Imeelezwa kuwa, utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati safi ya kupikia vijijini umeiwezesha Tanzania kung’ara katika Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW 69) unaofanyika jijini New York, nchini Marekani kuanzia tarehe 11 hadi 22 Machi, 2025.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Advera Mwijage amesema kuwa, Tanzania inatekeleza kwa vitendo maazimio ya Mkutano wa Beijing ya kuleta usawa wa kijinsia. 

Amesema kuwa, kwa kusambaza miradi ya nishati safi ya kupikia imesaidia kupunguza adha ambazo wanawake wanakabiliana nazo za kutumia muda mwingi wa kwenda kutafuta kuni pamoja na kupata magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa. 

“Utekelezaji wa miradi hiyo unachangia kuboresha ustawi wa maisha ya wanawake wa vijijini na ni azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya Kupikia, ” Amesema Mha. Mwijage. 

Awali, akifungua mjadala huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Mhe. Anjella Kairuki amesema kuwa utekelezaji wa Miradi ya nishati safi ya Kupikia utaleta mabadiliko chanya kijamii yatakayochangia kuboreha mazingira, afya na uchumi wa mwanamke.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Nyumba na Makazi, Bi. Lucy Kabyemera amesema kuwa utekelezaji wa Miradi ya nishati safi ya Kupikia unatoa fursa za biashara kwa kuuza bidhaa mbalimbali za nishati safi.