge wa Tandahimba, siasa yake ni korosho, Mbunge wa Mchinga au kwingine… hawa siasa zao si miradi mikubwa ya kitaifa ambayo haiwaunganishi wananchi wake moja kwa moja.
“Upinzani tunaweza kupoteza majimbo ya ubunge tuliyonayo kwa sababu ya mwenendo wa wabunge wetu wenyewe, lakini si kutokana na nguvu za CCM,” amesema.
Siasa za Zanzibar
Zitto amezungumzia siasa za Zanzibar na siri iliyopo nyuma ya nguvu za kisiasa za Maalim Seif Sharrif Hamad akisema: “Msingi wa siasa za Zanzibar ni Muungano, kisha mtu anakuja baadaye, kwa hiyo nguvu ya Maalim Seif ni hoja anazobeba kuhusu Muungano.
“Na ndiyo maana amekuwa anavuma misimu yote kisiasa huko Zanzibar. Ni wanasiasa wachache wenye hali kama hiyo. Hapa Afrika alikuwapo Abdoulaye Wade (alizaliwa Mei 29, 1926, akiwa amewahi kuwa Rais wa Senegal kuanzia mwaka 2000 hadi 2012).
“Wapo Wana CCM wanaopenda ionekane Maalim Seif hana lolote, lakini ukweli ni kwamba nguvu za Maalim Seif zitaendelea kudumu ilimradi changamoto katika Muungano hazitafanyiwa kazi. Kwa kadiri Muungano utakavyoendelea kulalamikiwa ndivyo Seif atakavyoendelea kubaki imara kisiasa.
“Amekuwa anatetea masilahi ya Zanzibar, na wananchi wa Zanzibar wanamwamini katika hilo, na kuna watu aina ya Maalim Seif ambao dalili zinaonyesha wanaelekea kubeba haiba kama hiyo ya Maalim kiasi kwamba hata ile hali ya siasa za Unguja na Pemba zinakuja. Utaona hata kwenye uchaguzi uliopita wa 2015 Maalim Seif kupitia CUF aliweza kupata wabunge sita Unguja.”
ACT kujinusuru kufutwa
Katika juhudi za kuhakikisha chama hicho hakifutwi, Zitto amesema licha ya kuwasilisha utetezi wao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mapema wiki hii, lakini pia wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ambazo ni pamoja na Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), mabalozi kadhaa wa Afrika na nje ya Afrika wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
“Tunaendelea kufanya mawasiliano na Jumatatu tutawasilisha utetezi wetu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Tunawaonyesha namna hoja za Msajili zisivyojitosheleza katika kufikia uamuzi wa kukifuta chama cha siasa,” amesema Zitto na kuongeza kuwa, kuna vyama vya siasa ambavyo vimewahi kufanya vitendo kinyume cha sheria dhidi ya ACT-Wazalendo, lakini Msajili wa Vyama hakuchukua hatua yoyote.
Ametoa mfano wa mmoja wa viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Ilala jijini Dar es Salaam aliyehusika kuchoma kadi za ACT-Wazalendo.
Kwa upande mwingine, Zitto anaamini kuwa kiini cha usumbufu wa kisiasa dhidi ya ACT-Wazalendo kuwa ni mtu anayesubiriwa na chama hicho kwenda kukabidhiwa kadi namba mbili, baada ya Maalim Seif Shariff Hamad kukabidhiwa kadi namba moja baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama cha Wananchi (CUF) ambacho alishiriki kukianzisha baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
“Kuliwahi kujitokeza msemo wa ‘Kazi na Bata’ ukahusishwa na mwanasiasa fulani. Kwetu ACT kuna kadi namba mbili imehifadhiwa kwa ajili ya mwanasiasa fulani, huyo ndiye anayehofiwa katika siasa za kuelekea 2020. Sisi hatujasema ni nani, lakini hofu ni kubwa.
“Na hofu hii inashangaza. Tazama, wewe timu yako inacheza uwanjani na timu pinzani inataka kufanya mabadiliko ya mchezaji ili kujiweka vizuri, unaona mchezaji anayetaka kuingia anapiga jalamba, unajijengea hofu kutokana na udhaifu wako, unazuia asiingie, kwa nini?” amehoji Zitto.
Uhakika wa ushindi CCM
Wakati Zitto akieleza mikakati hiyo, gazeti hili lilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kuzungumzia mipango hiyo ya upinzani dhidi ya chama hicho tawala na kikongwe nchini.
Polepole amejibu kwa kifupi: “Siwezi kuzungumzia mambo hayo kwa wakati huu.”
Katika hatua nyingine, mmoja wa viongozi waandamizi wa kitaifa wa CCM ameeleza kuwa kazi iliyokwisha kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inatosha kukipa ushindi wa ngazi zote kwenye uchaguzi ujao.
“Tayari tunayo ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. Hii ilikwisha kuwasilishwa kwenye Halmashauri Kuu (NEC). Kuna miradi mingi ya moja kwa moja imekwisha kutekelezwa karibu katika kila jimbo la uchaguzi nchini.
“Kuna miradi ya maji, kuna miradi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kila jimbo. Hakuna jimbo lisilo na hospitali kwa sasa nchini. Masilahi ya wananchi wa maeneo yote yanalindwa kwa nguvu kubwa. Tumezuia unyonyaji ulioota mizizi katika zao la korosho japo kuna mambo madogo ya kuyaweka sawa, lakini unyonyaji umekomeshwa. Tunawanusuru wakulima wa kahawa wanufaike zaidi.
“Wachimbaji wadogo wanafurahia shughuli zao, wamachinga wanaendelea na shughuli zao. Tunayo miradi ya umeme vijijini (REA), ujenzi wa barabara za ndani ya mitaa kupitia TARURA, hapo Dar es Salaam shida ya maji imetatuliwa, Dawasa wanafanya kazi kubwa. Kwa Zanzibar, kazi kubwa ya utekelezaji wa ilani imefanyika, wananchi wameridhika.”
Kiongozi huyo wa kitaifa wa chama hicho amesema changamoto iliyopo kwao ni kuongeza nguvu katika kunadi kazi nzuri ya Serikali ya CCM mbele ya wananchi.
Kuhusu kunasa kundi la wapiga kura vijana, kiongozi huyo amesema maendeleo yanayofanywa na serikali yanawagusa moja kwa moja, na kwa hiyo, haoni sababu ya wao kuwakosesha kura wagombea wa CCM.
UVCCM: Ni propaganda
Akizungumza na JAMHURI, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Raymond Mwangwala, amesema wapo katika utekelezaji wa mikakati ya ushindi katika chaguzi zote zijazo.
Amesema kete yao kubwa katika kujinyakulia ushindi ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kila kona ya nchi.
“Tumetekeleza kwa mafanikio makubwa miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya watu, inayokuza ustawi wa jamii. Tumefanya kwa mafanikio makubwa siasa ya maendeleo. Huduma za jamii zimeboreshwa kuanzia barabara, maji safi, huduma za afya, elimu na miundombinu.
“Viwanda vimejengwa kila mahali, Mkoa wa Pwani kuna viwanda zaidi ya 400. Maana yake unazungumzia ajira kwa vijana hapo. Serikali na hasa Rais Magufuli mwenyewe amewapa kipaumbele kikubwa watu wa maisha ya chini, tazama anavyowajali wamachinga hadi amewapa vitambulisho wasibughudhiwe.
“Wafanyakazi wameondolewa kodi zilizokuwa zinawakandamiza, ada imeondolewa shuleni. Hawa wapinzani wamebaki kupiga propaganda tu. Juzi hapa, zimetolewa ajira za walimu 4,500. Tutashinda Uchaguzi Mkuu ujao kwa asilimia 98.
“Tumekwisha kuwaonyesha dalili katika chaguzi ndogo za marudio ya ubunge zilizofanyika. Wanajua, hawana mtaji wowote wa kisiasa kwa sasa, kama ni vita dhidi ya ufisadi, Magufuli amewaonyesha namna ya kuiongoza kishujaa,” amesema.
Chadema wajizatiti
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema, katika mazungumzo yake na JAMHURI amekiri chama chake kuwamo katika mazungumzo ya ushirikiano wa kisiasa na vyama vingine.
“Ni kweli tumo kwenye mazungumzo ya namna ya kushirikiana. Jambo mojawapo la kwanza tutakalofanya kwa pamoja ni kufungua kesi kupinga sheria mpya ya vyama vya siasa. Hilo litafanyika, lakini mazungumzo yanaendelea katika maeneo mengine kadhaa,” amesema.
Kuhusu kundi la wapiga kura vijana na namna chama hicho na upinzani kwa ujumla unavyoweza kunufaika kisiasa, Mrema amesema: “Tumelenga kufikia kundi hili muhimu, sera na mipango yetu imejielekeza huko. Kuna vijana milioni 5.4 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, hawa wamezaliwa na kukua wakisikia Chadema na upinzani, tofauti na wale walioshuhudia siasa za chama kimoja (CCM).
“Wengi wamepata elimu katika shule za kata, kwa hiyo uelewa wao ni mkubwa. Wanaathirika na matatizo ya sasa yanayotokana na udhaifu wa serikali. Ajira ni shida kwao, utaona juzi serikali imetangaza ajira za walimu 4,500 lakini waliojitokeza kuomba ni 91,000. Kundi hili ni muhimu sana kwetu,” amesema Mrema ambaye amewahi kugombea ubunge Jimbo la Vunjo mwaka 2015, lakini kura hazikutosha.
Amesema wabunge wa CCM watakuwa kwenye hali mbaya kujinadi kwa kuwa serikali yao imeshindwa kuwekeza vya kutosha kwenye miradi ya wananchi majimboni.
“Mimi nilikuwa Nyanda za Juu Kusini, barabara ni mbovu. Halmashauri zimenyang’anywa vyanzo vya mapato na majukumu ya masuala ya barabara wamepewa Tarura ambao hawana fedha. Athari hizi zinawagusa wananchi moja kwa moja. Hawa hata uwaeleze kuhusu miradi ya Stigler’s Gorge, Reli ya Kisasa (SGR) au ndege hawatakuelewa. Wamejiangamiza wenyewe licha ya kwamba tumewahi kuwapa ushauri wasipore vyanzo vya mapato vya halmashauri,” amesema Mrema.
Hata hivyo, kigogo wa CCM aliyeomba asitajwe amesisitiza: “Kwa Wapinzania wa Tanzania wengi wanadhani kazi yao ni kupinga kila kitu. Wanapinga hadi mambo yanayoonekana kwa macho wazi. Leo utamwambia mwananchi serikali haijengi barabara? Shule wanafunzi hawasomi bure? Maji hayapelekwi vijijini? Umeme wa REA hauwafikii? Acha wajifurahishe, majibu watayapata kwenye sanduku la kura. CCM itawashinda hawataamini macho yao.”