Kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na vyote vilivyomo tukiwamo sisi wanadamu, kwa mema mengi mno anayonitendea na hasa kwa kutujalia uhai hadi leo hii.
Kwa vyovyote vile bila ya Mwenyezi Mungu kutuwezesha na kututia nguvu sisi wenyewe hatuwezi, bali hali ilivyo ya kimazingira na kimaumbile tutakwama tu, hata hao wanaokwenda angani na kufanya wanayoyafanya huko si kwa uwezo wao tu, bali pia ni kwa mapenzi yake Mola.
Hata kama watajidai kuwa ni kwa uwezo wao, hiyo ni hali ya kimwili, bali kiroho atabaki kuwa ni Mwenyezi Mungu. Hivyo, hatuna budi kumshukuru kila wakati na bila kukoma maana tunayaweza hayo yote kwa yeye atutiaye nguvu.
Siku chache zilizopita nilitoa makala yaliyoeleza kwa kirefu uharibifu unaofanyika katika misitu yetu ya asili Tanzania Bara. Makala hayo yalichapishwa kwa mara ya kwanza katika moja ya magazeti yatolewayo kwa wiki hapa nchini na pia kuchapishwa katika gazeti hili.
Ni matumaini yangu kuwa wananchi wengi wameweza kuisoma na kuyaelewa vizuri makala hayo, kwa lengo la kuchukua hatua sahihi za kulinda na kuiendeleza misitu ya asili nchini kwa faida ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Misitu ya asili ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Mwenyezi Mungu tangu alipouumba ulimwengu, ikiwamo sayari hii tunayoishi sisi wanadamu. Kwa maneno mengine, misitu au maliasili zote tulizonazo ikiwa ni pamoja na madini, wanyamapori, samaki na viumbe wengine waishio baharini, ardhi (kwa maana ya udongo), maji (kwa maana ya vijito, mito, maziwa, mabwawa, bahari na ardhioevu), nishati mafuta na gesi asilia ni zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.
Hivyo, yatupasa kutumia misitu ya asili pamoja na maliasili nyinginezo kwa uangalifu mkubwa, kwa ajili ya kuboresha maisha yetu na ya vizaji vijavyo.
Katika makala au mada hii nitazungumzia suala la umuhimu wa rasilimali misitu, hasa misitu inayopatikana katika ardhi ya vijiji na mchango wake kwa maendeleo ya jamii na hasa kwa Watanzania wanaoishi vijijini.
Kwa bahati nzuri Tanzania Bara imebahatika kuwa na eneo kubwa lenye misitu ya asili pamoja na mapori mazuri yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori. Kwa takwimu za mwaka 1998 (ambazo sasa zimeboreshwa na matokeo ya mradi wa kitaifa wa kupima na kutathmini misitu ya asili), Tanzania ilikuwa na eneo la misitu ya asili la takribani hekta milioni 33.5.
Kati ya hizo, hekta milioni 13 ni eneo la misitu lililohifadhiwa kisheria (misitu ya hifadhi ya Serikali Kuu (Central Government Forest Reserves) takribani misitu 600 na misitu 200 ikimilikiwa na Serikali za Mitaa (Local Authority Forest Reserves) chini ya halmashauri za wilaya); na zaidi ya hekta milioni 20 ya misitu ya asili bado haijahifadhiwa na kusimamiwa kisheria.
Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, vijiji vichache vimeweza kutenga sehemu ya misitu katika vijiji vyao na kuitangaza kuwa misitu ya hifadhi ya vijiji yenye jumla ya hekta zaidi ya milioni saba. Hatua hiyo ni ya kupongezwa maana vijiji husika sasa vina nguvu ya kisheria kusimamia na kutumia misitu husika ipasavyo na hatimaye kunufaika na usimamizi huo, kwa kuongozwa na Sheria ya Misitu na kanuni zake.
Vilevile, vijiji vinayo fursa ya kujiwekea sheria ndogo ndogo kwa lengo la kuimarisha zaidi utekelezaji wa shughuli za kulinda msitu kwa faida yao na Taifa kwa jumla. Pamoja na mafanikio hayo, bado sehemu kubwa ya misitu ya asili ambayo haijahifadhiwa kisheria inapatikana katika maeneo ya vijiji na haitumiki ipasavyo kuviletea vijiji maendeleo endelevu.
Miaka zaidi ya 20 Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Kutunza na Kuendeleza Misitu nchini (Participatory Forest Management-PFM). Dhana ya Ushirikishwaji ni mbinu ya uongozi inayowezesha kupata mchango wa mawazo na ushiriki mzuri kutoka kwa wadau mbalimbali, hasa katika utekelezaji wa shughuli za kujiletea maendeleo endelevu kwa kutumia rasilimali za asili tulizonazo.
Ushirikishwaji husaidia watu kubadilishana mawazo na kufahamu vizuri nini kinaendelea au kinatekelezwa kwa faida yao. Hivyo kwa kuwashirikisha wanavijiji katika masuala yanayohusu maendeleo yao vijijini ni suala muhimu sana na huondoa lawama, pia huongeza motisha wakati wa kutekeleza jambo lililoamuliwa.
Isitoshe, ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha kuwa anawajibika ipasavyo katika kutoa mawazo na kufikia uamuzi sahihi ili lengo na madhumuni ya mipango ya maendeleo katika sehemu yao iweze kufanikiwa. Ili wanakijiji au jamii katika ujumla wake waweze kufanya hivyo, ni lazima waelimishwe vya kutosha na kuwajengea uwezo (capacity) wa kusimamia na kutumia kwa misingi endelevu rasilimali na fursa zilizopo ikiwamo misitu ya asili.
Wanavjiji ni muhimu washirikishwe na viongozi wao katika kujadili na kubuni mbinu za ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili na zitakazojitokeza wakati wa kutekeleza shughuli zao za kimaendeleo. Hii ni pamoja na kuwapatia mafunzo ya fani na stadi mbalimbali kama vile uongozi bora, utunzaji wa mazingira, mipango na uendeshaji, ufumbuzi au utatuzi wa changamoto na utungaji wa sheria ndogo za vijiji.
Sera na Sheria za Misitu Tanzania Bara
Usimamizi shirikishi katika masuala ya kutunza na kuendeleza misitu nchini umekuwa ukifanyika kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 (inafanyiwa marekebisho) na kwa kuzingatia Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 (Sura 323 ya Sheria za Tanzania ). Vitendea kazi hivyo katika Wizara ya Maliasili na Utalii vinabainisha wazi haja ya kusimamia vizuri maeneo yote ya misitu yaliyohifadhiwa na yasiyohifadhiwa. Vilevile, kuweka fursa ya usimamizi madhubuti chini ya jamii husika, serikali za vijiji na watu binafsi: kama misitu ya hifadhi na kujulikana kama Usimamizi Shirikishi katika kutunza na matumizi endelevu ya rasilimali misitu.
Madhumuni makubwa ya Sera na Sheria ya misitu katika suala zima la Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) ni kuhakikisha kuwa kunakuwapo upatikanaji endelevu wa mazao na huduma za misitu wakati wote.
Ili kufikia lengo hilo, ni lazima kuwapo kwa maeneo ya kutosha ya misitu yenye usimamizi imara ndani ya jamii yenyewe. Kwa kuwa kuna vijiji vingi hasa katika mikoa ya Geita, Kagera (hasa wilayani Biharamuro), Katavi, Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya (hasa katika Wilaya ya Chunya), Mtwara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Tabora, na Tanga (hususan wilayani Handeni) vyenye maeneo mazuri ya misitu ya asili; ni vizuri vijiji vikatenga baadhi ya meneo ya misitu ya hiyo na kuyaweka chini ya usimamizi wa kisheria kwa maana ya kuitangaza kama misitu ya hifadhi ya vijiji au jamii (Village or Community Forest Reserves).
Kwa kufanya hivyo vijiji vitajihakikishia uwezo wa kumiliki na kuisimamia misitu hiyo kwa manufaa ya jamii au kijiji husika chini ya sheria na taratibu zilizopo, lakini pia vijiji vinaweza kujiwekea sheria ndogo ndogo kuhakikisha matumizi yake hayataadhiri uwezo wa misitu kuendelea kuwapo.
Aidha, Misitu ya Hifadhi ya Vijiji itasimamiwa na Serikali za vijiji au na vyombo vingine vilivyochaguliwa na Serikali za vijiji kwa ajili hiyo. Mathalan, kuwapo kwa Kamati Simamizi ya Msitu au Maaliasili. Misitu hii itasimamiwa kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji endelevu wa mazao ya misitu na/ama kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji au ardhi/udongo kulingana na hali ya kiikolojia ya mahali misitu ilipo pia madhumuni mengineyo kama kuendeleza shughuli za kimila/utamaduni au dini za asili (cultural & ritual values).
Itaendelea
Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012. Anapatikana kwa simu na. HYPERLINK “tel:0756%20007%20400”0756 007 400.