Katika sehemu ya nne, Dk. Felician Kilahama alizungumzia kazi ya kutoa huduma bora za kijamii na kujenga miundombinu imara katika nchi yenye eneo kubwa. Alisema shughuli hiyo inahitaji ujasiri mkubwa na uzalendo wa hali ya juu. Sehemu hii ya tano na ya mwisho, Dk. Kilahama anatoa hitimisho.

Rasilimali tulizonazo: ardhi yenye rutuba, madini mbalimbali, misitu, wanyamapori, samaki, maji (katika mito, maziwa, mabwawa, bahari na maji mengine chini ya ardhi) vyote hivi vikitumika kwa uangalifu mkubwa na kwa nia ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu, hakika tutasonga mbele bila ya kutegemea wahisani na wawekezaji kutoka nje ya taifa letu.

 

Ninalolizungumza hapa siyo nadharia, wala siasa maana kuna unadharia mwingi ndani ya siasa zetu kuliko uhalisia na ukweli wa mambo. Kwa nini nasema hivyo? Nchi yetu imesheheni wataalamu wengi wa fani zote na wengine wamebobea au kwa usemi mwingine ni magwiji katika fani zao, kiasi cha nchi nyingine kuweza kuwatumia kwa faida ya watu wao.

 

Tunazo rasilimali za asili za kutosha. Vitu hivyo viwili (wataalamu na rasilimali tulizonazo) ni mtaji wa kutukwamua kutoka katika hali ya umasikini tuliyo nayo.

Kinachotakiwa ni kuweka mipango mizuri, pia kuwa na utaratibu mzuri wa kuitekeleza kwa kuwatumia wataalamu waliopo. Siyo suala kusema hatuna fedha za kutosha. Fedha zipo, ni jinsi gani tunazikusanya au kuzitafuta na kuzitumia kwa faida ya Watanzania. Tunaowaita wawekezaji baadhi yao wanakuja hawana fedha za kutosha ila wana utaalamu na wanatumia rasilimali tulizonazo hapa nchini mwetu kutafuta hizo fedha na wakishazipata kwa kiasi kikubwa wanazitumia kujinufaisha wenyewe kuliko kutunufaisha sisi.

 

Mifano halisi ya waliofanya hivyo ipo. Hapa ni suala la kuwa na mipango mizuri na jinsi gani tunavyozitumia akili zetu, na pia kwa kuweka uzalendo mbele kwa faida ya Watanzania wote. Tutafanikiwa kama wanavyofanikiwa hao wawekezaji. Kwa nini tusiwekeze sisi wenyewe au kulikoni katika nyanja ya uwekezaji au nini kikwazo?

Dhana ya uwekezaji siyo mbaya ila inatokana na mwekezaji lengo lake kuu ni nini! Kwa wawekezaji wengi nia yao ni kutumia fursa tulizo nazo kupata faida kubwa wakati sisi tunahitaji kupata wawekezaji ili tutumie fursa zetu na kufaidika na hatimaye kuondokana na umasikini.

 

Hapa ndipo changamoto ilipo na ni jinsi gani tunapambana nayo ili pande zote mbili (wenye rasilimali na wawekezaji au sekta binafsi). Kwa mfano, sasa Tanzania inayo gesi asilia ya kutosha na sasa kupitia gesi hiyo tunasema sasa umaskini nchini ndiyo mwisho.

 

Hili linawezekana ni kujipanga vizuri ili tuitumie rasilimali hiyo muhimu Watanzania tuondokane na umasikini. Kwa dhamira sahihi na usimamizi imara hakuna lisilowezekana. Gesi asilia ni rasilimali muhimu sana na sasa inapatikana nchini mwetu, wataalamu pia wapo. Kinachotakiwa ni namna gani vitu hivi viwili vitatumika kwa kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania.

 

Kilichotokea katika Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ ni mfano halisi wa hicho nilichokielezea hapo juu. Yote yawezekana kwake aaminiye na tukisema tunaweza dhamira iwe ni hiyo na tuamini kuwa hakuna litakalotushinda. Hivyo ndivyo walivyojitosa wanakijiji kwa kuona kuwa rasilimali-watu ipo ya kutosha, misitu ya asili wanayo na wataalamu wapo hivyo wakaona ni vizuri wakatumia uwezo walionao kujiletea maendeleo endelevu.

 

Kulingana na mpango wa uvunaji katika msitu wao kwa kipindi cha 2013/2014 kijiji kinatarajia kuvuna meta za ujazo (m3) 1238 za mipingo ambazo kwa bei ya Sh 180,000 kwa kila ujazo kijiji kinatarajia kupata Sh 222,840,000. Kiasi hicho siyo kidogo kulingana ra rasilimali itakayovunwa na kuuzwa na kitasaidia kusukuma mbele maendeleo ya kijiji. Licha ya kuvuna mipingo kijiji kinatarajia kuvuna aina nyingine za miti iliyo tayari kuvunwa na hivyo matarajio ya kupata fedha zaidi ni makubwa sana.

 

Katika mkutano tuliofanya na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, tuliwauliza nini matarajio yao ya baadaye? Jibu lilikuwa kwamba; kwanza, wanataka kuongeza bidii kwenye kuhifadhi na kuutunza msitu. Pili, hali ya kifedha ikiwaruhusu wana mpango wa kununua gari (pick-up) ili kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa shughuli za msitu, pia kurahisisha usafiri kwa wakazi wa kijiji maana kipo mbali na barabara kuu iendayo Kilwa Masoko (Makao Makuu ya Wilaya) na Lindi mjini (Makao Makuu ya Mkoa).

 

Tatu, wana mpango wa kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi; kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana na kuwasaidia vyombo vya usafiri wakazi wa kijijini hapo ambao ni walemavu. Kwa upande mwingine kijiji kikiweza kuyatimiza haya kwa kutumia rasilimali misitu waliyonayo, kitakuwa kimeisaidia Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuweza kuvihudumia vijiji vingine ambavyo havina rasilimali kama hiyo na kuviboreshea huduma za kijamii kwa kutumia fedha za kodi kutokana na vyanzo vya mapato ya Serikali.

 

Ukiwa na vijiji vingi ambavyo vitaweza kutumia fursa walizonazo na kuweza kuboresha maisha yao wenyewe, Serikali itapata fursa ya kufanya makubwa zaidi ya kuiletea maendeleo Tanzania badala ya kuhangaikia huduma za kijamii vijijini na mambo yanavyozidi kuwa mazuri Halmashauri za Wilaya na Serikali Kuu, zitapata fedha kutoka vijijini ili kuchangia maendeleo ya sehemu nyingine zisizokuwa na rasilimali muhimu kama misitu ya asili.

 

Jambo muhimu la msingi ni kwamba uongozi wa kijiji uwe imara katika kusimamia matumizi ya rasilimali zilizopo kijijini kwa faida ya wote. Vilevile, uongozi na wanakijiji wote wawe makini ili wasije wakajitokeza wezi kuwavuruga akili kwa lengo la kujinufaisha wenyewe badala ya kijiji.

 

Hii ni pamoja na kukwepa vishawishi binafsi, kuweka kumbukumbu sahihi, kuwapo hali ya uwazi na kuhakikisha kila mwanakijiji anaelewa nini kinachoendelea kwa kutoa taarifa za mara kwa mara katika vitongoji na wakati wa mkutano mkuu wa kijiji (village council meeting).

 

Dk. Felician Kilahama, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Mstaafu na Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu Duniani-chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo-FAO, Rome, Italy.