Leo Mei 19, 2024 katika mji wa Shanghai China yamefanyika matembezi ya kitalii(Roadshows) ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China na uzinduzi wa mwaka wa utalii na utamaduni uliofanyika Mei 15, 2024.
Washiriki zaidi ya 250 wamejitokeza katika matembezi hayo ambapo wamepata nafasi ya kukutana na wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka Tanzania lengo ikiwa ni kutafuta namna ya kuongeza watalii kutoka China.
Wadau hao kutoka China wameibua changamoto mbalimbali zinazokwamisha Wachina kuja Tanzania ikiwemo kutokuwepo kwa Hoteli nyingi zenye huduma na tamaduni za China, Uhaba wa waongoza watalii wanaozungumza lugha ya kichina pamoja na ndege za mara kwa mara zinazoenda moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania.
Akizungumza mara baada ya hafla hiyo Katibu wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa amesema wao kama Serikali wamezipokea changamoto hizo na kuwa wapo tayari kuzifanyia kazi mara moja ili watalii kutoka China waongezeke maradufu.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania(TTB), Ephraim Mafuru amesema misafara hiyo inalenga kutangaza utalii wa Tanzania na ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kufanya filamu ya “Amazing Tanzania” kwa kushirikiana na msanii maarufu kutoka China, Jin Dong.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mbarouk, watendaji na wawakilishi kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Eneo la Ngorongoro (NCAA).
Misafara mingine ya kitalii itafanyika jijini Guangzhou, China tarehe 21-22 Mei, 2024.