Misitu inavyoinufaisha Nanjilinji ‘A’ (4)
Pongezi kwa wananchi wa Nanjilinji ‘A’
Kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana katika Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ na kwa kuelewa kuwa mafanikio hayo yametokana na wanakijiji kudhamiria kwa dhati kutumia rasilimali misitu inayopatikana ndani ya mipaka ya kijiji chao bila kushurutishwa na mtu yeyote, napenda nichukue fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa uongozi wa kijiji na wakazi wake wote kwa mafanikio hayo ya kutia moyo.
Hii inaashiria kuwa tukiwa makini na kwa kutambua kuwa maendeleo ya kweli tutayaleta sisi wenyewe kwa kutumia vizuri rasilimali za asili tulizonazo, suala la kuboresha huduma za kijamii katika vijiji vya Tanzania linawezekana. Si tu kuboresha huduma za kijamii, bali pia kuchangia ipasavyo katika jitihada za kuondokana na umasikini uliokithiri katika vijiji vingi vya Tanzania Bara.
Kusema kweli huwa natamani sana na kumwomba Mwenyezi Mungu atujaalie rehema nyingi ili nchi yetu iwe na maendeleo ya kweli, lakini yasambae kwa haraka vijijini. Hii itawezekana kama tutatumia maliasili tulizopewa na Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na dunia na vyote viijazavyo, kwa dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo endelevu Watanzania wote.
Vilevile, nitumie fursa hii kushukuru mashirika ya MCDI na Sound & Fair kwa kuiona nguvu ya kiuchumi iliyomo katika rasilimali zetu, hususan ardhi na maliasili (misitu ya asili), katika kuwaletea maendeleo wananchi walioko vijijini.
Kwa kusaidiwa na wahisani hasa WWF-Denmark, WWF-Ofisi ya Tanzania, MCDI iliweza kuwajengea uwezo wanakijiji cha Nanjilinji ‘A’ na vilevile kuwatafutia soko la kuuza bidhaa za misitu. Kazi nzuri imefanywa kwa kiwango cha kutia moyo.
Hatuna budi kutoa shukrani kwa mashirika haya na pengine inawezekana kuna mashirika mengine ambayo sikuyataja katika makala haya, ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakiiwezesha MCDI kutekeleza mipango yao na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea ikiwa ni pamoja na kuvisaidia vijiji katika Mkoa wa Lindi kuweza kutumia rasilimali misitu.
Kumbuka usemi: “Penye nia pana njia” au “Usione vyaelea, vimeundwa”. Hivyo, uongozi na wananchi wa Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ wana kila sababu ya kusema: “Wamethubutu, wameweza na sasa wanasonga mbele”.
Changamoto
Pamoja na mafanikio mazuri niliyoyaona na kuyaeleza katika makala hii, bado wananchi wanakabiliwa na changamoto kama ifuatavyo:
(i) Kuna utata wa mpaka kati ya Nanjilinji ‘A’ na Kijiji cha Mizui kilichopo wilayani Liwale. Wanakijiji wa Nanjilinji ‘A’ walilalamikia mzozo wa mpaka na waliomba uongozi wa Halmashauri ya Kilwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wawasaidie ili kupatikane ufumbuzi wa haraka hivyo kuwezesha wakazi wa vijiji hivi viwili kuendelea na shughuli za kujiletea maendeleo kwa amani.
(ii) Baadhi ya wakulima kuvamia eneo la msitu kwa lengo la kulima hivyo, Kamati ya Msitu na Serikali ya Kijiji wana dhima kubwa ya kudhibiti uharibifu huo na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wanaoufanya kwa faida zao.
(iii) Soko la uhakika ni changomoto yenye kuangaliwa kwa umakini. Wanakijiji wanaweza kukata tamaa kwa kuona hakuna tena soko la uhakika. Kinachonipa moyo ni kuwa duniani kote hakuna ambako mahitaji na matumizi ya mazao ya misitu, iwe ni katika nchi zinazoendelea au zilizoendelea, hayapo. Katika hali ya kawaida mahitaji (demand) ya mazao ya misitu ni makubwa kuliko upatikanaji na usambazaji (supply).
Vilevile, tusiangalie soko la nje tu hata hapa nchini mahitaji ya mazao ya misitu ni makubwa, mathalan mahitaji ya mbao ya vipimo na aina mbalimbali za miti. Matumizi ya mkaa nchi nzima ni makubwa kiasi cha kutishia uhai wa misitu. Matumizi ya nguzo na kuni pia ni kwa kiwango kikubwa. Iwapo vijiji vyenye rasilimali misitu vitajipanga vizuri na kusimamia utunzaji wake pia kuhakikisha matumizi yanakuwa endelevu soko lipo na vitanufaika wakati wote.
Matarajio na mwelekeo
Kwanza niseme kinachofanyika katika Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ ni ishara nzuri ya kuwa dhana ya kutegemea wawekezaji au misaada kutoka nje ya nchi hasa kwa nia nzuri ya kuboresha huduma za kijamii vijijini ni fikra za kutokujiamini.
Pili, wananchi wa kijiji hiki wanathibitisha kuwa hakuna atakayekuja Tanzania kuwekeza iwapo hakuna rasilimali za kumvutia awekeze.
Kusema kuwa wanahitaji uwepo wa siasa safi, uongozi bora na amani ni vichocheo tu kwa shughuli zao, lakini cha muhimu sana ni kujua nchini Tanzania kuna nini kama rasilimali gani zipo? Kwa kuzingatia kuwapo rasilimali muhimu kama ardhi, misitu, madini, mafuta na gesi asilia, wanyamapori wa kutosha, samaki wengi kutokana na kuwapo bahari, mabwawa, maziwa na mito mingi; hayo mengine ni ya ziada.
Kuwapo kwa rasilimali kama hizi vijijini kunawavutia baadhi ya wawekezaji kwenda huko na kuwalaghai wananchi, ili wapewe fursa ya kuwekeza kwa kutumia rasilimali ardhi ya kijiji kwa kisingizio kuwa wanakijiji watanufaika kwa kuwaboreshea huduma za kijamii, kwa mathalani, kujenga shule, nyumba za walimu, vituo vya afya, kusambaza huduma ya maji na kadhalika.
Je, umewahi kujiuliza swali kwa nini hawa watufanyie hayo kwa mgongo wa kutumia rasilimali zetu? Je, wanatusaidia kweli au wanajisaidia kwanza na hatimaye “kutupaka mafuta kwa mgongo wa chupa” kwa kutufanyia hayo ambayo mimi nathubutu kusema kuwa yako katika uwezo wetu iwapo mipango yetu ya kutumia rasilimali tulizonazo itaandaliwa na kutekelezwa kwa dhamira ya kujiletea maendeleo endelevu sisi wenyewe?
Ndiyo maana nathubutu kusema kuwa Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ kimeonesha mfano mzuri wa kutumia walicho nacho kwa faida yao bila ya kuegemea sana kwenye misaada kutoka kwa wawekezaji. Walichokihitaji ni uwezo wao wa kufikiri, kupanga na kutekeleza shughuli zao. Ingawa Shirika la MCDI limewasaidia, si kwa kutumia rasilimali zao, bali kuwajengea uwezo na wao wakatekeleza ipasavyo.
Kawaida Serikali inahitaji fedha nyingi kuweza kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu, ikiwamo kuboresha huduma za kijamii vijijini na mijini. Chanzo kikuu cha mapato ya Serikali ni kodi na tozo mbalimbali kwa bidhaa na huduma zinazotolewa nchini. Ni vema sisi kama wazalendo wa nchi yetu tukajivunia kulipa kodi kwa nia ya kuiwezesha Serikali kutuboreshea huduma mbalimbali mfano, kujenga barabara na kuimarisha miuondombinu na huduma nyinginezo za kijamii.
Serikali za Mitaa (halmashauri za wilaya) zimepewa jukumu la kuvipatia vijiji huduma za kijamii au kuboresha zilizopo wakati huo huo Serikali Kuu ikijitahidi kuzisaidia kwa kuzipatia ruzuku ili kutimiza malengo. Kazi ya kutoa huduma bora za kijamii na kujenga miundombinu imara katika nchi yenye eneo kubwa ukilinganisha na mataifa mengine yanayotuzunguka ni dhima kubwa na yenye kugharimu fedha nyingi.
Shughuli hii inahitaji ujasiri mkubwa na uzalendo wa hali ya juu. Kinachonipa faraja ni kuwa nchi ni kubwa, lakini pia imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili. Ingawa kuna usemi kuwa “ukubwa wa pua siyo wingi wa kamasi” usemi huu kwa nchi yetu hali ni tofauti kwa maana kuwa ni nchi kubwa na yenye rasilimali za kutosha ikiwamo rasilimali watu.
Dk. Felician B. Kilahama, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Mstaafu na Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu Duniani-chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo-FAO, Rome, Italy.