Misitu ya Asili na Maendeleo ya Jamii Tanzania (Hitimisho)

Wiki iliyopita, Dk. Kilahama alianza kuainisha manufaa ambayo wananchi vijijini watapata kutokana na Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu Vijiji. Hii ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala ya ‘Misitu ya Asili na Maendeleo ya Jamii Tanzania’

(iv) Miongozo mbalimbali ya kusaidia watendaji vijijini ikiwamo Serikali za vijiji kuandaa sheria ndogo, iandaliwe na wahusika waelimishwe namna ya kuitekeleza;

 

(v) Juhudi za makusudi  zifanywe na Serikali kusaidia na kuwezesha jamii au watu binafsi kuanzisha miradi mbalimbli ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki au samaki na kuanzisha vitalu vya miche ya miti ili wapate miche mingi na kuipanda katika maeneo yao kwa matumizi ya baadaye.

 

Kazi ya kusaidia vijiji vitumie rasilimali na fursa walizonazo, hasa ardhi na misitu ya asili, ni kubwa na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha kuwa misitu mingi ya asili inawekwa chini ya usimamizi shirikishi wa misitu kwa faida ya vijiji na jamii kwa jumla.

 

Mkazo zaidi uwekwe kwenye misitu mikubwa na ile yenye rasilimali za misitu za kutosha ili kuhakikisha kuwa jamii zinashiriki kusimamia misitu hiyo na hatimaye kunufaika ipasavyo kutokana na usimamizi thabiti.

 

IWE MWIKO KWA MISITU YA ASILI VIJIJINI KUGEUZWA SHAMBA LA BIBI AMBAPO KILA MTU ANAINGIA NA KUFANYA ANAVYOTAKA.

 

Uongozi vijijini uwe makini na kuhakikisha rasilimali misitu ndani ya mipaka ya vijiji wanavyoviongoza haitumiki kama kwamba haina mwenyewe. Naomba nitoe wito kwa Serikali katika ngazi zote pamoja na asasi za kiraia na zisizo za kiserikali, kutoa kipaumbele katika suala zima la kuvisadia vijiji ili vinufaike na rasilimali misitu ndani ya mipaka ya vijiji husika.

Hii ni pamoja na:

i. Kuendelea kuelimisha jamii nzima ili dhana ya kutumia rasilimali misitu vijijini kwa misingi endelevu iweze kufanikiwa. Vilevile, elimu ya uhifadhi itawezesha wanavijiji na jamii kwa jumla kuhakikisha kuwa shughuli za kutunza misitu zinafanyika kwa umakini sana hasa katika kusimamia na kuhakikisha kunakuwapo matumizi endelevu ya rasilimali misitu.

ii. Kuhakikisha vijiji vinaandaa na kuratibu utaratibu mzuri wa kugawana mafao (benefit sharing) yatokanayo na usimamizi wa misitu wa pamoja. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa malengo ya kutumia rasilimali za misitu kuboresha hali ya maisha ya jamii zinazoshiriki kusimamia misitu yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa.

iii. Kuimarisha ushirikiano na wadau wengine walio nje ya mipaka ya kijiji ikiwa ni pamoja na taasisi zisizokuwa za kiserikali na washirika wa maendeleo, kwa lengo la kufanikisha vizuri uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali misitu vijijini.

Mimi naamini kuwa tukiwa makini na kufanya kazi kwa moyo mkunjufu tutawakwamua Watanzania wenzetu wengi waliopo vijiji. Hao wanakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo kujikuta katika ‘dimbwi’ kubwa la umasikini wakati rasilimali ardhi na misitu vipo.

 

Tutakuwa tumetimiza wajibu wetu ipasavyo. Wote kwa pamoja tushirikiane – wanasiasa, wataalamu wote (hasa wa fani au taaluma za kilimo, misitu, nyuki, mifugo, afya, elimu, maendeleo ya jamii, maji, wanyamapori, uvuvi, mazingira, uhasibu na mipango), viongozi wa madhehebu na asasi za Serikali na zisizo za Serikali, lengo letu liwe ni kuinua kiwango cha maisha kwa Watanzania waishio vijijini kwa kutumia fursa zilizopo.

 

Hakuna siri katika hili tukidhamiria na kuwa wakweli na wawazi katika fikra zetu na matendo tutaweza na mafanikio yataonekana. Mwenyezi Mungu atusaidie na kututia nguvu.

Tusifurahie lugha za uwekezaji za kusambaza maji vijijini, kuboresha elimu, kuinua viwango vya huduma ya afya, kuimarisha miundombinu: vyote hivi tunaweza kuvifanya wenyewe iwapo tutakuwa makini katika kuvisaidia vijiji kutumia vizuri rasilimali zilivyonazo

 

Mathalani, katika mikoa ya Lindi na Mtwara bado kuna maeneo mazuri yenye misitu na miti ya thamani sana kama mipingo (Dalbergia melanoxylon), lakini miti hiyo inatumiwa visivyo kwa kutengeneza mkaa au kuivuna kama kuni au kufyeka eneo na kulichoma moto kwa minajili ya kuanzisha mashamba. Hili lazima likomeshwe sasa.

 

Iwapo kuna wawekezaji vijijini na wenye dhamira nzuri ya kuvisaidia vijiji viboreshe hali ya maisha yao; hawana budi kununua rasilimali zilizopo vijijini kama mipingo kwa bei nzuri na fedha zitakazopatikana zitumike kuboresha huduma za kijamii.

 

Vilevile, mwenendo wa biashara ya kuuza na kununua gesiukaa uwe wa kunufaisha vijiji zaidi kuliko kufaidisha kampuni za kigeni. Ni vizuri wawekezajii wenye nia nzuri ya kuchangia maendeleo ya Tanzania wakawasaidia wanavijiji kutumia ardhi waliyo nayo kuotesha miti itakayonyonya gesiukaa kutoka angani, na katika jitihada hizo wawekezaji wakainua hali za vijiji kwa kununua gesiukaa kwa bei itakayoashiria kuboresha hali ya maisha vijijini na siyo kinyume chake.

 

Iwapo wataona kuwezesha vijiji au kwa watu binafsi kuweza kuotesha miti hakuna motisha kwa wawekezaji, ni vema miti ipandwe kwa njia ya ubia (partnership) na mtaji wa kijiji au mtu binafsi uwe ni ardhi aliyonayo na mapato yatakayopatikana yagawanywe kwa kiwango cha asiliamia 40 kwa wageni na asilimia 60 kwa mwenye ardhi.

 

Kwa mwelekeo wa aina hiyo, uwekezaji utasaidia kuinua hali ya maisha vijijini. Hakuna kisichowezekana. Kuondoa umasikini katika nchi yetu ni jambo linalowezekana. Kinachotakiwa ni kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo na kwa kutendeana haki. Tukifanya hivyo, nina imani tutafanikiwa. MWENYEZI MUNGU ATUSAIDIE.

 

Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012. Anapatikana kwa simu na. HYPERLINK “tel:0756%20007%20400”0756 007 400.