Profesa-Makame-MbarawaDalali wa Mahakama, Japhet Kandonga, ameuza nyumba ya Serikali namba 162, kiwanja namba 1103 iliyoko Kitalu ‘S’ eneo la Mafiati Jijini Mbeya kwa Sh milioni 250 kwa mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Saul Henry Amon, na kudai kwamba mnunuzi huyo alishindwa kulipa kiasi hicho cha fedha.

Awali akihojiwa na JAMHURI, dalali Kandonga ameeleza kwamba aliuza nyumba hiyo kwa mnada kwa mfanyabiashara huyo kwa amri ya Mahakama, lakini aliposhindwa kulipa ikaamuriwa iuzwe kwa mshindi wa pili wa mnada ambao unaelezwa haukufanyika.

Kandonga alieleza kwamba uuzwaji wa nyumba hiyo ulizingatia taratibu za mnada, matangazo yalikuwa ya wazi na havikuwako vificho kama inavyodaiwa kwamba aliwatafuta wanunuzi wanne tu na kufanya makubaliano nao ndani ya gari.

“Kesi ilikuwa mahakamani na Mahakama ndiyo iliyotoa amri kwamba nyumba hiyo iuzwe, hivyo nikaenda kuikamata na kuiuza na fedha zilipelekwa mahakamani na kugawanywa kwa wahusika kwa maelekezo yaliyotolewa,” anasema.

Amesema, Amon alikuwa mnunuzi wa kwanza lakini alishindwa kulipa fedha hizo, hivyo kwa maelekezo ya Mahakama aliuziwa mtu aliyeshika nafasi ya pili katika mnada huo.

Alipoulizwa jina la mnunuzi wa pili wa nyumba hiyo, alishindwa kumtaja na kukata simu, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno uliomtaka ataje jina la mnunuzi huyo hakutoa jibu lolote.

Madai ya dalali huyo kwamba mnunuzi wa kwanza alishindwa kulipa fedha hizo, yanaibua mashaka makubwa ya uuzaji wa nyumba hiyo kwani hakuna kielelezo kinachomtaja kwa jina mnunuzi wa pili wa nyumba hiyo, huku ikielezwa kuwa hakukuwa na mnada wowote uliotangazwa.

Kutokana na utata huo uliogubika uuzaji wa nyumba hiyo aliyouziwa mtumishi huyo wa umma, Simbonea Kileo, na Serikali ikiwa na hati Namba 11443-MBYLR ilitolewa Oktoba 2007 baada ya kumaliza kulipa deni la nyumba hiyo. Hata hivyo, wanunuzi wote wanaendelea na biashara hiyo bila kuwa na hatimiliki.

Kileo alikopeshwa na Serikali nyumba hiyo kupitia Wakala wa Majengo (TBA) kwa mkataba namba 1531, lakini iliuzwa kiujanja na mazingira ya rushwa kwa mfanyabiashara huyo Julai 5, 2012 kwa amri ya Mahakama ya Mbeya Mjini, baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka 2007 kutokana na kutelekezwa na mkewe, Gladness Kimaro, na watoto wake watatu tangu Januari 2001.

Kileo anasema kabla ya nyumba hiyo kupigwa mnada, alimjulisha Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, ambaye alimshauri apeleke nyaraka zote zinazohusiana na kesi hiyo Makao Makuu ya Wakala wa Majengo Jijini Dar es Salaam na kwamba baada ya kukabidhi nyaraka hizo Juni 2012 lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi nyumba hiyo inaporwa.

Anasema baada ya kuona hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, aliomba ushauri kwa Mwanasheria wa Serikali ambaye alimshauri kupitia mwanasheria wa TBA kwamba afungue kesi dhidi ya mnunuzi wa nyumba ya Serikali kupinga uuzwaji wa nyumba hiyo.

Hata hivyo, kwa kuwa muda wa kukata rufaa ulikuwa umeshapita, alishauriwa na Mwanasheria wa Serikali kupitia Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, kwamba aombe marejeo (revision) ya hukumu kujibu upungufu wa Mahakama kutotambua mkataba.

“Kwa upande wangu nilikuwa tayari nimefungua kesi ya kupinga mnada huo pamoja na kuomba marejeo. Kesi ya kupinga mnada huo ilimalizika kwa kufutwa kwa mnada huo na kuamriwa mnunuzi arudishiwe fedha zake.

“TBA hawajatekeleza ushauri waliopewa na Mwanasheria wa Serikali hadi sasa, na sielewi kuna tatizo gani ingawa nilionana na Mtendaji Mkuu na kumfahamisha kila kilichojiri mahakamani – yeye na Meneja wa Wakala huo Mkoa wa Mbeya pamoja na kumpa nakala za hukumu.

“Nachelea kusema uongozi wa TBA unahusika katika uuzwaji wa nyumba hii kinyemela, kwani wamekaa kimya kama hakuna kilichotokea,” anaeleza Kileo katika barua aliyomwandikia Waziri Mkuu, yenye kumbukumbu namba SGK/MBY/2016/01 ya Februari 27, 2016.

Kileo anasema akiwa safarini alishangazwa na shauri hilo kuendeshwa kwa kasi ya ajabu ndani ya siku nane tu, huku Wakili wake (Shitambala) akishindwa kuhudhuria mahakamani hata mara moja licha ya kumlipa gharama zote za kesi hiyo na hivyo kutolewa hukumu ya upande mmoja.

Pamoja na hilo, anaeleza kwamba mawakili wake wanne akiwamo Shitambala, Mkumbe, Lwambano na Mary Mgaya kwa nyakati tofauti walijiondoa kwenye kesi hiyo bila taarifa huku akiwa amewalipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.

Kwa haraka aliyokuwa nayo Hakimu Seif Kulita aliamuru nyumba iuzwe huku akijua hakuna nakala (Notice of Execution) iliyokuwa imetolewa na hivyo Mahakama ya Wilaya iliamuru watoto wagawiwe asilimia 45 ya mauzo na ndani ya jalada hilo kukiwa na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo, ambayo haijawahi kupingwa popote iliyoeleza kwamba watoto wote watatu wataendelea kuishi na baba yao.

Anasema alikata rufaa mara mbili kupinga hukumu ya upande mmoja na pia marejeo Mahakama Kuu kwa hati ya dharura kabla ya mnada Julai 5, 2012. Maombi hayo hayakufanyiwa kazi hadi Aprili 2015 yalipotupiliwa mbali na Jaji Mfawidhi Chocha na kuamuru alipe gharama.

Licha ya kupewa amri ya zuio na Baraza la Ardhi na barua kutoka TBA Mkoa wa Mbeya zikimtaka Kandonga asiuze nyumba hiyo, yeye aliendelea na mnada uliozua mashaka kwani haukutangazwa.

“Nilipata ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu muda mfupi kabla ya mnada kwamba yangu itabadilika jina na kuwa Landmark na baada ya ujumbe huo nilielezwa imeuzwa kwa Amon kwa Sh milioni 250,” inaeleza sehemu ya barua aliyomwandikia Waziri Mkuu.

Dalali Kandonga alizuiwa na Meneja wa TBA Mkoani Mbeya kuuza nyumba ya Serikali kwa kuwa ni kinyume na taratibu na masharti ya nyumba zilizouzwa na Serikali kwa watumishi wake kwa barua ya Julai 4, 2012 lakini alikaidi maelekezo hayo.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, Jaffary Kiyonga, inaeleza kwamba mkataba wa mauziano kifungu Na. 9 na 10 vinaeleza kwamba mtumishi yeyote aliyeuziwa nyumba za Serikali au mrithi wake, hawaruhusiwi kuuza nyumba hadi hapo itakapotimia miaka 25 kuanzia tarehe aliyopewa hatimiliki.

Pia barua nyingine ya TBA kwenda kwa Kileo, iliyoeleza kuhusu ukiukwaji wa taratibu na masharti juu ya kuuzwa kwa nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wake, inaeleza kwamba Wakala umepokea ushauri kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali wakati hatua za kisheria kwa waliokiuka amri ya Mahakama zikifanyika kwamba ifungue kesi dhidi ya mnunuzi wa nyumba hiyo kupinga uuzwaji wake.

JAMHURI ilimtafuta mfanyabiashara Amon ili kuelewa kama alishindwa kulipa kiasi cha fedha za ununuzi wa nyumba Sh milioni 250 na hivyo Mahakama kuagiza auziwe mnunuzi mwingine kama alivyodai Kandonga, lakini alikanusha madai hayo.

“Mimi nililipa fedha hizo nikiwa mnunuzi wa kwanza, kesi bado iko mahakamani, nadhani unaelewa kuhusu suala hilo,” anasema Amon, ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Magharibi.

Anasema baada ya kununua nyumba hiyo, ameiuza kwa mtu mwingine na siyo kama inavyodaiwa na dalali Kandonga. Hata hivyo, amechukua uamuzi huo pamoja na kuelewa kwamba kuna mgogoro mkubwa uliotokana na kuuzwa kwa nyumba hiyo huku akikiri kesi iko mahakamani.

Naye Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, Kiyonga, alipohojiwa kuhusu suala hilo na hatua zinazochukuliwa na ofisi yake ili kuhakikisha nyumba hiyo inarudishwa kwa mmiliki wake halali aliyeuziwa na Serikali, hakutaka kueleza chochote kwa madai kwamba mlolongo ni mrefu.

“Mzozo wa nyumba hiyo upo, lakini kama ninavyokueleza siwezi kukueleza kwa njia simu labda uwasiliane na TBA Makao Makuu, wao ndio wasemaji,” anasema.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga, amesema nyumba hiyo iliuzwa kwa njia za ujanja, kwani kifungu kinachoeleza kwamba mtumishi aliyeuziwa nyumba na Serikali, hapaswi kuiuza ama kubadili matumizi yake hadi kipindi cha miaka 25 kitakapomalizika tangu alipokabidhiwa hatimiliki.

“Kifungu hicho labda kiliondolewa na ili wahusika waiuze nyumba hiyo kwa urahisi na kubadilisha matumizi yake na hivyo suala hili silielewi vizuri, kwani wakati inauzwa mwaka 2012 sikuwa mtumishi wa Wakala wa Majengo,” anasema.

Hata hivyo, pamoja na madai ya Mwakalinga kuhusu kuondolewa kwa kifungu hicho, Kileo aliyeuziwa nyumba na Serikali anasema mkataba wa kuuziwa nyumba na TBA ulikuwa na kifungu hicho lakini kwenye hati kilisahaulika na baada ya kuonekana upungufu huo, Msajili wa Hati Kanda ya Nyanda za Juu, alifanya marekebisho na kukiingiza kipengele hicho.

Kileo anasema wakati shauri linaendelea mahakamani na taratibu za uuzwaji wa nyumba yake zikiendelea, wahusika wote walikiona kifungu hicho na kuamua kukaidi.    

Iwapo utaratibu wa kuuza nyumba hiyo na kubadilisha matumizi ya ardhi ungefuatwa kulingana na mkataba aliopewa Kileo na watumishi wengine wa umma waliouziwa makazi kwa kuzingatia kifungu hicho namba 9 na 10 kinachoeleza masharti kwa mnunuzi wa nyumba ya Serikali cha kuuza au kubadili matumizi yake baada ya kipindi cha miaka 25 tangu alipokabidhiwa hati, ilipaswa kuuzwa Oktoba 2032.