DAR ES SALAAM
NA MICHAEL SARUNGI
Mary Njogela (70), mjane anayehifadhiwa kwenye jumba bovu lililoko Mikocheni ‘B’ jijini Dar es Salaam baada ya kuondolewa kwa nguvu na watoto wa kufikia wa marehemu mume wake, anaomba msaada wa Serikali ili arejeshewe mali hiyo.
Amesema nyumba aliyonyang’anywa alikuwa akiishi na mumewe, Said Hamza (marehemu) kwenye kiwanja namba 483, kilichopo kitalu ‘B’ huko Mikocheni ‘B’, akiwa mlezi wa watoto hao (majina tunayo) anaodai kuwalea baada ya kuachika kwa mama yao.
Kwa mujibu wa Njogela, ambaye afya yake inadhoofika kutokana na kusumbuliwa na miguu iliyosababishwa na ajali ya pikipiki, nyumba nyingine waliijenga kwenye kiwanja namba 221, kitalu ‘F’ maeneo ya Msasani jijini humo.
Njogela anasema alifunga ndoa ya kiserikali na mumewe huyo mwaka 1979, wakati huo alimkuta (mume) akiwa na watoto wawili, akazaa naye mtoto mmoja aliyefariki na hakupata mwingine, hivyo akaendelea kuwalea watoto wa mke wa kwanza.
“Alipofariki mume wangu, watoto wa mke wa kwanza kwa kupewa ushauri na ndugu zao wasonitakia mema waliamua kunitoa kwenye nyumba niliyoshiriki kuijenga kwa nguvu,” amesema Njogela.
Amesema alikwenda Ofisi ya Serikali ya Mitaa ya Mikocheni ‘B’ kushughulikia hatua za awali kwa masuala ya mirathi, lakini kutokana na tofauti za kidini kati yake na walalamikiwa, hakuna uamuzi uliofikiwa. Anasema yeye ni Mkristu wakati walalamikiwa Salma Said na Hamza Said ni waumini wa dini ya Kiislamu.
Njogela amesema baada ya hali kuwa hivyo, ofisi hiyo ilimshauri kutafuta msaada wa kisheria, ndipo alipokwenda Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) waliompa mwanasheria kutoka kampuni ya uwakili ya White Law Chambers ya jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Mikocheni B, Mariam Ngasa, amesema mgogoro huo ulishafika ofisini kwake na walishindwa kuupatia ufumbuzi kutokana na tofauti ya dini iliyojitokeza.
“Rekodi tulizonazo zinaonesha kuwa marehemu kabla ya kifo alikuwa na wake wawili japo alimuoa Mary Njogela. Huyo mwingine (bila kumtaja jina) alikuwa ameachana naye zaidi ya miaka mitatu na hakuwa ametoa talaka,” amesema Ngasa.
Njogela amedai kuwa walifungua kesi namba 37 ya 2010 iliyokuwa chini ya Jaji wa Mahakama Kuu, Fredrica Mgaya, lakini hata hivyo kesi ilipokaribia kutolewa hukumu pakatokea ubishani wa kisheria kati ya mawakili wa pande zote, mwisho ikaamuliwa kuwa ilikosewa kwa kisheria kwa hiyo ifutwe na kufunguliwa upya.
Kwa mujibu wa Njogela, kesi hiyo ilifutwa na Jaji Mgaya Agosti 28, 2013 na kuamuriwa ifunguliwe upya, lakini kutokana na kukabiliwa na maradhi alishindwa kuendelea nayo.
TLS YANENA
Afisa Mipango wa TLS, Rose Salvatory, amethibitisha kumtambua mjane huyo kuwa mmoja wa wateja waliofika kuomba msaada wa kisheria na kwamba mara ya mwisho (Njogela) alikwenda ofisi kwake akimlalamikia wakili wake.
Amesema walimshauri akachukue faili la kesi yake kuliwasilisha TLS kwa ajili ya msaada zaidi, lakini hakurejea. Salvatory amesema, kwa kawaida mteja anapopewa wakili wa kumtetea anapaswa kurudisha mrejesho TLS kuhusu mwenendo wa kesi yake, hali ambayo haikutokea kwa Njogela.
Wakili wa White Law Chamber aliyemwakilisha mjane huyo kwenye shauri kupitia msaada wa TLS, Mathias Kisegu, amesema anachokumbuka ni ‘kushindana’ na mteja huyo katika mwenendo wa shauri hilo.
“Ni kweli niliwahi kuwa wakili wake, lakini tulishindwana, akachukua faili lake nami sikufuatilia kilichoendelea juu ya kesi hiyo,” amesema Kisegu.
JAMHURI limemtafuta na kumpata Hamza Said, mtoto wa marehemu ambaye pia ni mmoja wa walalamikiwa wanaodaiwa kumtoa kwa nguvu kwenye nyumba mjane, lakini hakutaka kutoa ushirikiano kwa kujifungia ndani ya nyumba.
mwisho