*Tume ya Jaji Warioba ilianika madudu yake

*Ni bilionea anayehodhi vitalu vya uwindaji

Hivi karibuni, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) aliuibua bungeni mkataba ulioingiwa baina ya kampuni za Uranium Resources PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited uliotengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya Rex Attorneys, na kusainiwa Machi 23, 2007.

Mkataba husika ambao vipengele vyake vinaainisha kwamba unatakiwa uwe wa siri, unaihusu kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa na Mohsin M. Abdallah na ndugu Nargis M. Abdallah.”

Mohsin Abdallah ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na mmoja wa wafadhili wakubwa wa chama hicho. Pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA). Mtu huyu ameshutumiwa kwa ukwepaji kodi na ‘kuwanunua viongozi’ wa kisiasa na wa vyombo vya dola.


Mwaka 1996 Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliunda Tume ya Kuchunguza Kero ya Rushwa nchini. Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe kenda, iliongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba.


Katika ripoti hiyo, Mohsin, pamoja na washirika wake walituhumiwa kwa mambo mbalimbali. Gazeti la JAMHURI limeona ni vema likawakumbusha wasomaji ili waweze kumjue vema kada huyu wa CCM mwenyhe ukwasi wa kutisha.

Ifuatayo ni sehemu ya ripoti hiyo ililiyomhusu Mohsin na wenzake – neno kwa neno:

Hill Top Hotel and Tours Ltd inayomilikiwa na Mohsin Abdallah na Hitesh P. Arjun ilipewa Certificate of Approval Enterprise na Kituo cha Uwekezaji Rasilimali tarehe 3/1/1991.


Baadaye watu hao walianzisha kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel iliyosajiliwa tarehe 2/4/1992 na ambayo ilirithi ‘Certificate of Approval Enterprise iliyokuwa imetolewa kwa kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel and Tours kuendeleza ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya Kigoma. Kampuni hii mpya inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Hitesh Arjun na Deusidedit Kisisiwe. Wamiliki hawa pia wanamiliki makampuni mengine ama kwa pamoja au mmoja kama ifuatavyo:


(i) SHENIS COMMERCIAL LTD inayoshughulika na mauzo ya nguo, vitambaa na vipuri vya magari na mashine inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Mrs Nargis Mohsin Abdallah na Deusdedit Kisisiwe. Kampuni hii ilisajiliwa tarehe 27/7/1988.

(ii) TILE ANDA TUBE LTD iliyosajiliwa tarehe 7/12/1992 inashughulikia na biashara ya vifaa vya ujenzi, umeme, pombe na dawa na inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Deusdedit Kisisiwe na Tariq Mirza.

(iii) FIVE WAYS CLEARING AND FORWARDING AGENCY iliyosajiliwa tarehe 23/10/1992 kwa ajili ya kuondoa mizigo bandarini na usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia mbalimbali, biashara ya vipuri na vifaa vya ujenzi, uchimbaji na uuzaji wa madini nchi za nje inamilikiwa na Triphon Maji na Deusdedit Kisisiwe.

(iv) ROYAL FRONTIER (T) LTD iliyosajiliwa tarehe 7/3/1994 kwa ajili ya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa watalii, inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Deusdedit Kisisiwe na Rashid Omar.

(v) GAME FRONTIER (T) LTD nee MNM Hunting Safaris Ltd, inafanya shughuli zinazofanana na zile za Royal Frontier na inamilikiwa na Mohsin Abdallah, Mr. Abdikadir Mohamed na Mr. Ahmad Muhidin.

 

Shenis Commercial Ltd ndiyo kampuni ya kwanza kisha ikafuatiliwa na Kigoma Hill Top. Baadaye makampuni mengine yaliibuka haraka haraka, jambo linaloashiria kwamba yalitokana na Kigoma Hill Top na yanafanya shughuli zake kwa kushirikiana. Vifaa vilivyoagizwa na Kigoma Hill Top na kusamehewa kodi ni vingi kuliko mahitaji ya hoteli.


Kwa mfano, kampuni iliagiza vigae vya sakafu 27,248, containers 3 za marumaru zenye ujazo wa mita za mraba 3264.8, magodoro 120 na taulo 4,00 wakati hoteli ina vitanda 60 tu. Aidha, iliruhusiwa kuagiza boti tatu na injini nne (outboard engines) na kufanya Hoteli hiyo kuwa na boti 7.


Idadi hii ya boti ambazo imeelezwa kwamba zitatumika kwa uvuvi wa kitalii ni nyingi sana ikilinganishwa na idadi ya vyumba vya hoteli hiyo na inawezekana zitatumiwa kwa shughuli nyingine. Vifaa vya ziada inaaminiwa viliuzwa na makampuni mengine yanayomilikiwa na wakurugenzi wa Kigoma Hill Top Hotel.

Taarifa ya IPC inaonyesha kwamba ingawa kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel ilipatiwa misamaha ya kodi, IPC haikuona na haikupendekeza aina ya vifaa vya ujenzi wa Kigoma Hill Top Hotel vinavyotakiwa kusamehewa kodi.


Wakurugenzi wa kampuni walikuwa wanawasiliana na Hazina moja kwa moja kuanzia mwaka 1991 hadi Julai 1995 walipoanza kupitisha maombi ya misamaha hiyo IPC. Hata hivyo, baadhi ya vifaa ambavyo vilisamehewa kodi na Hazina havikustahili kusamehewa kodi.

 

Kwa mfano, kampuni ilisamehewa kodi magari Na. TZF 5059 Toyota S/Wagon, TZF 8455 Toyota L/Cruiser, TZF 8612 Land Cruiser S/Wagon na TZF 6001 ambalo ni gari ya kifahari aina ya magari ya Mercedes Benz Sportscar, na ndege moja.


Ijapokuwa magari na ndege hiyo vyote vilisamehewa kodi chini ya mradi wa Kigoma Hill Top yamekuwa yanatumika na kampuni zao nyingine hapa Dar es Salaam na Kigoma. Kwa mfano, gari TZF 8454 lililoandikishwa tarehe 16/6/1994 kama mali ya Kigoma Hill Top, chini ya Import Declaration, mwagizaji alikuwa Royal Frontiers na Import Entries zilionyesha Kigoma Hill Top.

 

Kampuni hii ilikuwa iagize ndege mwaka 1995 na ikasamehewa kodi kwa barua Kumb. Na TYC/1/150/9/176/7. Uchunguzi umeonyesha kwamba hakuna ndege iliyosajiliwa hapa nchini kwa jina la kampuni hiyo, lakini kampuni ya Game Frontiers ina ndege yenye namba za usajili 5H-GFT (Cesna 206) iliyosajiliwa mwaka 1995.


Uchunguzi pia unaonyesha kwamba kampuni ya Kigoma Hill Top Hotel inatumia sana ndege hiyo kwa kuwapeleka watalii na wageni huko Kigoma Hill Top Hotel ingawa haina leseni ya biashara ya usafiri wa anga. Tume imezungumza na mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Kigoma Hill Top, Deusdedit Kisisiwe, lakini maelezo aliyoyatoa kuhusu tuhuma hizo hayakuridhisha.

Tume inaamini kwamba:


(i) Bwana Mohsin Abdallah na wenzake, hasa Deusdedit Kisisiwe wamefungua kampuni nyingi za biashara na kuomba misamaha ya kodi kwa kampuni moja ya Kigoma Hill Top Hotel. Kampuni imeagiza vitu vingi vilivyosamehewa kodi na kuvitumia au kuviuza kupitia makampuni yao mengine ambayo hayakupata misamaha ya kodi.

(ii) Wafanyabiashara hawa wamekuwa wanawatumia viongozi wa Serikali katika kuficha maovu yake. Kwa mfano, Kampuni ya Fiveways Clearing and Forwarding Agency ilimpa hisa Bw. Tryphon Maji aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo alikuwa habughudhiwi na polisi anapofanya vitendo kinyume cha kanuni na taratibu.


Katika makampuni ya Royal Frontier (T) Ltd hisa zimetolewa kwa ndugu wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Utalii na Mazingira Bw. Juma Hamad Omar na katika kampuni ya Game Frontiers (T) Ltd hisa zimetolewa kwa Ahmed Muhidin ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori Bw. Muhidin Ndolanga.

 

Hisa hizi zimetolewa kwa wakubwa hawa kama kivuli (cover) ili waweze kuyapatia makampuni haya vitalu vya uwindaji pamoja na kurahisisha shughuli za uwindaji.(iii) Bw. Mohsin Abdallah na Kisisiwe wanapenda kuwatumia viongozi kama chambo katika biashara zao, ili waweze kuvuka kikwazo chochote kile kitakachokwamisha biashara zao.