Na Mwandishi Maalumu, JamhuriMedia,Dar es Salaam
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi milioni 950 ambazo Serikali ingetumia kama watoto 37 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu hayo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirikal la Mending Kids lililopo nchini Marekani Daktari bingwa wa upasujai wa moyo kwa watoto wa JKCI Godwin Sharau alisema watoto 16 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kuziba matundu, kurekebisha valvu za moyo na mishipa ya damu ambayo haikuwa sawa.
Dkt. Godwin amesema kama watoto hao 16 waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wangepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu gharama za kupatiwa matibabu yao zingekuwa shilingi milioni 250 wakati matibabu hayo kwa kufanyika JKCI yamegharimu kiasi cha shilingi milioni 90 na baadhi ya watoto kupatiwa msamaha wa matibabu kutokana na hali zao za kiuchumi kutomudu gharama za matibabu.
“Katika kambi hii tumeweza kuwafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto wa umri tofauti kuanzia mwezi mmoja hadi miaka mitano ambapo mtoto wa mwezi mmoja alikuwa na matatizo manne katika moyo wake ikiwemo tundu katika vyumba vya juu vya moyo, tundu katika vyumba vya chini vya moyo, mishipa inayorudisha damu kutoka kwenye mapafu kupeleka damu upande wa kulia wa moyo badala ya kuipeleka upande wa kushoto na mshipa wa PDA unaotakiwa kujifunga baada ya mtoto kuzaliwa kutokujifunga”, amesema Dkt. Godwin.
Dkt. Godwin amesema huu ni mwaka wa kumi tangu Taasisi hiyo ianze kushirikiana na Shirika la Mending Kids ushirikiano ambao umezaa matunda mazuri kwani kila mwaka wataalam wa shirika hilo wanavyofika JKCI ufika na mbinu mpya za matibabu pamoja na kutoa vifaa vya matibabu kwa watoto bila gharama.
“Upasuaji wa moyo kwa watoto katika nchi zilizoendelea umepiga hatua sana, Taasisi yetu inakuwa kwa kasi katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto ndio maana tunaendelea kufanya ushirikiano na nchi zilezoendelea lengo likiwa kukuza ujuzi wetu pamoja na kuwa na ubora wa huduma tunazozitoa kwa wagonjwa wetu”, amesema Dkt. Godwin.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema upande wa matibabu ya upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab watoto 21 waliokuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu na mishipa ya damu iliyobana wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Dkt. Stella alisema matibabu ya upasuaji mdogo wa moyo kwa watoto 21 yamegharimu chini ya shilingi milioni 100 kwa kufanyika hapa nchini tofauti na watoto hao kama wangepelekwa nje ya nchi matibabu yao yangefika kiasi cha shilingi milioni 700.
“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha huduma za afya zikiwemo huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na kupunguza idadi ya watoto wanaopelekwa nje ya nchi kwani kwa kufanya hivyo imeweza kuokoa fedha nyingi ambazo zingehitajika kwa ajili ya matibabu nje ya nchi”, amesema.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa watoto kutoka Shirika la Mending Kids lililopo nchini Marekani Darren Berman alisema madaktari kutoka shirika hilo wataendelea kushirikiana na madaktari wa JKCI kwa karibu, kubadilishana ujuzi na kuwasaidia watoto wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo.
“Kupitia kambi zetu za matibabu ya moyo hapa JKCI tumeweza kuwasaidia watoto wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu na kwa wiki hii tumeweza kumfanyia upasuaji wa tundu dogo mtoto wa miezi nane aliyekuwa na tundu kwenye moyo ambapo kupitia matibabu tuliyompa tumeweza kuokoa maisha yake”, amesema Dkt. Darren.
Dkt. Darren Berman alisema utaalamu wa kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto JKCI umeongezeka hivyo sasa hakuna haja ya watoto watanzania wenye magonjwa ya moyo kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Naye mama ambaye mtoto wake amepatiwa matibabu katika kambi hiyo Prisca Elius aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kumsaidia mtoto wake kupata matibabu kupitia kambi hiyo kwani hakuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya mtoto wake.
Prisca alisema baada ya kuambiwa kuwa mtoto wake ana tatizo la moyo alipoteza matumaini kwani hakujua ni kwa namna gani angefika Dar es Salaam na angepata wapi fedha kwa ajili ya matibabu.
“Nawaomba madaktari wa JKCI na wenzenu kutoka nchini Marekani muendelee kuwa na moyo huu wa kutusaidia sisi tusiokuwa na uwezo, mmetusaidia sana maana nilishaambiwa tatizo alilokuwa nalo mwanangu nisipomtibu nitampoteza, nawashukuru sana”, amesema Prisca