Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Kiasi cha Shilingi Milioni 466 zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi vya Wanawake, Vijana, na Watu wenye Ulemavu kama mkopo wa asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.

Akikabidhi hundi kwa vikundi vya wanufaika wa mkopo ,Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, amesema kuwa Serikali inatarajia wananchi kufanya maendeleo makubwa kiuchumi baada ya kuwezeshwa kupitia mikopo hiyo.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Endapo mtaenda kinyume na malengo ya mikopo hii, mtakuwa mmejiondoa kwenye mwelekeo wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kamati ya uhakiki wa mikopo. Hivyo, hakikisheni mikopo hii inatumika kama ilivyokusudiwa na mkiwa na dhamira ya kufanya marejesho kwa wakati,” alisema Mhe. Mangosongo.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Juma Salum, amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kuhakikisha wanazingatia taratibu zilizowekwa katika biashara zao, ikiwemo ulipaji wa leseni za biashara na ushuru, ili wananchi wengine waweze kufaidika na fursa hiyo.

Wanufaika wa mikopo akiwemo Hajji Muarabu alishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya wananchi na kuahidi kuwa watakuwa waaminifu katika marejesho.

“Kabula ya kupata mkopo, nilikuwa na biashara ndogo, lakini nilipopata taarifa za mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, nikaamua kuomba na kufanikiwa kupata mkopo. Nimekuwa nikipunguza kwa wakati, na sasa tena nimeomba,” alieleza Haji Mwarabu, mfanyabiashara wa samaki mwenye ulemavu kutoka kata ya Kanga, Bweni.

“Natoa wito kwa wananchi wenzangu kuomba mikopo na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati,” aliongeza.

Halmashauri ya Wilaya ya Mafia inatarajia kufungua dirisha la pili la uombaji wa mikopo ya asilimia 10 ifikapo Januari 31, 2025.