Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na msaada wa fedha zilizotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kuimarisha miradi itakayoongeza tija na ufanisi katika sekta mbalimbali ambayo inatekelezwa nchini.

Akizungumza jana jijini Dodoma mara baada ya kushuhudia uwekaji saini wa mikataba mitatu ya makubaliano ya fedha kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU),Dkt. Samia alisema “Misaada hii ni muhimu na itasaidia na kuongeza kasi katika utekeleza miradi ya maendeleo katika nchi yetu.

Nikiwa ziarani Brussels Februari mwaka 2022 nilipata fursa ya kufanya mazungumzo na Rais wa Tume ya Ulaya na nimefurahi kwa kuwa moja ya matokeo ya mazungumzo yale ni uundwaji wa programu zilizosababisha haya malipo ya pili ambayo ni Euro milioni 46.11 baada ya malipo ya kwanza Euro milioni 21 iliyotolewa mwezi Juni 2022”.

Alisema kuwa malipo hayo yataekelezwa katika mageuzi ya sera, uchumi wa buluu, ukuaji wa fedha, jinsia, kupendezesha miji, kuboresha sekta ya kidigitali na maboresho ya barabara za vijijini katika mikoa ya nyanda za juu kusini.

Aidha, Rais Mhe. Dkt. Samia aliongeza kuwa kwa muda mrefu EU ni moja wa washirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania na imejidhihirisha kupitia misaada yake inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti alisema kuwa anategemea kuwa mchango wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kupitia mikataba hiyo utaleta chachu katika maeneo yenye fursa za kukua katika ubunifu.

“Ushirikiano wetu unatabirika kutokana na ushirikiano mzuri wakati wa uandaaji wa miradi, nampongeza Mhe. Rais Samia katika mabadiliko ya kisera yanayolenga katika kuleta usawa wa kijinsia, aidha, Umoja wa Ulaya tunaunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia”, alisema Mhe. Balozi Fanti.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba alitaja mikataba mitatu iliyowekwa saini kati ya Serikali ya Tanzania na EU kuwa ni Mkataba wa Uchumi wa Buluu utakaosaidia kuleta mabadiliko ya tabia nchi katika pwani za Tanzania na Zanzibar wenye thamani ya Shilingi milioni 279.20.

Kuimairisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Serikali na Kukuza Sekta Binafsi wenye thamani ya Shilingi bilioni 160.79 na kuimarisha mahusiano kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania katika Kuongeza ufanisi wa kubuni miradi inayofadhiliwa na EU wenye thamani ya shilingi bilioni 15.23.