Na James Mwanamyoto (OR-TAMISEMI)
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 331 kupitia mradi wa BOOST zilizojenga madarasa yatakayotatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika shule ya Msingi ya Mambamba ‘B’ Wilayani Tandahimba.
Ndejembi amesema hayo akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, mara baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kumpatia fursa ya kuzungumza na wakazi wa eneo hilo.
Ndejembi amefafanua kuwa, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitafuta zaidi ya bilioni 230 kwa ajili ya kujenga shule mpya na madarasa nchi nzima kupitia Mradi wa BOOST kwenye maeneo ambayo shule zina msongamano wa wanafunzi au hakuna shule, ambapo Tandahimba imenufaika na ujenzi wa shule ya Msingi ya Mambamba ‘B’ iliyogharimu milioni 331.
“ Waziri Mkuu milioni 331 imejenga madarasa haya mazuri yenye kupendeza katika Shule hii ya Msingi ya Mambamba ‘B’ ambayo yatasaidia kutatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi uliopo katika shule mama ya Mambamba, ikiwa ni pamoja na kuwaondolea hadha wanafunzi kutembea umbali mrefu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imepokea milioni 95 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa shule ya msingi na milioni 95 nyingine kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa shule za sekondari.
Aidha, Ndejembi amesema TARURA imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati barabara ya Kilomita 7.2 ya kutoka Mambamba kwenda Mwimbi hadi Tandahimba ili iweze kupitika katika majira yote.
.
.