Ukishangaa ya Musa…hivyo ndivyo naweza kusema kuhusu binti (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria) mwenye umri wa miaka 16, ambaye anatakiwa kuwa shuleni, lakini haiko hivyo kwake, yupo nyumbani analea mtoto wake mwenye umri wa miezi minne.

Anatamani kupata nafasi ya kusoma tena lakini anashindwa kuwatumikia ‘mabwana wawili’, yaani mtoto na shule, yeye amechagua kumlea mtoto. Mtoto wake amepewa jina la ‘Miracle’ yaani (Muujiza).

Historia ya binti huyo inasikitisha, alibeba ujauzito akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule moja ya sekondari iliyoko ndani ya Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano na Gazeti la JAMHURI, amesema ilibainika kuwa yeye ni mjamzito baada ya walimu wa shule aliyokuwa akisoma kufanya vipimo vya mimba kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo wakati wa maandalizi ya kufunga shule muhula wa kwanza mwaka jana.

Anasema hakuwa anafahamu kama ni mjamzito japo anakiri kwamba suala la mahusiano ya kingono alilianza tangu akiwa na umri wa miaka 13.

Ameliambia JAMHURI kwamba wakati anasoma shule moja iliyopo katika Kata ya Saranga alianza mahusiano na mjomba wake anayefahamika kwa majina ya Saimoni Elias.

Anasema kuwa kwa mara ya kwanza mjomba wake alianza kumshawishi waingie kwenye mahusiano kwa ahadi ya kumpatia pesa za kutumia akiwa shuleni pamoja na ahadi ya kumsomesha shule ya sekondari iliyo bora atakapofaulu mtihani wa darasa la saba.

“Sikuwa na namna ya kukwepa vishawishi hivyo, kwa sababu mazingira niliyokuwa nikiishi na bibi yangu yalikuwa ni ya hali ya chini mno, bibi kwa kipindi hicho alikuwa akinipatia Sh 500 kila siku kama pesa za kula shuleni, na siku nyingine alikuwa hanipi pesa hizo.

“Hali hiyo ikanisababisha kuingia vishawishi vya kumkubalia mjomba ili niweze kupata pesa za kutosha kula vyakula nilivyokuwa navipenda wakati nikiwa shuleni, tangu nikiwa mdogo nilipenda kula, hali hiyo ilinisumbua wakati nilipokosa pesa za matumizi kutoka kwa bibi,” amesema binti huyo.

Hali ya kukosa pesa za kutumia shuleni anaitaja kusababishwa na kipato kidogo kitokanacho na shughuli ya bibi yake (Anna Elias) ya kuuza chakula eneo la Kimara Mwisho (mama lishe), shughuli ambayo inategemewa kutunza familia nzima.

Ameliambia JAMHURI kuwa pamoja na ahadi hizo, kilichomsababisha akubali ni kitendo cha kuwahi kupata malezi ya mjomba huyo kabla ya kuishi na bibi yake, kwani alianza kulelewa na mjomba wake maeneo ya Tegeta Wazo Hill. Aliishi na mjomba wake huyo baada ya mama yake kutengana na baba yake.

“Mjomba alinichukua na kwenda kuishi naye, baada ya kuanza kuishi naye alianza kunisomesha masomo ya awali lakini kutokana na changamoto za kimaisha mjomba alihamia mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya shughuli za kibiashara, hali iliyosababisha nirudishwe kwa bibi Kimara Stop Over,” amesema.

Binti huyo anasema alipofikisha umri wa miaka 13 mjomba wake huyo alianza ‘kumtamani’ na kumweleza haja yake ya kuwa naye kimapenzi kwa sharti la kumsaidia mahitaji yake na kumsomesha zaidi.

Kutokana na mjomba wake huyo kuhamia Arusha na kuamua kuwa na makazi ya kudumu huko, kila alipokuwa akija Dar es Salaam ilimlazimu kufikia Kimara Stop Over kwa mama yake, ambaye ni bibi yake binti aliyeharibiwa maisha.

Binti huyo anasema bibi yake alikuwa akishinda kwenye biashara, hivyo mjomba wake huyo alitumia fursa hiyo kumrubuni na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi.

“Siku ya kwanza tunafanya mapenzi nilipata maumivu makali sehemu zangu za siri, lakini kutokana na ahadi nilizopewa na mjomba huku akiniambia nisiseme atanipatia zawadi, nilimtunzia siri,” amesema.

Binti huyo anasema kuna siku mjomba wake huyo amewahi kufumaniwa na bibi yake. Anasema bibi yake alikuwa akitoka katika shughuli zake usiku, akamkuta Saimoni anatoka kwenye chumba cha binti huyo.

Anasema wakati bibi yake anamuona mwanaye (Saimoni) akitokea chumbani mwa binti huyo ilikuwa ni muda wa usiku, saa ambazo watu wamelala.

Hali hiyo ilimfanya bibi yake kumtilia shaka mwanaye kwani mazingira yalijionyesha dhahiri kwamba kuna kitu kinaendelea baina ya mjukuu wake na mwanaye, maana alikuwa anatoka chumbani kwa binti huyo akiwa amevaa bukta pekee.

Mazingira hayo yalimfanya bibi huyo kufanya upekuzi katika chumba anacholala mjukuu wake huyo na kubaini nguo za ndani (Boxer) tatu za mwanaume katika chumba hicho.

Binti huyo anakumbuka kwamba aliulizwa na bibi yake kuhusu uwepo wa nguo hizo za kiume kwenye chumba cha binti huyo, lakini alipoulizwa hakuwa tayari kutaja nguo hizo za ndani zilikuwa za mwanaume gani, kwa sababu alikuwa kwenye mahaba mazito na mjomba wake, hivyo hakuwa tayari kufichua siri hiyo.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba mbali na bibi huyo kugundua kinachoendelea baina ya mjomba mtu na binti, bado hakuwa tayari kulizungumza suala hilo katika ngazi ya familia.

Binti huyo anasema hali ya kufanya mapenzi baina ya wawili hao haikukoma, waliendelea kufanya hivyo kila mjomba wake alipokuja Dar es Salaam akitokea Arusha.

“Miezi kadhaa kabla sijabainika kuwa mjamzito ulitokea mgogoro wa kifamilia baina ya bibi yangu na mjomba, mgogoro huo ulihusu kugombania mirathi, ugomvi huo ulikuwa unalenga kuuzwa nyumba iliyoachwa na babu yangu.

“Ugomvi huo ulisababisha kuzuka migogoro ya kifamilia hadi kufikishana kwenye vyombo vya sheria kutafuta suluhisho,” amesema binti huyo.

Inaelezwa kuwa kabla ya mgogoro huo kuwa mkubwa, familia ilitenga vyumba ambapo kila mtoto alipewa chumba chake, ambavyo katika vyumba hivyo Saimoni alikuwa na chumba kimojawapo ambacho kiko karibu na chumba anacholala binti huyo.

JAMHURI limezungumza na Saimoni Elias, ambaye anatuhumiwa kumbebesha ujauzito mpwa wake. Katika mahojiano na JAMHURI, amesema kuhusishwa kwake na jambo hilo kunahusu mgogoro wa kifamilia uliopo.

“Jambo hili lilichochewa na mgogoro wa kifamilia baina yangu na mama pamoja na dada zangu, mgogoro wa mirathi ya nyumba iliyoachwa na baba yangu, Elias Clian, baada ya kufariki dunia mwaka 2005, ndio unanitesa,” amesema.