DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema wanatarajia kufanya mjadala wa matumizi ya magari ya umeme yanayopita kwenye nyaya (cable cars) kwa ajili ya kuwapandisha watalii katika Mlima Kilimanjaro.
Kauli ya Ndumbaro imekuja huku kukiwa na mgongano wa hoja kutoka kwa baadhi ya wadau wa sekta ya utalii wakipinga ‘cable cars’ kupandisha watalii kutokana na sababu kadhaa ikiwamo athari za kimazingira, ikiwamo kumaliza uoto wa asili wakati wa ujenzi wake, usalama wa watalii kuwa mdogo kutokana na urefu wa Mlima Kilimanjaro na yatasababisha ukosefu wa ajira kwa waongoza watalii.
Miongoni mwa wanaopinga ni kampuni za kigeni kutoka nje ya nchi ikiwamo Cumbre Tours, Boss Adventure Treks and Expedition, Bergfalke na mdau mwingine wa utalii, Meinrad Bittel.
Pamoja na mambo mengine, wanatoa uzoefu wa athari zilivyotokea katika nchi nyingine ikiwamo Uswisi, kuna ‘cable cars’ zinazopanda mlima wenye urefu wa mita 3,900 lakini watalii hawazitumii na wakizitumia wanaumwa na wanashindwa kupumua, sasa wanahoji itakuwaje kwa Mlima Kilimanjaro wenye urefu wa mita 5,895.
Pia wanasema ‘cable cars’ zitasababisha kampuni hizo kufunga biashara zao kwa sababu watakosa watalii na baadhi ya Watanzania wanaojihusisha kutoa huduma za utalii nao watakosa ajira.
Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Ndumbaro amesema mjadala huo utafanyika Machi 8, mwaka huu mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na utahusisha wadau wote.
“Mwaka 2017 Tanapa walikuja na wazo la kuanzisha ‘cable cars’ katika Mlima Kilimanjaro. Lilikuwa wazo zuri kwamba liwasaidie watu wenye ulemavu na wazee waweze kupanda mlima.
“Lakini watu wengine wanakwambia raha ya mlima ni kuupanda, sasa hiyo ndiyo demokrasia na tumeitisha huo mjadala kwa hiyo wadau wote waje wakiwamo na wananchi, tujadiliane, tukikubaliana ‘cable cars’ zianze, basi zitaanza na tusipokubaliana basi hazitaanza,” amesema.
Katika hatua nyingine, Ndumbaro, amesema licha ya athari za janga la ugonjwa wa Covid-19 lakini kuna matumaini mapya katika sekta ya utalii baada ya idadi ya watalii kuongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka juzi hadi watalii 922,692 mwaka jana.
Pia amesema mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa nayo yanakadiriwa kuongezeka kutoka dola milioni 714.59 za Marekani kwa mwaka juzi hadi dola milioni 1254.4 kwa mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 76.
Vilevile amesema kuimarika kwa utalii hapa nchini kumetokana na mwelekeo na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kutekeleza mpango wa chanjo kitaifa ya Covid-19 unaoleta taswira mpya kiutalii kwamba Tanzania ni eneo salama zaidi kutembelewa na watalii.
“Utalii umekuwa ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa wafanyakazi kupatiwa chanjo na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanzisha vituo viwili vya kuchukulia sampuli kwa ajili kupima Covid-19 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuweka maabara maalumu ya kupima ugonjwa huo katia eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,” amesema.
Ndumbaro amesema Programu ya Royal Tour iliyomshirikisha Rais Samia imeanza kuleta matunda kwa kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali kuja hapa nchini.
“Wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika nchi masoko ya utalii yakiwamo Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.
“Wawekezaji kutoka Bulgaria nao wanakusudia kuwekeza katika huduma za malazi za hadhi ya kimataifa kwa kujenga loji nne zenye hadhi ya nyota tano, zitakazoendeshwa na Kampuni ya Kempiski katika hifadhi za Serengeti, Manyara, Tarangire na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, hatua itakayoleta matokeo chanya katika kuongeza idadi ya vyumba na wigo wa mnyororo wa huduma katika sekta ya utalii,” amesema.
Aidha, amesema pamoja na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa, pia idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi nayo iliongezeka kutoka watalii 562, 549 mwaka juzi hadi watalii 788,993 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 40.2 huku mapato nayo yakiongezeka kutoka Sh bilioni 9.7 mwaka juzi hadi Sh bilioni 12.4 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 27.8.
Pia amesema katika kuimarisha utoaji wa huduma za sekta ya utalii wamekuwa wakifanya maboresho mbalimbali yaliyosaidia nchi kupata tuzo 10 za kimataifa pamoja na kupewa heshima mpya kushiriki na kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali na miradi ya maendeleo.
Amezitaja baadhi ya tuzo kuwa ni iliyotolewa na World Travel Award kwa Hifadhi ya Taifa ya Serngeti kwa kuongoza barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo (mwaka 2019, 2020 na 2021).