Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,
Songea

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Mkoa wa Ruvuma,katika kipindi cha miezi sita imefuatilia jumla ya miradi 31 yenye thamani ya Sh.bilioni 19,681,124,604.63 kati ya hiyo miradi mitano yenye thamani ya Sh.bilioni 7,053,240,916.51 imebainika kuwa na mapungufu.

Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani Ruvuma Janeth Haule alitaja miradi iliyokutwa na upungufu ni ya sekta ya elimu,miundombinu na barabara na hatua mbalimbali zimechukuliwa na ili kuondoa mapungufu hayo.

Alitaja miradi hiyo ni ujenzi wa soko katika Halmashauri ya Madaba wenye thamani ya Sh.milioni 171,176,339.00 ambapo bati 98 zimenunuliwa zaidi ya mahitaji na manunuzi ya Terazo kinyume na taratibu za manunuzi.

Miradi mingine ni mradi wa maji Nangombo-Kilosa unaojengwa na Mkandarasi Contructions Of Gravity Pumping Water Supply kwa gharama ya Sh.bilioni 4.1 ambaye ameshindwa kuendelea na kazi kutokana na kuisha kwa mkataba kabla hajamaliza kazi.

Aidha mradi mwingine ni ukarabati wa Zahanati ya Litolomelo wenye gharama ya Sh.milioni 50 ambao kamati ya manunuzi na mapokezi zilifanya udanganyifu kwenye fedha za ukarabati na kupokea vifaa vya ujenzi wa mradi huo vikiwa pungufu.

Kwa mujibu wa Haule,mradi mwingine uliokutwa na mapungufu ni mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Nakawale Halmashauri Namtumbo wenye thamani ya Sh.milioni 80.

Alisema,mradi mwingine ni ujenzi wa tenki la maji Mchomoro wilayani Namtumbo wenye thamani ya Sh. bilioni 2 ambapo miradi yote haijakamilika kwa muda uliopangwa.

Haule ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuendelea kuunga mkono jitihada za kufichua vitendo vya rushwa na wala rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa.