WAZIRI Mkuu Mstaafu,Mizengo Pinda ametoa wito kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kutangaza fursa za Biashara ya Kaboni ili kuwawezesha wananchi kupata mwako wa kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti hivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa rai hiyo leo Jumatatu (Agosti 7, 2023), wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya
Mhe. Pinda amesema biashara ya kaboni inahusisha zaidi upandaji na utunzaji wa miti na kuweka mifumo inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kilimo, nishati, viwanda, na miundombinu hivyo ni wajibu wa elimu ya biashara hiyo iendelee kutolewa katika Mikoa yote nchini.
“Biashara hii imeingia katika Mkoa wa Katavi na tayari wananchi wamenufaika na mradi huu kwa kuongeza mapato na kuimarisha utoaji wa huduma kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa sambamba na kuzuia uharibifu wa misitu iliyohifadhiwa” amesema Mhe. Pinda
Kwa mujibu wa Mhe. Pinda amesema iwapo elimu ya kutosha itatolewa kwa wananchi kuhusu fursa ya biashara ya kaboni ni matumaini kuwa kuwa jitihada hizo zitawawezesha wananchi kupata uelewa na kunufaika na biashara hiyo wakiwemo wakulima na wafugaji.
Akifafanua zaidi Mhe. Pinda amesema kazi kubwa iliyopo kwa sasa ni kuhamasisha wananchi kuhifadhi misitu ya asili na kutunza mazingira kwa kuhakikisha hakuna ukataji miti hovyo, uchomaji misitu na kuzuia kufanyika kwa shughuli zingine hatarishi.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Mwandamizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Lungo amesema kwa kutambua umuhimu wa Biashara ya Kaboni, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kufanyia maboresho Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 ili ziweze kuwatambua na kuwanufaisha wakulima na wafugaji nchini.
Aidha Lungo amesema kuandaliwa kwa kanuni na mwongozo wa biashara hiyo, kutawezesha kuuzwa kwa wingi hewa ya ukaa na ukamilifu wake na kuwezesha misitu iliyopo katika vijiji husika kulipwa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo Serikali inaendelea kuwahimiza wananchi kuhifadhi misitu na kutunza mazingira.
“Matumizi bora ya ardhi ndio chanzo cha biashara hii kwa maana ya kutenga maeneo ya hifadhi ya misitu na kuilinda. Tumeendelea kuhimiza jamii kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa ajili matumizi mbalimbali sambamba na kufyonza hewa ukaa kwa manufaa endelevu” amesema Lungo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Pinda aliongozana na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Rukwa akiwemo Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Makongoro Nyerere na Katibu Tawala Bw. Gerald Kusaya.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara na Taasisi za Umma na binafsi kushiriki Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) mwaka 2023 yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifuko ya Chakula”