Serikali imesema kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa mwaka 2022 kimesajili miradi 293 ikilinganishwa na 256 iliyosajiliwa mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.5.
Hayo yamebainishwa leo Juni 16, 2023 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba,alipowasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa katika mwaka 2022.
Kati ya hiyo, miradi 99 ilikuwa ya Watanzania, huku 112 ikiwa ni ya wageni na miradi 82 ni ubia kati ya Watanzania na wageni.
Amesema thamani ya miradi iliyosajiliwa ilikuwa Dola za Marekani 4,537.7 milioni mwaka 2022 ikilinganishwa na Dola 3,749.3 milioni za mwaka 2021.
Amesema miradi iliyosajiliwa ilikuwa na fursa za ajira 40,889 mwaka 2022 ikilinganishwa na 53,025 mwaka 2021.
Amesema sekta ya uzalishaji viwandani iliongoza kwa kusajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani 3,277.0 milioni ikifuatiwa na ya usafirishaji Dola 647.7 milioni na ya ujenzi wamajengo ya biashara Dola 184.2 milioni.