DAR E SALAAM
NA MWANDISHI WETU,
Akiwa ziarani katika Mkoa wa Simiyu, Rais John Magufuli, alimsifu Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka, na kumtaja kama kiongozi mahiri aliyefanya mambo mengi, mazuri kwa muda mfupi.
Akasema awali alipopendekeza jina la Mtaka, aliambiwa (vetting) kuwa kiongozi huyo kijana hafai hata kuwa Mkuu wa Wilaya (DC), lakini kazi alizofanya zimemfanya awe RC mchapa kazi bora kati ya wakuu wa mikoa wengine.
Kwa kulitambua hilo, JAMHURI limeona ni vizuri kuwaletea wasomaji wake wasifu wa RC Mtaka kama ulivyoandaliwa na kundi la Watanzania wanaounga mkono juhudi za kuijenga Tanzania mpya.
Anthony John Mtaka Chiganga alizaliwa Julai 5, 1983 Majita mkoani Mara. Yeye ni mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Merciana Magati na John Mtaka.
Alisoma Shule ya Msingi Suguti, Musoma mkoani Mara ambako alihitimu mwaka 1996. Alisoma Shule ya Sekondari Mwembeni, Musoma mkoani Mara kuanzia mwaka 1997 hadi 2000. Alisoma kidato cha tano na sita mwaka 2001 hadi 2003 katika Shule ya Sekondari Suji, Kilimanjaro.
Mwaka 2004 alijiunga katika Chuo cha Ualimu Marangu, lakini hakuendelea baada ya muhula wa kwanza. Akaenda kupata mafunzo ya Jeshi la Polisi. Namba yake ni F. 6886 PC A. MTAKA.
Baadaye alikwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro ambako alihitumu Shahada ya Utawala mwaka 2009.
RC Mtaka alifanya kazi kwenye Mfuko wa PPF kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero (Morogoro) na baadaye Hai (Kilimanjaro). Machi 13, 2016 Rais John Magufuli, alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
RC Mtaka ni mwanariadha. Ni Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Tanzania, ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za Injili, na mwandishi wa makala.
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa mwaka 2012 ukiwa hauna maendeleo makubwa. Chini ya uongozi wake, Simiyu imekuwa ya kupigiwa mfano kimaendeleo. Ndani ya muda mfupi amehakikisha Simiyu inapata viwanda mbalimbali na miradi mingine ya maendeleo. Miongoni mwa viwanda hivyo ni vya maziwa na chaki.
Amesimama imara katika kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda mkoani Simiyu, akitumia mbinu ya kuwapa motisha walimu na shule zinazofanya vizuri kimkoa na kitaifa.
Septemba, mwaka jana alipewa tuzo ya Asasi ya Wazalendo na Maendeleo Tanzania kutokana na maendeleo makubwa aliyoyafanya mkoani Simiyu katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
.tamatiā¦.