Shule ya Filbert Bayi iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, mwaka jana iliruhusu mwanafunzi mjamzito kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu Kidato cha Nne.
Mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) alifanya mtihani huo kwa namba S 1437/0002 katika matokeo ya mtihani yaliyotangazwa Januari mwaka huu, alifaulu kwa kupata daraja la pili lenye alama 20 (Division II, 20).
JAMHURI limeelezwa wakati anakutwa na mimba hiyo ilikuwa imekwisha kutimiza miezi saba na kwamba kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 16.
Mwanafunzi huyo inadaiwa kuwa alibainika kuwa mjamzito zikiwa zimebaki siku chache za kufanya mtihani wa taifa.
Mmoja wa wafanyakazi wa shule hiyo ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini ameliambia JAMHURI kuwa kubainika kwa mwanafunzi huyo kulitokana na utaratibu wa kupima afya za wanafunzi shuleni hasa upimaji wa mimba kwa wanafunzi wa kike.
Inadaiwa kuwa kutokana na mwanafunzi huyo kuwa mwanafamilia ya mmiliki wa shule hiyo, ilipobainika kuwa mjauzito suala hilo lilifanywa siri.
“Familia ilifanya hivyo kulinda heshima ya shule na jina la shule lisichafuke,” kinasema chanzo chetu.
Kumekuwa na madai kutoka kwa vyanzo vya habari vya gazeti hili kwamba, mbinu za kuficha suala hilo ziliratibiwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa shule hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Shule, Anna Sangoma Bayi, ambaye ni bibi wa mwanafunzi huyo.
“Shule ilipobaini kuwa (jina linahifadhiwa) ana ujauzito wa miezi saba, bibi yake, kwa kushirikiana na mkuu wa shule walimruhusu afanye mtihani, wakakubaliana suala hilo kulifanya siri hadi kwa wazazi wa (jina linahifadhiwa) wasijue mpaka hapo mtihani wa taifa utakapokwisha,” anasema mfanyakazi huyo.
Hata hivyo, baada ya kumaliza mtihani na kuhitimu elimu ya sekondari, Januari mwaka huu, mwanafunzi huyo alijifungua mtoto wa kiume na kumpa jina (linahifadhiwa). Huduma ya kujifungua alipatiwa katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es Salaam.
Ester Minja, ni mama mzazi wa mwanafunzi huyo, amefuatwa na Gazeti la JAMHURI ofisini kwake na kueleza kuwa anafahamu kila kitu kuhusu mwanaye kubebeshwa mimba, lakini hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa undani.
Anasema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu mtoto huyo haishi naye na kwamba, kimepita kipindi kirefu bila kuwa karibu na mwanaye huyo na kuongeza kuwa anayeweza kuzungumzia hilo zaidi ni bibi yake ambaye ndiye mlezi wake kwa sasa.
“Siwezi kuongea chochote kuhusu (jina linahifadhiwa) kwa sababu hapa niko kazini na suala hili mnalotaka kujua ni la kifamilia, kwani mpaka mnanifuata ofisini kwangu hampajui nyumbani kwangu? Kwa nini hamjanipigia simu, kwanza, nani kawaeleza?
“Kama mnataka kujua suala hili mngenifuata nyumbani na si hapa kazini, nakwambieni siwezi kuongea chochote, hata mkinifuata nyumbani msitegemee kuambiwa lolote, siwezi kulizungumzia suala hilo, mtafuteni bibi yake,” amesema Minja.
Baada ya mazungumzo hayo, Minja akiwa katika hali ya hasira akaanza kuondoka huku akiomba kufahamu jina la mtu ambaye ametoa taarifa hizo kwa Gazeti la JAMHURI.
JAMHURI lilimtafuta mwalimu mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Yasintha, ambaye alieleza kuwa hafahamu lolote kuhusu tukio hilo kwa sababu hakuwepo shuleni hapo kwa mwaka jana.
“Mimi nimeletwa shuleni hapa mwaka huu, mwalimu mkuu aliyekuwepo kwa mwaka jana unaweza kumuuliza akakupa ufafanuzi,” amesema Yasintha.
Ameongeza kuwa mwalimu mkuu aliyekuwepo mwaka jana kwa sasa yupo masomoni na kwamba mkuu huyo pamoja na mkurugenzi wa shule hiyo ndio wenye kuweza kuzungumzia suala hilo kwa undani.
JAMHURI limezungumza na mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Sangoma Bayi na kukana kutokuwa na taarifa za mwanafunzi mjamzito kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kwa mwaka jana katika shule yake.
“Hilo haliwezekani, yaani mwanafunzi awe na ujauzito wa miezi saba halafu ashindwe kubainika? Kwenye chumba cha mtihani chenye wasimamizi kama wanane wakiwamo watu wa Ofisi ya Rais, hicho kitu hakiwezi kutokea, sijui atavaa nguo gani ambazo zinatamficha mimba hiyo isionekane?” alihoji Sangoma.
Hata hivyo, anakiri kwamba suala hilo linaweza kutokea na asifahamu kwa sababu amekuwa na majukumu mengi ya kikazi shuleni hapo.
“Hapa tunapambana na mengi, watoto tunawafundisha malezi kila siku lakini hawasikii, hilo linaweza kutokea ikawa bahati ya mwanafunzi huyo kufanikiwa kufanya mtihani bila kubainika kwa sababu baadhi ya wanawake wana maumbile ambayo huwaficha na kushindwa kujulikana hadi siku ya kujifungua,” amesema Sangoma.
Alipoelezwa kuhusika katika kuficha taarifa za ujauzito wa mwanafunzi kwa kushirikiana na mkuu wa shule hiyo, alisema suala hilo halifahamu.
Hata hivyo baada ya kuelezwa kwamba mwanafunzi anayetajwa ni mjukuu wake, alisema hilo halimaanishi kwamba anaweza kumsaidia kumvusha kwenye tuhuma kama hizo na jambo hilo lisihusishwe na shule yake.
“Shule haihusiki kumpa mimba mwanafunzi, kama wazazi wake walishindwa kumpa malezi ya kutosha wasitake kuchafua jina la shule yetu kwa hoja kama hiyo.
“Hata hivyo, mtihani umekwishafanyika nyinyi gazeti, sijui la JAMHURI mnafuatilia suala hili ili mfaidike na nini?
“Kama mtoa taarifa kwenu alikuwa na mapenzi mema na shule yetu, kwa nini hakuja hapa shuleni kutueleza kabla ya kulifikisha kwenu?
“Kwa hiyo nyinyi mmefuatilia jambo hili ili iweje? Haya, mwanafunzi huyo ameshajifungua, Mungu kampitisha bila sisi kumgundua, nyinyi mnataka sisi kama shule tufanye nini kwa mwanafunzi ambaye ameshamaliza shule?” anahoji Sangoma.
Alipoelezwa kwamba yeye ndiye mlezi wa mwanafunzi huyo na mpaka sasa anaishi naye nyumbani kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo (Ester Minja), alisema taarifa hizo zinaonekana kulenga kuchafua jina la familia ya Bayi kwani mtoto huyo hakai kwake.
“Mume wangu hana mpango na kugombea aina yoyote ya uongozi, hana mpango wa kuwa diwani, mbunge wala kugombea nafasi yoyote katika siasa, sasa sijajua mnaleta taarifa kama hizo ili nini kitokee?” alihoji Sangoma.
Majibu ya wizara
Akizungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk. Ave-Maria Semakafu, alimweleza mwandishi wetu kuwa wizara haisimamii uendeshaji wa shule hiyo moja kwa moja.
“Wizara haifanyi usimamizi wa moja kwa moja wa shule hiyo pamoja na shule nyingine, masuala ya uendeshaji wa shule yamo mikononi mwa uongozi wa shule. Kuna mambo yanayosimamiwa na wizara katika shule hizi, mambo ya jumla ya kitaifa na si uendeshaji wa kila siku,” alisema kiongozi huyo wa wizara, akielezea nafasi ya wizara katika masuala ya elimu.
Sera ya elimu
Sera ya elimu, pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa msingi wa elimu na mafunzo utajikita katika kumjengea Mtanzania misingi bora ya malezi, maadili, ujuzi, umahiri na kumwezesha kujitegemea.
“Elimu ya kujitegemea itaendelea kuongoza utoaji wa elimu na mafunzo kwa kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika jamii, kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia,” inaeleza sera hiyo.
Kuhusu dira, sera inaeleza malengo ya kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya taifa, wakati dhima ikilenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo pamoja na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.