Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea. 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa wa chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Gombo Samandito amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu na kushiriki kikamilifu uchaguzi wa Serikali za Mitaa akisisitiza umuhimu wa ushiriki sauti zao zinasikika na kuimarisha demokrasia nchini. 

Samandito ameyasema  hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za chama cha waandishi wa habari zilizopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,alisema kuwa ushiriki huo ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.

Gombo Samandito Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa wa CHAMA cha UMD akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za chama Cha waandishi wa Habari zilizopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

” Nipo hapa kuzungumza na ninyi waandishi wa habari kuelekea uchaguzi za serikali za mitaa na hatimae mwakani uchaguzi mkuu na nipo hapa ili kuwaeleza wananchi wa Tanzania UMD tunataka nini ukizingatia chama cha siasa chochote kinapokuwa kimeanzishwa maana lengo lake ni kuchukuwa dola hakuna lengo lingine”alisema Samandito. 

Alisema chama cha UMD kitashiriki uchaguzi kila mahala na watakuwa na wagombea ambao watawasimamisha kugombea  nafasi mbalimbali ikiwemo ujumbe wa Serikali za Mitaa na vijiji.

“Tunajaribu kuhamasisha wananchi wote wazingatie taratibu ambazo zimewekwa na serikali, wajiandikishe kwa wingi ,wajitokeze kwa wingi kwenye kupiga kura na kugombea nafasi ” alisema.

Alisema kuwa utaratibu wa kupokezana madaraka ni uchaguzi hivyo chama cha UMD tunawataka wananchi wajitokeze kwa wingi ili waweze kupiga kura zao na wachague chama wanachokitaka ili kiweze kuongoza nchi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo .

Aidha amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi na waende wakakichague chama cha UMD vizuri kabisa ili kiweze kushika dola na kuweza kufanya maendeleo mengi na makubwa ambayo chama cha UMD kimepanga kuyafanya kwa ajili ya wananchi wa Tanzania.