Mpigania haki za weusi na alama kuu ya udhalimu wa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Mzee Nelson Madiba Mandela, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu, kutokana na maambukizo ya mapafu kushindwa kutengamaa.
Mzee Mandela amefariki dunia nyumbani kwake jijini Johannesburg, ambako alipelekewa akitokea Hospitali ya Moyo ya Mediclinic jijini Pretoria, Afrika ya Kusini baada ya familia yake kuomba arejeshwe nyumbani.
Alipelekwa hospitalini Juni 8, mwaka huu baada ya kusumbuliwa tena na ugonjwa wa mapafu. Ugonjwa huu anadaiwa kuupata akiwa kifungoni. Mandela alipata ugonjwa wa kifua kikuu (TB) mwaka 1982 kutokana na kazi ngumu ya kupasua mawe kama sehemu ya adhabu ya kifungo chake.
Alitolewa hospitalini hapo Septemba 1, 2012 baada ya familia kuomba hivyo na kuahidiwa huduma nzuri ya kitabibu akiwa nyumbani. Wakati anaondoka hospitali, hali yake ikiwa imeimarika kidogo ingawa kulikuwapo na tishio la maisha yake.
Kinyume na matarajio ya wengi kutokana na taarifa za kutia matumaini zilizokuwa zikitolewa, taa ya Mzee Madiba wiki iliyopita imezimika. Historia ya Mandela ni ndefu na yenye kuvutia.
Mandela (95) alikuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, kutokana na kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliofanywa na makaburu kwa karibu karne moja, ila ukafikia kilele mwaka 1948 pale ilipotangazwa rasmi sera ya Ubaguzi wa Rangi (apartheid policy).
Wazungu walitangaza kusitisha haki zote za kiraia kwa Waafrika weusi. Hakuna aliyeruhusiwa kupiga kura, kupanda magari walimopanda Wazungu, kumiliki ardhi, kugombea nafasi yoyote ya kisiasa, na ilikuwa mwiko kabisa Mwafrika kumuoa Mzungu.
Mwaka 1943, Mzee Mandela alijiunga na Chama cha African National Congress (ANC), kisha akateuliwa kuwa kiongozi wa tawi la Umoja wa Vijana. Ikumbukwe wakati huo, Mandela alikuwa tayari ameingia kwenye vuguvugu (movements) la kudai mageuzi na alianza masomo ya sheria.
Wakati akiendelea na harakati, mwaka 1962 Serikali ya makaburu iliyokuwa ikimfungulia kesi nyingi kadiri ilivyowezekana, ilimkamata na kumfungulia mashitaka, ambapo hatimaye alitiwa hatiani na kufungwa maisha.
Mandela alitumikia kifungo kwa miaka 27 jela, huku akitumikia miaka 18 katika Kisiwa cha Robben.
Pamoja na kazi ngumu jela, aliendelea kuongoza kundi la wapigania haki wengine kudai usawa, utu, na umoja wa Waafrika Kusini.
Mandela ndiye mfungwa maarufu zaidi wa kisiasa duniani. Harakati za kutaka afunguliwe zilipiganwa na wanaharakati sehemu mbalimbali duniani licha ya upinzani wa Serikali ya Afrika Kusini na baadhi ya nchi za Magharibi, ambazo zilimuona Mandela kama gaidi na mchochezi.
Maisha yake ya awali
Mzee Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, mji mdogo wa Umtatu, Jimbo la Cape. Akiwa ni mmoja wa watoto wa Mzee Gadla Henry Mphakanyiswa, Nelson Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu wa Mzee Gadla – katika Kijiji cha Qunu, ambako pamoja na shughuli nyingine za nyumbani alikuwa mvulana mchunga ng’ombe.
Baadaye alianza masomo ya shule ya msingi na sekondari ambapo aliamini kuwa alikuwa anaandaliwa kwa ajili ya utumishi katika nyumba ya Chifu wa Kabila lake la Xhosa kama mshauri.
Hata hivyo, baada ya kurudi nyumbani kutoka masomoni mwaka 1940 alikuta Chifu Jongintaba amemwandalia ndoa Mandela na mtoto wa kiume mwingine wa Chifu huyo aitwaye Justice. Kwa pamoja walitoroka nyumbani na kukimbilia jijini Johannesburg.
Alifanya kazi kama mlinzi katika kampuni ya madini ya Crown, lakini alifukuzwa kazi na msimamizi wa kampuni hiyo, baada ya kugundulika kuwa alikuwa ametoroka kwao. Mandela alianza kuishi na binamu zake.
Kuingia katika siasa
Akiwa na binamu zake, Mandela alitambulishwa kwa mwanaharakati wa chama cha ANC, Walter Sisulu. Sisulu alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya Wanasheria ya Witkin, Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya masomo ya elimu kwa njia ya posta kupata shahada ya kwanza ya sheria.
Mwaka 1943 alihitimu masomo yake ya sheria na kuanza kazi kama mwanasheria badala ya kurudi kijijini kutumika kwa chifu. Akiwa ameanza kazi kama mwanasheria, Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi wa Sisulu, ambaye alikuwa anaendeleza harakati za kudai haki za weusi.
Alikutana mara kwa mara na wanaharakati wengine nyumbani kwa Sisulu. Mandela alikutana pia na rafiki yake, Oliver Tambo. Ilikuwa ni katika mikutano hiyo alipokutana na mwanamama Evelyn Mase, ambaye walianza uhusiano wa kimapenzi na baadaye kufunga naye ndoa ya kwanza Oktoba 1944.
Walijaaliwa watoto wanne — wa kiume Madiba “Thembi” Thembikile alizaliwa Februari, 1945 na Magkatho Mandela aliyezaliwa mwaka 1950, akafariki 2005 na wa kike Makenzie alizaliwa mwaka 1948, lakini alifariki miezi tisa baadaye baada ya kupata maambukizo ya ugonjwa uti wa mgongo.
Evelyn alizaa tena mtoto mwingine, akaitwa Makenzie kama dada yake aliyetangulia mbele ya haki. Makenzie huyu alizaliwa mwaka 1954 na yuko hai hadi leo. Jumla Mandela ameacha wajukuu 17.
Baada ya uchaguzi wa 1948 ambapo watu weupe peke yao walishiriki vyama vya Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party viliungana na kuunda chama cha National Party, ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya ubaguzi na kikaongeza ukali wa sera ya ubaguzi kupitia sheria mbalimbali za ubaguzi wa rangi.
Serikali ya kikaburu ilitunga mojawapo ya sheria kali kupambana na wanaharakati ambayo inajulikana kama Ukandamizaji wa Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa inashughulikia karibu mambo yote yanayohusu kuipinga Serikali na ikiwahusu watu wote. Migongano kati ya ANC na serikali ya kikaburu ilianza kupamba moto.
Mwaka 1952 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa makaburu kwa kilichodaiwa kujihusisha na vitendo vya kikomunisti chini ya sheria iliyopitishwa miaka michache iliyopita.
Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi ngumu”, lakini utekelezaji wa hukumu hiyo ulisitishwa kwa miaka miwili. Desemba mwaka huo huo Mandela alipigwa marufuku kuzungumza na zaidi ya mtu mmoja kwa miezi sita.
Mwaka 1953 Mandela na rafiki yake Oliver Tambo walifungua kampuni yao ya wanasheria katika Jiji la Johannesburg na kuifanya kuwa kampuni ya kwanza ya wanasheria weusi katika Afrika Kusini.
Walijishughulisha na malalamiko mbalimbali ya wananchi hasa yanayohusu ukatili wa kisiasa. Hata hivyo, Serikali ikitumia sheria nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi hiyo iliyokuwa na wateja wengi na kuihamishia sehemu nyingine ambapo ilikuwa ni vigumu kwa wateja kuifikia.
Mwaka 1955 Mandela na wenzake walishirikiana kuandaa kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini, ambao wanaamini katika taifa moja la watu wamoja japo wanatoka katika makabila na rangi mbalimbali.
Katika kongamano hilo kulisainiwa mkataba unaoaminika kama mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo ilijulikana kama Freedom Charter.
Mkataba huo unafananishwa na Azimio la Uhuru la Marekani au waraka wa Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania tunaweza kuufananisha na Azimio la Arusha. Freedom Charter uliweka ramani ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa katika Afrika Kusini.
Hata hivyo, kwa upande wa familia ndoa yake na Evelyn ilianza kuwa matatani. Kulikuwa na tuhuma za kukosa uaminifu ambapo Mandela alidaiwa kuwa na uhusiano ya kimapenzi na baadhi ya kina dada wa ANC.
Evelyn alijaribu kufuata taratibu za kisheria watengane, na pamoja na jitihada mbalimbali za kuwapatanisha na Mandela, Machi 1958 waliamua kupeana talaka na mke wake wa kwanza.
Wakati huo wa mchakato wa talaka, Mandela alikuwa ameanza uhusiano na Winnie Madikizela, mmoja wa wafanyakazi wa mambo ya kijamii. Walifunga ndoa Juni 1958.
Katika ndoa ya Winnie walipata watoto Zenani Dlamini Mandela aliyezaliwa 1959 na Zindzi Mandela (1960).
Migogoro na utawala wa kikaburu haikukoma. Mandela alizidi kuwa na siasa za mlengo wa kushoto. Njia za amani za kupata mabadiliko ya kisiasa zilionekana kutozaa matunda; Mandela na wenzake walianza kuamini katika njia za kimapinduzi na za kutumia silaha. Hili lilimletea matatizo zaidi na watawala wa Kikaburu.
Hatimaye Augusti 2, 1962 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa makaburu na kushtakiwa kwa kuchochea mgomo wa wafanyakazi na kuondoka nchini bila kibali.
Ikumbukwe, hapa ziara iliyomponza Mandela ni ile aliyosafiri kuja nchini Tanganyika wakati huo, alikopewa hati ya kusafiria kwenda nchini Ethiopia kufanya mafunzo ya kijeshi. Alirejea nchini kwake baada ya kujulishwa kuwa hali imekuwa mbaya, wapigania uhuru wanaanza kukata tamaa bila uwepo wa Mandela. Alikuwa nje ya nchi kwa miezi sita.
Mandela alijiwakilishi mwenyewe mbele ya Mahakama, huku akitumia nafasi hiyo kutoa hotuba motomoto za kisiasa dhidi ya utawala wa kibaguzi wa makaburu.
Alikutwa na hatia na kuamuriwa kufungwa miaka mitano jela. Wakati anatoka mahakamani mashabiki wake walisimama pembeni na kuimba wimbo wa Mungu Ibariki Afrika (Nkosi Sikeleli Afrika).
Kesi ya Rivonia
Matatizo yake hayakufikia mwisho. Julai 11, 1963 polisi walivamia shamba la Lilliesleaf, mji mdogo wa Rivonia nje ya Johannesburg, ambako pamoja na vitu mbalimbali walidai walikuta ushahidi wa kutosha kumhusisha Mandela na mipango ya kuipindua Serikali.
Mandela na wenzake walitumia shamba hili kama sehemu yao ya kujificha huku Mandela akijifanya ni mtunza bustani. Kesi hii ilikuwa moto moto kwani Mandela na wenzake walishtakiwa kwa makosa manne yakiwa ni ya uhujumu wa miundombinu ya nchi (vitendo zaidi ya 200) pamoja na kutaka kupindua Serikali.
Serikali ilikuwa inapendekeza kuwa wakikutwa na hatia basi wahukumiwe kifo. Mashahidi wengi wa Serikali waliitwa pamoja na lundo la ushahidi wa picha na nyaraka kuthibitisha mashtaka ya Serikali dhidi ya Mandela na wenzake tisa.
Baadaye Mahakama ilimtia hatiani Mandela na kuhukumu afungwe jela maisha, baada ya Mahakama kudai kuwa ushahidi ulikuwa na nguvu, lakini ulikosa uthibitisho wa wazi kuwa kweli Mandela alipanga kuipindua Serikali.
Baada ya hapo ilikuwa kazi ngumu ya kutumikia kifungo cha maisha na kupasua kokoto gerezani kwa muda wa miaka 27.
Wakati Mandela na wenzake wakiwa gerezani, vuguvugu lilizidi kuwa kubwa kwa nchi za mstari wa mbele ikiwamo Tanzania na hata Marekani ambalo mwaka 1986, lilitunga sheria ya kuwawekea vikwazo viongozi wa Serikali ya Afrika Kusini.
Hali iliendelea kubana hadi Februari 11, 1990 Mandela alipoachiwa huru kutoka gerezani. Makaburu walibanwa na jamii ya kimataifa kwa kiwango ambacho wasingeweza kuvumilia, kwani walizuiwa kuuziwa silaha, kuuza bidhaa nje ya kutembelea mataifa makubwa hadi Mandela aachiwe huru.
Wengine ambao walikuwa pamoja na Mandela ni pamoja na Sisulu na Govan Mbeki. Katika kesi hiyo Mandela alitoa mojawapo ya hotuba zinazosifiwa zaidi duniani na inasomwa na wanafunzi wa siasa sehemu mbalimbali duniani kwani ilielezea falsafa ya kupinga ubaguzi wa rangi.
Mandela alisema hapiganii haki ya weusi kuwabagua weupe, bali haki ya watu wote kuishi kwa pamoja kama watu wa jamii moja.
Mandela alisema: “Haya ni mapambano ya watu wa Afrika yaliyotokana na mateso na mang’amuzi yao wenyewe. Haya ni mapambano ya kupigania haki ya kuishi. Nimelifurahia wazo la jamii ya kidemokrasia na huru, ambapo watu wote wanaishi katika amani na haki sawa. Ni wazo ambalo ninatumaini kuishi kwa ajili yake na kulitimiza. Lakini, ikibidi, mheshimiwa, ni wazo ambalo nimejiandaa kufa kwa ajili yake.”
Maneno haya Mandela aliyatoa mahakamani wakati kesi inaendelea.
Pamoja na utetezi wake, timu ya Mandela ilishindwa kesi hiyo na wote wakakutwa na hatia isipokuwa mmoja. Kwa vile tayari kulikuwa na mwamko sehemu mbalimbali duniani kupinga adhabu ya kifo, Mahakama ikawaamuru Mandela na wenzake kutumikia kifungo cha maisha na huo ndiyo ukawa mwanzo wa kifungo cha chake miaka 27 jela.
Mandela na wenzake walipelekwa katika gereza liloko katika Kisiwa cha Robben ambako pale peke yake alitumikia miaka 18. Mandela na wenzake walihukumiwa kufanya kazi ngumu pamoja na kuponda mawe kupata kokoto na baadaye kuponda mawe ya chokaa.
Kwa muda alikatazwa kuvaa miwani ya jua, kitu ambacho kilimsababishia ubovu wa macho. Akiwa kifungoni mamake alimtembelea mwaka 1968 na siku chache baadaye alifariki dunia, mwaka uliofuata mtoto wake wa kwanza, Thembi, alifariki katika ajali ya gari, lakini Mandela hakuruhisiwa kuhudhuria mazishi yao wote hao.
Maisha kifungoni yalikuwa magumu kwa kila kipimo licha ya maisha baada ya miaka kuanza kuboreshwa kidogo kutokana na maandamano na harakati za kutaka Mandela afunguliwe.
Utawala wa makaburu haukusikia kauli ya mtu yeyote hasa kwa nchi washirika wa karibu na Serikali ya Marekani na Uingereza, ambazo zote zilimuona Mandela kama mkomunisti na gaidi.
Mandela alitumikia pia katika magereza ya Pollsmoor huko Cape Town na jingine kati ya 1982 hadi 1988 na baadaye Gereza la Victor Verster 1988-1990 ambako kwa kiasi kikubwa alikuwa amepewa maisha ya unafuu kulinganisha na alivyoishi katika Gereza la Kisiwa cha Robben.
F. W. de Klerk
Chini ya utawala wa Pieter Botha, Afrika Kusini ilizama katika siasa na sera za ubaguzi wa rangi. Botha aliwachukia weusi na aliamini kabisa kuwa utawala wa kikaburu utadumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, mwaka 1989 Botha alipata kiharusi na kulazimishwa kujiuzulu, hali iliyompatia fursa Frederick W. de Klerk kutoka katika chama kilichoamini katika ubaguzi wa rangi, isipokuwa yeye alijikuta akiukataa kwani aliona hauwezi kudumu.
Kwa muda tangu 1988 Mandela alikuwa na mazungumzo ya siri na baadhi ya viongozi wa Serikali juu ya masharti ya yeye na wenzake kuachiwa huru na mwelekeo wa siasa za Afrika Kusini.
Mazungumzo hayo yalikumbana na vikwazo vingi ikiwamo kutokukubaliana na masharti. Kwa mfano, Serikali ilitaka Mandela asijiingize kwenye siasa na kuwa wasilazimishwe kuwa na utawala wa wengi (majority rule), ndipo aachiwe huru ila masharti hayo Mandela aliyakataa.
Mandela na wenzake waliachiliwa huru na utawala lwa De Klerk Februari 11, 1990. Baada ya kuachiwa huru muda mrefu ulitumika kufanya mazungumzo na utawala wa kikaburu kuhusu mwelekeo wa siasa za Afrika Kusini na hata kuelekea uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, kutokana na matukio mbalimbali ya vurugu na mauaji ya kisiasa yaliyokuwa yanaendelea na hata migongano ya chama cha Inkatha cha Chifu Mangusuthu wa Buthelezi, Mandela aliona hana jinsi isipokuwa kufikia makubaliano ya msingi.
Baadhi ya makubaliano hayo yalihusisha kufunguliwa kwa wafungwa wa kisiasa, kuitishwa kwa uchaguzi mkuu, kuwa na Katiba ya mpito na kuhakikisha kuwa weupe wasingefukuzwa kazi iwapo utawala wa weusi ungeingia madarakani.
Mandela na De Klerk walitunukiwa tuzo ya Nishani ya Amani ya Nobel mwaka 1993 kwa pamoja kutokana na kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Uchaguzi Mkuu wa 1994
Afrika Kusini iliingia katika uchaguzi mkuu wa kwanza huru ulioshirikisha wananchi wote Aprili 27, 1994. Kampeni zilikuwa na vurugu za hapa na pale, lakini kwa ujumla wananchi wa Afrika Kusini, hasa weusi walijikuta kwa mara ya kwanza wanapiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Mandela akiongoza ANC walishinda kwa asilimia 62 ya kura na kushindwa kupata theluthi mbili ambayo ingewawezesha kubadili Katiba. Serikali yake ilikuwa ni ya umoja wa kitaifa ikitegemea kwa kiasi kikubwa baadhi ya maofisa waliokuwa katika utawala wa kikaburu. De Klerk alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Thabo Mbeki akiwa Makamu wa Pili wa Rais.
Mandela aliiongoza nchi hiyo kwa kipindi kimoja na kutangaza kuwa hatagombea kipindi pili na kumwachia Thabo Mbeki kuwa Rais wa Afrika Kusini.
Baada ya kustaafu siasa, Mandela aliamua kujishughulisha na masuala mbalimbali ya ndani ya Afrika Kusini na kutembelea baadhi ya nchi.
Hata hivyo, udhaifu wa mwili uliotokana na magonjwa na uzee ulimzidia na kumfanya apunguze safari za nje. Kwa mara ya mwisho alionekana katika shughuli za hadhara katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambayo yalifanyika Nchini Afrika Kusini.
Mandela na Tanzania
Tanzania kama nchi imehusika kwa kiasi kikubwa kuvunjavunja utawala wa kikaburu na katika kuongoza harakati za kutaka Mandela aachiliwe huru. Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere na utawala wake baada ya Uhuru 1961 aliazimia kutoa msaada unaohitajika kwa wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, ikiwamo Afrika Kusini.
Kama ilivyodokezwa hapo juu kuwa mojawapo ya mashtaka dhidi ya Mandela ni lile la kwenda nje ya nchi bila kibali. Mwaka 1962 Mandela akitumia njia za panya, ambapo alitoroka Afrika Kusini na hatimaye kuingia Tanganyika na kukutana na Mwalimu Nyerere ambaye aliwapa ahadi ya ushirikiano mkubwa. Mandela alipokewa na Mzee Mwakangale kule Mbeya, ambaye alimsafirisha hadi Dar es Salaam kwa Nyerere.
Mandela mwenyewe akizungumza katika dhifa aliyomwandaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, mwaka 1997 Oktoba 17; alisema “Inanyenyekesha kukumbuka mchango wa Mwalimu Nyerere katika ukombozi wa bara letu na Uhuru wa Afrika Kusini.”
Aliendelea kumsifia Nyerere kwa kusema kuwa wakati watu wengine walikuja baadaye kuona ubaya wa utawala wa kikaburu, Nyerere aliliona hili mwaka 1959 ambapo akishirikiana na Fr. Huddleston walianzisha harakati za kupinga ubaguzi wa rangi (anti-apartheid movement), ambao zilikuwa maarufu baadaye – hasa baada ya kesi ya Rivonia.
Mandela alisema kukutana na Mwalimu mwaka 1962 kulimwonesha jinsi Nyerere alivyokuwa anataka haki sehemu zote duniani na jinsi alivyojitoa yeye na taifa lake changa kuona kuwa Afrika yote inakuwa huru.
Katika kuonesha hili Mandela alichagua Tanzania miongoni mwa nchi za kwanza kutembelea baada ya kuachiliwa huru mwaka 1990. Aliingia nchini Tanzania Machi 7, 1990 na kupokewa na maelfu ya watu wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Wakati anatembelea nchini kama mtu huru, Tanzania ilikuwa na wapiganaji karibu 10,000 wa Afrika Kusini waliokuwa wanaishi Tanzania na kujihusisha na mambo mbalimbali.
Yote haya yalisaidia kuifanya Tanzania kuwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Nchi Zilizo Mstari wa Mbele ambayo kwa muda mrefu iliongozwa na Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Uhusiano huu wa karibu wa Tanzania na wapigania uhuru ulithibitika zaidi baada ya Tanzania kuwapatia wapigania uhuru hao maeneo ya mafunzo ya kijeshi na taaluma mbalimbali huko Morogoro eneo la Mazimbu na maeneo mengine Mtwara na sehemu nyingine nchini.
Pamoja na vyuo, wapigania uhuru hao walipewa maeneo ya shule za msingi na sekondari vile vile kwa ajili ya kujifunza kusoma na kuandika.