Mmoja wa wakurugenzi wastaafu wa idara iliyoshika moyo wa nchi (jina linahifadhiwa) ametajwa kushirikiana na baadhi ya Maofisa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuandaa mpango wa kumpokonya kiwanja mkazi wa Ilala, jijini Dar es Salaam, Habiba Mtema, JAMHURI limearifiwa.

Mkurugenzi huyo anatajwa kushirikiana na Msajili Mkuu wa Hati, Subira Sinda na Afisa Ardhi, Apolo Laizer ambaye sasa amehamishiwa kikazi mkoani Mbeya kubatilisha hati ya umiliki wa kiwanja chenye ukubwa wa ekari tano ambacho, Habiba Rashid (57) anasema ni chake.

Habiba ameliambia JAMHURI kuwa watumishi wa Serikali wameunda mpango wa kubatilisha umiliki wake wa kiwanja Na 34 kilichopo Mikocheni ‘B’ eneo la viwandani, jijini Dar es Salaam na kulihamishia kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais.

Habiba amesema kiwanja hicho ambacho marehemu mume wawe alikipata kutoka Manispaa ya Kinondoni, Julai 17, 1983 kwa barua ya toleo yenye Kumb Na. A/KN/A/13641/3/MHKN kupitia jina la Marine and Farm Products Ltd kimebatilishwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Ardhi kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais kwa jina la Tanzania Transport and Taxi Servises (TTTS), taasisi ambayo indadaiwa kuwa ilikuwa inafanya kazi chini ya uangalizi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Habiba anamtaja Mkurugenzi huyo kuwa na maslahi binafsi na kiwanja hicho na kwamba amediriki kushirikiana na maofisa Ardhi Kinondoni na makao makuu kutengeneza nyaraka ambazo zinaonyesha kuwa kiwanja hicho ni mali ya TTTS kupitia barua ya toleo ya Novemba 21,1978 yenye Kumbu No. D/KN/A/13611/1/TMM.

“[Afisa Ardhi] aliniambia kuwa hiki kiwanja unachokihangaikia kuna mkubwa hapa anasema ni cha kwake.Nikamuuliza mkubwa huyo ni nani?Akaniambia hawezi kunitajiaNikamwambia ndugu yangu hapa duniani anayeogopwa ni Mungu peke yake anayenifanya mimi na wewe tunahema.

 “Kwa bahati nzuri nikafanikiwa kumpata msamalia mwema akaniambia atanisaidia kuonana na huyo mkubwa. Nikapelekwa,nilipofika,kumwona tu yule bwana nikajitambulisha. Akaniambia hauna haja ya kujitambulisha wewe si mama Mtema?  Nikamwambia, baba yangu mimi nimekuja kukulilia. Kilichotokea wewe unakifahamu. Mwaka 2012 ulituma watu waje kunivunjia wakati mimi nalipa kodi kwa eneo langu. Unanivunjia bila sababu aliyekutuma ni nani? Akaniambia mimi bwana kile kiwanja nakijua vizuri. Kile kiwanja ni cha Mtema, lakini nikikuandikia kimemo saa hizi uende upewe kiwanja chako huu mtandao wangu nitaueleza nini? Nikamwambia mimi mtandao wako haunihusu. Mimi ninachojua kile kiwanja ni changu na mume wangu ambaye saizi (sasa hivi) ni marehemu.

“Akaniambia kuna gharama zangu nimeziweka pale. Nikamjibu pia mimi gharama zako hazinihusu. Mimi sikukwambia uje univunjie.  Maana kama wewe ungekuwa mstaarabu ungekuja ukaniambia mama hiki kiwanja labda kina ‘interest’ (maslahi) na Serikali.  Unaitwa twende tukafanye mazungumzo na Rais labda, wanataka kwa ajili ya shughuli za kijamii mimi ningekuelewa. Kwahiyo maana yake unakitaka wewe binafsi unidhulumu kwa maslahi yako wewe na wakati kiwanja ni changu na watoto nimeachiwa na mume wangu?”anasema Habiba.

Habiba anasema walibishana kwa muda mrefu bila kupata mwafaka akalazimika kuondoka. Hakuishia hapo aliamua kurudi wizarani aweze kusaidiwa, lakini aligonga mwamba.

Msajili Mkuu wa Hati, Subira Sinda, amekiri kumfahamu Habiba Mtema na kwamba alishafika ofisini kwake kutoa malalamiko yake juu ya kiwanja hicho.

Alipoulizwa kuhusu shutuma kutoka kwa Habiba kwamba yeye na watumishi wenzake hapo wizarani wameshirikiana kubatilisha umiliki wa kiwanja hicho kwenda ofisi ya Rais kupiti idara nyeti, amesema yeye si mtoaji wa hati.

“Mimi sitoi hati, anayetoa hati ni Kamishna wa Ardhi. Mimi naletewa tu hati ambazo zipo tayari kukamilika na zimepigwa muhuri ili mimi niziidhinishe. Sina mamlaka ya kutoa hati. Alikuja huyo mama siku zimepita, akanieleza mgogoro huo nikamwambia kuwa amuone Kamishina wa Ardhi iwapo ana malalamiko ya kubatilishiwa umiliki wa kiwanja chake,” anasema Sinda.

Alipoulizwa kuhusu madai kwamba alimwambia Habiba hawezi kumsaidia kwa sababu amekwishapokea maagizo ya ‘mkubwa’ kuwa eneo hilo analihitaji mkubwa huyo, Sinda alikanusha.

“Anasema uongo. Mimi sijawahi kuambiwa na mamlaka yoyote ya juu kuwa nisishughulikie suala hilo na nilimwambia huyo mama mimi siyo Kamishna ni Msajiri tu, hivyo siwezi kufanya hivyo maana sitoi hati,” amesema Sinda.

Sinda amekiri kuwa Laizer ni mfanyakazi wizarani hapo ambapo amehamishiwa Mbeya kwa sasa ila amekanusha Laizer  kuhusika kubatilisha umiliki wa kiwanja chake.

Awali Habiba Mtema alilieleza JAMHURI kuwa ameandika barua ya kuomba kumwona Rais Dk. John Magufuli aingilie kati suala hilo kutokana na baadhi ya vigogo wa Ikulu wa Awamu ya Tatu na Nne (majina tunayahifadhi kukiri kuwa kiwanja hicho hakipo kwenye orodha ya viwanja ambavyo vipo chini ya Ofisi ya Rais, lakini hawakumsaidia.

Amesema barua hiyo aliiwasilisha kwa Sekretari aliyepo kwenye lango kuu la kuingia Ikulu Januari 20, 2017. Na kwamba, alifahamishwa kwa njia ya barua pepe kuwa barua yake ilipolewa siku mbili baada ya kupekwa.

JAMHURI limewasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa aliyesema jambo hilo ni geni kwake hivyo hawezi kulitolea ufafanuzi.

“Mbona hizo taarifa mimi bado hazijanifikia? Labda nitajaribu kuuliza kama barua ipo, ila bado haijaletwa kwangu. Lakini hata hivyo masuala hayo yanatakiwa kupelekwa Wizara ya Ardhi na kama hakuna uwezekano yatapelekwa mahakamani. Mimi nitafuatilia habari za kiwanja hicho na nitakujulisha zikiwa tayari,” amesema Msigwa.

Awali Habiba alilieleza JAMHURI kuwa baada ya hukumu ya Desemba 15,2016 kutolewa na Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi na umiliki wa kiwanja kutolewa kwa jina la Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais, aliamua kurudi kwa Waziri wa Ardhi kulalamikia hukumu ile kuwa haikuwa ya haki ambapo Waziri William Lukuvi alimshauri aende Mahakama ya Rufaa.

Hata hivyo, Habiba anasema kuwa hana fedha ya kuendesha kesi mpya na hivyo anamuomba Rais Magufuli aingilie kati mgogoro huo.

Pamoja na hukumu hiyo kutolewa, Desemba 18,2016 Habiba alipokea notisi kutoka kwa Kamishna wa Ardhi Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi ikimtaka kulipa kodi ya kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na malimbikizo yake kiasi cha Sh milioni 7,168,342.44.

Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam, Nathaniel Nhonge alipoulizwa kuhusu ofisi yake kumpelekea notisi ya malipo ya kodi ya mwaka 2016/17 ilihali Habiba siyo mmiliki tena wa kiwanja hicho baada ya hukumu ya Mahakama Kuu alishindwa kutoa ufafanuzi.

“Leo tuna kikao kikubwa na Waziri, hatuwezi kuzungumza lolote. Kwanza suala lenyewe linahitaji kueleweshana kwa kufungua mafaili. Njoo wiki ijayo nitakueleza kwa nini alitumiwa notisi hiyo,” anasema Nhonge.

JAMHURI limefanya juhudi za kumpata Mkurugenzi mstaafu bila manfanikio.

Habiba Mtema amesema baada ya kugundua kuwa zipo mbinu za kutaka kumdhulumu kiwanja chake kwa hila na madai kuwa mmiliki wake ni Usalama wa Taifa alikimbilia mahakamani kufungua kesi namba 347 ya mwaka 2013 akiwashitaki 1.Mkurugenzi wa Manispaa Kinondoni, 2.Kamishina wa Ardhi, 3.TTTS na 4.Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kula njama za kutaka kubatilisha na kumdhulumu kiwanja chake (ambapo mshitakiwa/mlalamikiwa namba 2 hadi 4 waliunganisha nguvu katika shauri la kesi hiyo) na kampuni nyingine ya .H.H.Hilal and Company Ltd, ambayo ilikuwa mlalamikiwa Na. 5 kwa kutaka wamilikishwe kiwanja hicho baada ya kuingia makubaliano ya kukinunua na mlalamikaji.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi, na hukumu yake kutolewa na Jaji J.J.Mwangesi Desemba 15, 2016, Jaji Mwangesi aliieleza Mahakama kuwa mlalamikaji alidai kupata kiwanja hicho kutoka kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Julai 17,1983 kwa barua ya toleo yenye kumb.A/KN/A/13641/3/MHKN.

Alisema wakati mlalamikaji akiwa katika mchakato wa kupata hati yake, aliingia makubaliano ya kuuza kiwanja hicho na mlalamikiwa namba 5. Hata hivyo, aliieleza Mahakama kuwa wakati yakitokea hayo mlalamikiwa namba 3 alikuwa tayari akimiliki barua ya ofa yenye kumb.D/KN/A/13611/1/TMM ya Novemba 21,1978 kutoka Halmashauri ya Kinondoni.

Jaji alihitimisha kesi hiyo kwa kusema kuwa kutokana na ushahidi wa pande zote ulivyowasilishwa umiliki wa kiwanja hicho ni wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais.

Habiba Mtema anadai kuwa hukumu hii imetolewa kwa kumuonea na kwamba Tanzania Transport and Taxi Services imetumika kuhalalisha dhuluma hiyo.