Yakomba majokofu mawili, televisheni, deki
Pia jenereta kubwa kwa deni la Sh. 600,000
Mama aona maisha magumu, ataka kujiua
Malalamiko dhidi ya Benki ya FINCA Tanzania, Tawi la Geita, kwamba inanyanyasa wajasiriamali, yamemuibua mjane aliyeeleza alivyoporwa kwa mabavu vitu vyake vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 1.65 kabla ya kuuzwa kwa bei ya Sh 600,000.
Kwa mujibu wa mlalamikaji huyo, Magati Ally Liku, vitu vilivyochukuliwa ni jokofu, televisheni aina ya Hitachi aliyoinunua mwaka 2008 kwa Sh 450,000; jokofu dogo alilolinunua kwa Sh 400,000 mwaka 2011.
Kadhalika, jenereta kubwa aliyoinunua mwaka 2012 kwa Sh 500,000; televisheni ya inchi 14 aliyoinunua kwa Sh 130,000 na deki ya DVD aliyoinunua kwa Sh 150,000 — ambavyo kwa pamoja alivinunua mwaka 2010 wakati huo akiwa na mume wake.
Mwanamke huyo ameibuka ikiwa ni wiki moja tu tangu gazeti hili liliporipoti taarifa za mjasiriamali Kipara Ng’wendesha aliyedai kuporwa pikipiki yake kutokana na deni la Sh 26,359.22, hali inayochangia kudidimiza uchumi wa wajasiriamali.
Mwanamke huyo mkazi wa Mtaa wa Kampaundi, Kata ya Mtakuja wilayani Geita mkoani hapa, ambaye pamoja na malalamiko hayo ameiomba Serikali kuingilia kati ili FINCA warudishe vitu vyake ili naye alipe deni.
Liku anadai kuwa angejua mapema kwamba FINCA Tanzania, Tawi la Geita, imevaa ngozi ya kondoo wakati matendo yake ni ya mbwa mwitu, asingethubutu kuchukua mkopo kwani umembadilisha na kuwa masikini.
Ilikuwaje?
Akisimulia mkasa wote alipozungumza na JAMHURI, Liku anasema Agosti 2013 wakati mumewe akiwa hai, walijaza mkataba wa mkopo kwenye Benki ya FINCA na kuelezwa pesa ingetoka ndani ya wiki tatu.
Wakati wanasubiri mkopo huo, mumewe alianza kuugua na kufariki dunia baada ya muda mfupi Septemba 9, 2013. Tukio hilo lilikwenda sambamba na kumpoteza mama yake aliyefariki dunia Septemba 22, mwaka huo.
“Msiba wa mama ulinifanya nichanganyikiwe…nisijue la kufanya maana baada ya kuondokewa na mume wangu tegemeo pekee lilibaki kwa mama,” anasema Liku huku akibubujikwa na machozi na kudai “Natamani kufa.”
Novemba 27, 2013 alipata taarifa za kutakiwa kuonana na Meneja wa FINCA, Francis Kazaura, aliyehoji ukimya wa mwanamke huyo kutofuatilia mkopo. Liku anasema alimweleza matatizo ya kufiwa yaliyompata.
“Alinifariji na baadaye kunisihi kuchukua mkopo,” anasimulia Liku ambaye kutokana na matatizo yaliyompata hakuwa na haja tena ya kuchukua mkopo huo akihofia kuongeza matatizo juu ya matatizo kwani tayari biashara yake ilikwishaanza kudorora.
“Alinisihi sana nikubali kuchukua mkopo ule. Akasema taasisi yao inajali watu kama mimi na kunihakikishia mkopo ule utainua biashara yangu ambayo kwa wakati ule ilikuwa imeyumba kwa kiasi kikubwa, mwishowe nikawa nimekubaliana naye nikiamini maneno yake matamu kama asali,” anasema.
Yeye na hayati mume wake waliomba mkopo wa Sh 2,000,000 lakini alipewa Sh 1,950,000 baada ya makato. Alitakiwa awe anafanya marejesho ya Sh 225,000 kila mwezi.
Kwa mujibu wa Liku, mwezi uliofuata yaani Desemba 27, 2013 mpaka Mei 27, 2014 alikuwa akipeleka marejesho hayo bila ya kukosa kabla ya mwanaye mmoja kuugua, hali iliyomlazimu kufunga biashara na kuhangaikia tiba, lakini FINCA walimkejeli baada ya kupata taarifa.
Akinukuu maneno aliyoelezwa FINCA, Liku anasema, aliambiwa: “Dada usilete mchezo na hela ya FINCA, aliyekuambia FINCA inauguliwa ni nani?”
Anasema, wakati akiendelea kuuguza mwanaye, asubuhi Oktoba 1, 2014 alivamiwa na maofisa wa FINCA, na baada ya mazungumzo aliamuriwa kupeleka Sh 400,000 itakapofika saa 6 mchana ya siku hiyo.
“Walisisitiza kunifilisi pamoja na viongozi wangu wa mtaa kuwasihi na kuwaeleza matatizo niliyonayo hawakuelewa na walisisitiza kuwa FINCA huwa haiuguliwi wala kufiwa, wanachotaka wao ni hela na si porojo,” anasema.
Kauli hiyo iliamsha kidonda cha uchungu na kuanza kujutia mkopo huo na kujilaumu kushindwa kutii mawazo yake ya awali yaliyomkataza kuchukua mkopo kabla ya kushawishiwa na Kazaura.
Kutokana na hali hiyo, alimfuata jirani yake, aliyemtaja kwa jina la George aliyemkopesha Sh 120,000 na kuzipeleka ambazo hata hivyo hazikutosha kwani siku tano baadaye, Oktoba 6, 2014 maofisa wale walimfuata tena.
Baaba ya kufika, waliingia ndani ya duka na kuanza kubeba vitu, bila hata kuona uongozi wa mtaa anakoishi huku yeye akikimbia kumwita balozi wa eneo hilo kushuhudia kinachofanywa na maofisa hao.
“Balozi wangu alipofika, mbali na kuhoji kulikoni hakusikilizwa zaidi ya maofisa wale kutuporomoshea matusi ya nguoni,” anasema Liku na kuongeza kuwa Oktoba 10, 2014 zikiwa zimepita siku nne tu tangu wabebe vitu hivyo, mmoja wa maofisa wa FINCA alimpigia simu kumtaarifu kuwa vimeuzwa kwa Sh 600,000 na deni analodaiwa liko palepale ambalo ni Sh milioni 1.1.
“Niliambiwa kama sikulipa watakuja kusafisha duka lote, masufuria, godoro na vitanda ninavyolalia mimi na watoto wangu,” anasema Liku huku akihoji kiwango hicho cha deni cha Sh milioni 1.1 ilhali alichokopa ni Sh 1,950,000. Tayari alikuwa amelipa Sh 1,350,000 na deni ambalo analitambua ni Sh 600,000.
Liku anasema kwamba alipohoji sababu za kudaiwa tena ilhali vitu walivyouza vinazidi deni la Sh 600,000, akaambiwa kwamba fedha hiyo ni adhabu na deni lingali liko palepale, kauli iliyomfanya azidi kuchanganyikiwa.
“Nilikata simu yao na kujiinamia huku nikilia kwa uchungu, akili ya kujiua ikitawala mawazo yangu na ndipo mwenyekiti wangu wa mtaa alipofika na kuanza kunifariji na kunisihi nitizame watoto nilioachiwa na mume wangu na si kitu kingine maana kila jaribu huwa na mlango wa kutokea,” anasema huku akionekana kuwa na mawazo.
Anasema, “Kilichonifanya niwaze, kwanza ni FINCA kuuza vitu vyangu bila kunishirikisha tena kwa bei ya hasara, na kingine ni kuhusu mkataba wa kumaliza mkopo wao, maana mkataba ulikuwa haujaisha, kwani nilichukua mkopo Novemba 27, 2013 na mwisho wa kulipa deni lote ilikuwa Novemba 27, 2014 lakini nafilisiwa Oktoba 6, 2014 kabla ya kumaliza mkataba, nililia sana.”
Kutokana na hali hiyo, alikwenda ofisi za FINCA kutaka apewe maandishi yanayothibitisha vitu vyake kuuzwa kwa bei ya kutupa, lakini alinyimwa huku wakimtishia kurudi tena nyumbani kwake kwa ajili ya kumchukulia kila kitu, hali iliyomlazimu kutoka ofisini kwao akiwa mnyonge huku akihisi mshono wake wa upasuaji wakati akijifungua wanawe ukifumka.
“Hapa nilipo nimebaki yatima, sina mama wala baba, na sina mume nimebaki na watoto wawili — Juliana James (5) na Lightness James (2), kodi ya pango la nyumba na duka nalipia Sh 960,000 kwa mwaka. FINCA hao.
Je, alielimishwa?
Akizungumzia namna wanavyochukua mkopo huo, Liku anadai hakupewa elimu yoyote kabla ya kuchukua mkopo.
“Mtu hapewi elimu yoyote kabla ya kuchukua mkopo, kinachofanyika ni kujaza fomu, unalipa pesa ya ada kulingana na mkopo unaouhitaji; kwa mfano mimi katika milioni mbili nilitoa ada ya Sh 50,000 nikapatiwa mkopo,” anasema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kampaundi, Kata ya Mtakuja wilayani Geita, Mariam Minyami, ameiomba Serikali kuchunguza utitiri wa taasisi za fedha wilayani Geita kwa kile alichodai zimekuwa kero kubwa kwa jamii.
“Kama hazitafuatiliwa kuna hatari ya kutokea uvunjifu wa amani na kuzalisha Taifa la watoto wa mitaani kutokana na wazazi kuzikimbia familia wakihofia kukamatwa na kufilisiwa mali inapotokea wameshindwa kulipa mikopo husika,” anasema Minyami.
“Kwa kweli kama hawa FINCA wanapaswa kuchunguzwa maana hawafuati kabisa haki za binadamu, hawajui kama kuna kukwama, kuuguliwa wala kufiwa, mimi ni kiongozi wa watu nimeshuhudia mambo makubwa sana yanayofanywa na hizi taasisi za fedha ikiwamo FINCA,” anasema.
“Taasisi hizi zimevunja ndoa nyingi sana, uaminifu wa fedha haupo kabisa na mbaya zaidi hawawapi hata elimu ya ujasiriamali wateja wao. Yaani kama FINCA haijali utu wa mwanadamu na ndiyo maana hapa Geita watoto wengi wamegeuka chokoraa kwa sababu wazazi wanakimbia madeni yao hapa,” anasema.
Akizungumzia madai ya Liku, Meneja Francis Kazaura anasema: “Mara nyingi kinachotokea huwa ni makubaliano kati ya maofisa wa FINCA na mteja husika na kila kitu kinakuwa chini ya kontro ya mteja. Na baada ya mnada na kinachobaki baada ya kulipia marejesho tunaangalia utaratibu kwa hiyo deni kupunguzwa.”
“Kuna wateja tulikuwa tunawadai wengine walikuja na ‘laptop’ tukauza wakalipa madeni yao hapahapa, kwa hiyo ni maamuzi ya mteja mwenyewe lakini mteja hawezi akalazimishwa kutoa vitu au kitu kikabebwa bila ridhaa yake,” anasema.
“Kuuzwa vitu vyake pasipo yeye kuwapo hapana kinachofanyika mteja anapoleta dhamana zile bidhaa zinakuwa na thamani yake anaambiwa, kwa hiyo wewe umeleta hivi vitu kwa hiyo sasa sisi tunahitaji hela, kwa hiyo baada ya siku tano uje hapa sisi tunauza,” anasema na kuongeza kwamba taasisi yake inakuwa kwenye nafasi ya kuuza bidhaa hizo baada ya siku tano ikitokea mteja haonekani.
Lakini, Nsia Mananda ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Kitengo cha Wanawake na Watoto, ndani ya Idara ya Maendeleo, Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Halmashauri ya Mji wa Geita, anasema tayari Serikali imeanza mkakati wa kupunguza matatizo ya wananchi kujiingiza kwenye mikopo isiyokuwa na manufaa kwao.
Mkakati huo ulianzishwa rasmi kwenye mwaka wa fedha 1993/1994 ukiwa na lengo la kuwainua wanawake wajasiriamali kiuchumi pamoja na vijana. Kabla ya Serikali kuwakopesha, wanatakiwa wawe katika vikundi vya watu watano na hukopeshwa kupitia makusanyo na mapato ya ndani ya halmashauri husika.