Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imepakana na vijiji 19, Kijiji cha Ihombwe kilichoko Kata ya Mikumi, wilayani Kilosa kinajivunia mradi wa mkaa endelevu uliopo kijijini hapo.
Ni kupitia mradi huo kijiji kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 40 wanaofanya kazi ya doria ya kulinda misitu iliyopo kijijini hapo huku kikitajwa kujipatia maendeleo makubwa kutokana na kuuza mkaa.
Mkaa endelevu ni shughuli inayofanywa na vijana wa kijiji hicho ukihusisha kulinda misitu kwa ajili ya kuvuna mkaa.
Mkaa huo ambao unatokana na miti ambayo imelindwa na kutunzwa katika mradi wa matumizi bora ya ardhi ni manufaa ambayo yamechagizwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa misitu na mazingira wakiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Shughuli za mradi wa mkaa endelevu zinafanyika kwa njia za kitaalamu, ambapo wananchi wamefundishwa namna ya kuvuna misitu kwa kuzingatia kanuni ya mraba ‘draft’. Katika mradi huo msitu umepangwa katika vitaru ambavyo kila kimoja kinakuwa na upana sawa ambao wakati wa kuvuna watu wanakuwa kama wanacheza mchezo wa draft.
Taratibu za kutunza vitaru hivyo zinaratibiwa kwa kutumia mfumo unaofahamika kama EDU (Eneo Dogo la Usimamizi). Maana yake ni kwamba uvunaji wa mkaa unategemewa kufanyika katika eneo dogo lililosimamiwa kwa ufasaha na litavunwa kwa awamu mbili ambazo zimepangwa kufanyika kila baada ya miaka 12.
Njia hiyo huhusisha kitaru ‘A’ kikivunwa leo, kitavunwa tena baada ya miaka 12 na kwa kipindi hicho kitaru ‘B’ nacho kitavunwa kwa kuzingatia utaratibu huo huo.
Katika eneo dogo inaelezwa kuwa uvunaji wa mkaa unaweza kufanyika kwa miaka 24 bila kuathiri uoto wa eneo hilo, wala kuathiri uhai wa viumbe wengine na kwamba katika eneo lenye chanzo cha maji uvunaji wa mkaa hauruhusiwi.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ihombwe, Vashly Climile, anaeleza kuwa kijiji hicho kupitia mradi wa mkaa endelevu kimeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Anasema tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2012, kijiji kimekusanya jumla ya Sh milioni 206. 4 ambazo zimetokana na uuzaji wa mkaa pamoja na shughuli nyingine za kuuza mbao na ulinzi shirikishi wa msitu.
Anasema katika fedha hizo Sh milioni 129.118 zilipelekwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara ya Sekondari ya Kata ya Mikumi, huku kijiji hicho kikichangia zaidi ya Sh milioni 4.4.
Climile anasema hata baada ya TANAPA kujenga Zahanati ya Ihombwe haikuwa na umeme, hivyo kupitia mfuko huo wa maendeleo kijiji kilinunua solar zenye thamani ya Sh 400,000 pamoja na kulipia bima za afya kwa wananchi wake, ambapo Sh milioni 6.9 ziligharamia bima hizo.
Anaeleza kuwa katika awamu tatu tofauti kijiji kilitenga zaidi ya Sh milioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa barabara inayoingia katika kijiji hicho ikitoka barabara kuu ya Mikumi – Kilosa.
“Kwa sababu ya ujirani mwema, TANAPA wanatusaidia greda, sisi kama kijiji tunaweka mafuta na kuifanyia ukarabati barabara yetu,” anasema Climile.
Hata kwenye ujenzi wa ofisi ya kijiji walichangia Sh milioni 4 ambayo ni sawa na asilimia 5 ya fedha zilizotoka kwenye mfuko wa maendeleo huku asilimia 95 iliyobaki ikitajwa kutoka kwenye mradi wa mkaa endelevu.
Anasema kijiji kimenunua pikipiki mbili ambazo zinasaidia katika shughuli za ujenzi, huku fedha hizo zikisaidia katika ujenzi wa madarasa mawili na choo cha wanafunzi.
Mbali na ujenzi wa madarasa hayo, kijiji hicho kimesaidia kujenga nyumba ya muuguzi wa zahanati ya kijijini hapo pamoja na kuifanyia maboresho nyumba ya ofisa mtendaji wa kijiji.
Climile anasema mwaka jana kijiji kimeweza kutenga asilimia 10 ya pato lake na kulipeleka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ili wilaya hiyo iweze kusaidia kutuma wataalamu wa kutoa elimu ya maendeleo katika kijiji hicho.
“Mwaka jana tulichangia jumla ya Sh milioni 3, na hiyo ni sehemu ya maendeleo sisi kama kijiji tumefanya kutokana na shughuli za kuvuna mkaa endelevu, miradi yote niliyoitaja inaingia katika hizo Sh milioni 129.118 nilizotaja awali,” anasema.
Hata hivyo anasema jumla ya Sh milioni 77.250 zimetumika katika shughuli za kuratibu usimamizi wa msitu wa kijiji hicho.
Anasema fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kulipana posho, kununua vifaa vya kufanyia doria na kuwawezesha maofisa wanaotoa elimu ya uhifadhi katika msitu huo.
Mipango ya mwaka huu kwa mujibu wa ofisa mtendaji huyo ni pamoja na bajeti ya Sh milioni 15 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu cha maji ya kunywa. Anasema karibia asilimia 60 ya fedha zote zinazotokana na mradi wa mkaa endelevu zinafanya kazi ya usimamizi wa misitu huku asilimia 40 inayobaki inatengwa kwa ajili ya maendeleo.
Mradi huo wa mkaa endelevu katika kijiji hicho umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2012 katika Wilaya ya Kilosa ukihusisha vijiji 10 vya awali, ambavyo ni Ihombwe, Kisanga, Msinda, Ulaya – Kibaoni, Ulaya – Mbuyuni, Kigunga, Nyali, Kitunduweta, Mhenda na Dodoma – Isanga.
Inaelezwa kuwa lengo kuu la mradi huo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuboresha masuala ya utawala na kuwafanya wananchi waweze kunufaika na rasilimali zinazowazunguka ikiwemo misitu.
Utekelezwaji wa mradi wa mkaa endelevu unatajwa kufanyika katika awamu kuu mbili, ambapo awamu ya kwanza ilianza Machi, 2012 hadi Novemba 2015 huku awamu ya pili ikitajwa kuanza Desemba 2015 na inatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Kufanikiwa kwa mradi huo ni matokeo ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umeratibiwa na kijiji hicho kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG).
Michael Nilongo, ni Mratibu wa Mradi wa Mkaa Endelevu chini ya Shirika la TFCG katika Kijiji cha Ihombwe, anasema kuwa kijiji hicho ni mnufaika mkuu wa mradi huo katika vijiji 10 vya awali vilivyopokea mradi.
Anasema kijiji hicho eneo lake limepimwa kisheria na kupatiwa hatimiliki ya ardhi na kwamba ukubwa wake ni hekta 20,001.37 huku eneo la misitu peke yake akilitaja kuwa na ukubwa wa hekta 13,790.
Nilongo anaeleza kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo katika eneo la kijiji hicho walianza kwanza na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya ardhi pamoja na usimamizi shirikishi wa misitu.
“Tulianza kufanya mikutano na wananchi wa kila kitongoji ili waweze kuuelewa mradi na mara baada ya kuuelewa na kuupitisha tulianza kuwasaidia kuhusu matumizi bora ya ardhi.
“Tulifanya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa maana ya eneo lote la Ihombwe lilipimwa kwa kuonyesha eneo la makazi ya watu, eneo la mifugo, eneo la mashamba na shughuli zingine zote,” anaeleza Nilongo.
Katika hekta 13,790 za msitu zilizopo katika eneo la kijiji hicho, Nilongo anasema ziligawanywa katika matumizi tofauti kulingana na mapendekezo ya wananchi waliyoyatoa kuhusu msitu huo.
Anaeleza kuwa msitu uliopo katika eneo hilo umegawanywa katika kanda kuu tano, ambazo ni kanda ya malisho iliyopo katika Kitongoji cha Mfilisi, kanda ya uzalishaji wa mbao, kanda ya kuni pamoja na majengo, hii anaieleza kuwa ilitengwa kwa lengo la wananchi kuitumia kwa kukata miti ya kujengea nyumba na kuni za kupikia.
Kanda nyingine ni kanda ya uzalishaji wa mkaa endelevu na kanda ya kutunza bayoanuai na vyanzo vya maji. Kwa mujibu wa Nilongo, mradi wa mkaa endelevu katika eneo lote la msitu uliopo katika kijiji hicho unatekelezwa kwenye asilimia 10 peke yake ya msitu wote.
Anafafanua kuwa katika hizo asilimia 10 za eneo lililotengwa kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa na kuni nalo limegawanyika katika vitaru vidogo vidogo.
Anasema katika kila kitaru kimoja kunakuwa na bloku 24 ambazo kila bloku moja inakuwa na ukubwa wa mita 50 kwa 50 kwa kuzingatia ukubwa wa msitu.
Kwa mujibu wa Nilongo, Kijiji cha Ihombwe kina jumla ya vitaru 107 ambavyo kwa mwaka huvunwa kwa kuzingatia utaratibu maalumu.
“Lengo la kufanya hivi ni kutaka kuvuna kitaalamu, mfumo wa kuvuna unaitwa ‘draft’, ni mfumo wa kuvuna bloku moja halafu unaruka bloku moja na kuvuna inayofuata hadi bloku zote zitakapoisha,” anaeleza Nilongo.
Kwa mfumo huo Nilongo anasema vitaru hivyo vitavunwa kwa miaka 24 na kwamba kutokana na tabia ya miti ya miombo kukua kwa kujirudia baada ya miaka hiyo kupita, bloku za mwanzo zilizovunwa wanatarajia mashina yatakuwa yamechipuka na kukua upya, hivyo uvunaji utaanza upya kwa kuzingatia mfumo wa draft.
Hata hivyo anaeleza uvunaji wa aina hiyo unaacha baadhi ya miti bila kuvunwa huku akiitaja miti inayofaa kwa mbao na ile yenye viota vya ndege kuachwa ili baadaye ivunwe kwa utaratibu unaofaa ikiwa ni pamoja na kuzingatia usalama wa viumbe vingine vinavyopatikana katika miti hiyo.
Anabainisha pia miti inayopaswa kuvunwa kuwa ile yenye kipenyo cha sentimeta 15 kwenda juu na kwamba ikiwa haijafikisha ukubwa huo inaachwa ili ikue zaidi.
“Pale kijijini kuna kamati ya maliasili imeundwa na wajumbe wake wamepewa elimu kuhusu misitu, shughuli zote zinazohusiana na misitu wao wenyewe wanaziendesha,” anasema Nilongo.
Zawadi Mahinda, Mhifadhi ujirani mwema wa Hifadhi ya Mikumi, ameeleza kuwa kazi ya kitengo hicho ni kushirikiana na wananchi wa vijiji husika kufanikisha miradi mbalimbali wanayokuwa wameiibua katika vijiji vyao.
Anasema asilimia 30 ya utekelezaji wa miradi inayoibuliwa na vijiji hivyo hutegemea wananchi wenyewe huku asilimia 70 iliyobaki ikitegemewa kutoka kwenye mfuko wa kitengo cha ujirani mwema kinachoratibiwa na TANAPA.
Mahinda anasema kupitia kitengo hicho karibu asilimia 80 ya miradi iliyoanzishwa katika vijiji 19 vinavyozunguka Hifadhi ya Mikumi wameshiriki kuifanikisha huku akitaja Kijiji cha Ihombwe kunufaika na mradi wa matumizi bora ya ardhi pamoja na ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho ambao umeratibiwa na TANAPA Mikumi.
Eda Nundwa, Muuguzi wa Zahanati ya Ihombwe anasema anaishukuru TANAPA na serikali ya kijiji kwa kutambua mchango wa sekta ya afya kwa wananchi na kwamba uamuzi wa kujenga zahanati hiyo umepunguza taabu za wananchi walizokuwa wakipata kwa kutembea zaidi ya kilometa 25 wakifuata huduma ya afya katika vituo vya afya vilivyoko Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi.
Anasema kwa sasa katika zahanati hiyo wananchi wanapata matibabu bila shida yoyote huku akiupongeza uamuzi wa serikali ya kijiji hicho kuwapatia bima za afya kaya zisizojiweza.
Godson Chilongola, mkazi wa kijiji hicho amesema mafunzo ambayo wamepata kuhusu matumizi bora ya ardhi yamewasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kuiheshimu mipaka ya Hifadhi ya Mikumi ambayo imepakana na kijiji hicho.
Anaeleza kuwa kijiji hicho kupakana na Hifadhi ya Mikumi ni fursa kwao kwa sababu wanapofanya doria za kulinda misitu iliyopo katika maeneo yao wanapata fedha za kujikimu wao na familia zao.
Kwa upande mwingine, Michael Nilongo, ameeleza kuwa kuna changamoto za kisera kuhusu masuala ya uhifadhi wa misitu na uvunaji wa mazao yatokanayo na misitu.
“Mti ukiwa msituni unakuwa chini ya Wizara ya Maliasili ila ukisha kuuchoma kama mkaa mti huo huo unakwenda kwenye Wizara ya Nishati, lakini ukienda kwenye sera ya misitu, mkaa umezungumziwa kidogo.
“Ukienda kwenye Wizara ya Nishati, wao wamejikita kuzungumzia gesi na umeme, lakini ukiangalia karibu asilimia 90 ya Watanzania wanatumia nishati ya kuni na mkaa kupikia, lakini hiyo kwenye sera haijazungumzwa kwa kina na kuona ni kwa namna gani tunaweza kutumia nishati ya gesi na umeme na kuachana na kuni na mkaa,” anasema Nilongo.
Anasema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa ili Watanzania wote waweze kufikia kiwango cha kutumia nishati ya gesi na mkaa ambavyo ni vipaumbele vya serikali kwa sasa kuna safari ndefu inayohitaji miaka zaidi ya 20 au 30.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).