Wiki takribani tatu zilizopita niliandika makala kuhusu fursa ya kilimo cha miti. Nina furaha kubwa kuwajulisha kuwa watu wengi wamekuwa na mwitikio mkubwa na wamechangamkia fursa ile. Ninapenda kuwatambua ndugu wawili (sitawataja majina) ambao wiki iliyopita walisafiri kutoka Tabora hadi hapa Iringa kuwahi fursa ya kilimo cha miti.

Nilizunguka na ndugu hawa katika vijiji na mashamba mbalimbali na walionekana kuhamasika sana. Ndugu hawa nimewasaidia hadi wamefanikiwa kupata shamba lenye ukubwa wa ekari 40 katika Kijiji cha Igeleke wilayani Mufindi kwa ghamara inayokaribia Sh  milioni tano!


Baada ya makala ile kutoka, jamaa mwingine alisafiri siku mbili kutoka Lindi hadi hapa Iringa na akafanikiwa kununua shamba la miti yenye umri wa miaka minne; lenye ukubwa wa ekari tano kwa gharama ya milioni 2.5! Ukweli ni kuwa fursa hii ni pana na ina mambo mengi mazuri ambayo nafasi haikutosha kuyaandika yote katika makala ile.


Waliofika Iringa kutoka mikoa mbalimbali kuchangamkia fursa hii ni mashahidi na wengi wameondoka na utajiri. Kiukweli baada ya kushirikisha fursa ile na kuahidi kuwasaidia watu; nimekuwa “bize” sana. Nina miadi (appointments) nyingi kupindukia za watu kutoka mikoa mbalimbali wanaotaka kuja kuwekeza Iringa katika kilimo hiki. Milango ingali wazi, karibuni shambani mtajirike! Katika siku za usoni nitaendelea kuwashirikisha fursa nyingi za kijasiriamali kutoka sekta mbalimbali.


Leo ninataka nitupie jicho katika eneo la namna mjasiriamali unavyoweza kulinda biashara zako kwa kuwa na mbinu za kutafuta, kuajiri na kukaa na wafanyakazi bora. Uzoefu unaonesha kuwa biashara nyingi huyumba kutokana na uzembe, udokozi, wizi na hujuma zinazofanywa na watu tunaowaajiri katika biashara zetu.

 

Kila mahali ninapofanya, kuandika ama kufundisha ujasiriamali nimekuwa nikiweka msisitizo katika eneo la mjasiriamali kuhakikisha anakuwa na fedha na muda wa kutosha. Hakuna maana ya kuwa na fedha nyingi halafu ukose muda kwa sababu kamwe hutafurahia maisha yako.

 

Ukiacha hilo la kuwa na fedha na muda wa kutosha, kuna kitu kingine kinachojitokeza kiuhalisia. Hiki ni kuongezeka kwa wanaokula mali zako kwa kadiri unavyozidi kukua kibiashara. Hili halikwepeki hata kidogo. Ninachotaka tukiangalie hapa ni namna ya kudhibiti hawa walaji ili angalau ulaji wao usilete hasara katika biashara zetu.


Kutokana na mambo hayo mawili (kufurahia maisha kutokana na biashara zako na kuwadhibiti walaji wa mali zako), ndipo tunapokuja kwenye “pointi” ya msingi ambayo ni umuhimu wa kuajiri watu katika biashara. Ili uwe na muda wa kutosha ni lazima uajiri watu wakufanyie kazi (money working for you), lakini ili uepukane na suala la kuwanufaisha watu (walaji wanaoweza kukuibia kupita kiasi), inatakiwa kufahamu mbinu za hali ya juu za kuajiri na kusimamia wafanyakazi.

 

Ninapotaja kuajiri wafanyakazi ninafahamu kuwa kuna wajasiriamali wataanza kujitoa wakifikiri kuwa wao hawajafika katika hatua ya kuajiri. Mfanyakazi ni mfanyakazi, hata kama una banda la nyanya na ukawa na msaidizi (kibarua) wa kukusaidia, huyo moja kwa moja ni mfanyakazi. Mtu unayefanya naye biashara (hata awe ni mke wako ama ndugu yako) anatakiwa kuwa katika kundi la wafanyakazi wako.


Nafasi ya wafanyakazi utaiona pale aidha wanaposaidia kung’arisha biashara yako ama wanapochangia kufilisika kwako. Wapo wajasiriamali wengi waliorudishwa nyuma na wafanyakazi ‘wabaya’. Kama ni duka kuna mtu unaweza kumuajiri kumbe anachota pesa kuliko hata faida inayokusanywa. Unapokuja kushtukia unakuta hasara kubwa ama kuanguka kabisa kwa mtaji.


Kutokana na hatari kama hizo hapo juu, kuna wajasiriamali wanaoamua kushughulika wao wenyewe bila kuajijri watu. Wengine hupendelea kuwatumia wanafamilia (watoto, mume, mke ama ndugu) wakidhani kuwa hiyo ndiyo salama yao. Huwa nawasikia wajasiriamali wakisema, “Bora umuweke ndugu yako, akikuibia utakuwa umesaidia ukoo”. Hizi ni kauli za waliokata tamaa. Pia ni vema kufahamu kuwa bila kufanya kazi na watu ‘sahihi’ ni vigumu kukua kibiashara.


Kwanza inabidi kufahamu kuwa hakuna watu waliozaliwa kuwa wafanyakazi bora ama wafanyakazi wabaya. Watu wote wanatengenezwa kutegemea na mazingira ya kazi. Kwa maana hii hakuna ‘garantii’ kuwa eti ndugu, mke wako ama familia yako watakuwa wasaidizi bora katika biashara zako.


Isipokuwa unatakiwa kuwa na mbinu sahihi za namna ya kuwapata watu makini watakaobeba uchungu kama ulionao wewe katika biashara zako. Hivyo iwe ni watu unaohusiana nao kiundugu ama usiohusiana nao, wote unatakiwa kuwaajiri ama kufanya nao kazi kwa welevu mkubwa.


Suala la kuwapata wafanyakazi makini linatakiwa kuanza na wewe kubaini tabia ama hulka za watu zitakazoendana nao katika mawazo na uamuzi wa kibiashara. Jambo la pili ni kuangalia matakwa yao ya ndani (motivations drives) na la mwisho ni uwezo wako wa kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kukaa nao kwa muda mwafaka.


Kuna tofauti kubwa ya kimbinu unaposhughulika na wafanyakazi waliosoma na ambao hawajasoma, kati ya wajanja (wa mjini) na washamba (wa kutoka kijijini). Ngoja niioneshe tofauti hii katika kipengele cha mshahara kati ya wasomi na wale ambao hawajasoma.


Unapomwajiri mfanyakazi ambaye hajasoma unaweza kuamua kumlipa mshahara wa labda shilingi laki mbili, bila kumpa mchanganuo wowote na akafanya kazi kwa bidii na kuleta matokeo unayotarajia. Lakini unapompa kazi ile ile msomi, ili afanye kazi kwa matokeo unayotarajia ni lazima uongeze mbinu nyingine ya kisaikolojia.

 

Kwa kuwa wasomi (kwa asili) wanapenda kutambuliwa thamani ya elimu zao (hata kama ni kidato cha nne), kuna mbinu nyingi za kutumia lakini mojawapo ni hii. Unachotakiwa kufanya ni kutoa mchanganuo wa kisomi wa mshahara utakaomlipa (tuchukulie umepanga kumlipa shilingi laki mbili, sawa sawa na yule ambaye hajasoma ama ana elimu ndogo kuliko yeye).


Unamwambia hivi; “Nitakulipa mshahara wa 150,000, lakini nitakuongezea gharama ya nyumba 30,000, usafiri nitakupa 10,000 na mawasiliano nitakulipa 10,000. Mchanganuo huu unaleta hesabu ile ile ya shilingi laki mbili, lakini mfanyakazi huyu atafanya kazi kwa moyo akijua kuwa kumbe kampuni ama uliyemwajiri unayajali hata maisha yake binafsi kama malazi, mawasiliano na usafiri. Ukifanya hivi unakuwa ‘umemroga’!


Vile vile ili kuboresha ari ya wafanyakazi kufanya kazi na kujiona kuwa wana hadhi ni vema kutengeneza vyeo katika biashara zako. Kwa mfano, unaweza kuwa na biashara ya duka, halafu ukawa na mfanyakazi wa stoo, ukawa na anayeuza ndani, ukawa na unayemtuma mara kwa mara benki na akawepo anayesambaza bidhaa kwa wateja. Badala ya kuwaacha wafanyakazi wote hawa bila majina ya vyeo, jambo zuri ni kuwapachika vyeo.

 

Yule anayeuza ndani unaweza kumpa cheo cha Afisa Mauzo (sales officer), aliyepo stoo mpe Mratibu wa Stoo (store keeper), anayepeleka fedha benki, mwite mhasibu (accountant), anayesambaza bidhaa kwa wateja, mwite afisa masoko na usambazaji (marketing and distribution officer). Vyeo hivi ikibidi vichapishe katika karatasi na ubandike katika ofisi za duka ama shughuli zako na pia uwatengenezee vitambulisho.


Kimsingi vyeo hivi havitaathiri kiwango cha mshahara unachowalipa kwa sasa, lakini vitaleta mabadiliko makubwa kihamasa. Itakuwa ni fahari kwa mfanyakazi anayesambaza bidhaa kwa wateja, pale anapojitambulisha hata kwa familia yake kuwa yeye ni afisa usambazaji wa labda “Sanga Shop”. Badala ya hadhi ya kibarua anayoendelea kuwa nayo kabla ya kuundwa kwa vyeo hivyo.


Jambo jingine la msingi ni namna unavyotengeneza kanuni na sheria za kushughulika na wafanyakazi wanapofanya makosa. Kuna baadhi ya wajasiriamali ambao mitindo wanayotumia kuwadhibiti wafanyakazi ndiyo inayosababisha waibiwe zaidi na zaidi. Wengi wa wajasiriamali wanaogopwa, hawana urafiki na wafanyakazi, wanaishi kama paka na panya.


Mfanyakazi katika biashara ama shughuli zako mara nyingi anafahamu kiwango cha faida unayoingiza kwa siku ama mwezi, ‘unaporogwa’ na kumlipa mshahara kiduchu kuna mambo mawali yanatokea. Mosi unampunguzia morali ya kufanya kazi kwa bidii, pili unamwingiza katika mafunzo ya tamaa na mbinu za kukuibia. Mkono wa birika haufai hata kidogo kwa watu tunaofanya nao kazi na wanaotuingizia faida.


Unapofanikiwa kutafuta, kuajiri na kubaki na wafanyakazi bora unakuwa na nafasi ya kukua kibiashara huku ukiendelea kupata faida. Pamoja na kuwa kadiri unavyokua kibiashara wanaofaidi mali zako nao wanaongezeka (wafanyakazi na washirika), lakini unapokuwa na mfumo bora wa wafanyakazi, unakuwa na nafasi ya kuwa mwenye fedha na muda wa kutosha.


Wajasiriamali tunahitaji ushindi katika kulinda mali zetu.

[email protected] 0719 127 901