Uongozi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) unakabiliwa na tuhuma za kukilipa kiwanda cha pamba kilichofilisika, Sh milioni 826 bila maelezo ya kuridhisha.
Malipo haya tata yanaelezwa kuwa yamesukumwa na watendaji wa NIC, ambao wanafanya kazi bila mikataba.
Fedha zimelipwa Desemba 2012 kwa kiwanda cha kuchambua pamba kinachodaiwa kufilisika siku nyingi cha jijini Mwanza kilichofungua madai ya Sh milioni 104 mwaka 2003, lakini kimeishia kulipwa mamilioni hayo mwaka jana.
Watendaji wakuu wa NIC inasemekana wameshirikiana na watu wasio waaminifu, kulipa kiasi hicho cha fedha, kutoka akaunti ya NIC iliyopo NBC Makao Makuu Na. 011103002789 baada ya kupata amri ya Mahakama Kuu ya Biashara.
Viongozi wakuu wa NIC karibu wote mikataba imekwisha Desemba, mwaka jana, hivyo kati yao wapo walioamua ‘kuchukua chao mapema’.
NIC wamekuwa wakifanya ununuzi kwa bei za kutisha. Hivi karibuni, wamenunua server za kompyuta nne kwa gharama ya Sh milioni 60, wakati wangeweza kutumia Sh milioni 25 wakanunua ‘server’ moja ikafanya kazi kwa usahihi.
Wafanyakazi wanalalamika kuwa NIC imeingia mkataba na kampuni moja kuanzia Januari hii, itakayotengeneza mawasiliano ya kompyuta ofisi za Makao Makuu Dar es Salaam (Active Directory) kwa gharama ya Sh milioni 53.7.
Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa NIC uliisha Julai, mwaka jana.
Matokeo yake, watendaji wakuu wa NIC wanasafiri kila kukicha hadi wastani wa siku 28 kwa mwezi, na kuishia kuvuna mamilioni ya shilingi.
Juhudi za kumpata Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIC, Justine Mwandu, hazikuzaa matunda. Meneja Uhusiano wa NIC, Mwanaidi Shemweta, aliiambia JAMHURI kuwa walikuwa na msiba hivyo asingeweza kulizungumzia suala hili mwishoni mwa wiki.