Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa
sekta mbalimbali nchini.
Masuala mengi yalizungumzwa na wafanyabiashara wenyewe, tofauti na ilivyozoeleka ambako
kazi hiyo ilifanywa kwa uwakilishi. Waliopata nafasi walizungumza matatizo yanayowakabili na
wakatoa mapendekezo ya kutatua kero mbalimbali.
Tunampongeza Rais Magufuli na Serikali kwa jumla, kwa kuwa wasikivu. Hata hivyo, mkutano
huo unaweza usiwe na tija endapo yale yaliyozungumzwa hayatatafutiwa ufumbuzi haraka.
Tunatambua na kuheshimu dhima ya wafanyabiashara katia ujenzi wa uchumi wa Taifa letu, na
ndiyo maana mara zote tumeunga mkono utaratibu wa kuwakutanisha na watunga sera na
sharia, ili kwa pamoja waweze kupata majawabu ya kuwawezesha kusonga mbele.
Kwa upande wa vyombo vya habari, tunasikitika kuwa hatukupata uwakilishi, lakini sekta hii
inakabiliwa pia na matatizo makubwa. Baadhi ya matatizo hayo ni wingi wa kodi kwenye
karatasi na vifaa vya uchapishaji, gharama kwenye vifaa vya kielektroniki na kupungua kwa
kiwango kikubwa mno kwa ununuzi wa magazeti.
Sekta ya habari ina mchango mkubwa mno katika ujenzi wa uchumi wa taifa lolote. Habari
ndiyo kiunganishi cha serikali na wadau wengine wote wa maendeleo. Matarajio yetu ni kuwa
viongozi wakuu watakuwa na siku maalumu ya kuzungumza na wadau wa habari ili kuyapatia
ufumbuzi masuala yanayowakwamisha.
Mazungumzo ya Rais Magufuli na wafanyabiashara, yaligusa sehemu nyingi. Miongoni mwa
maeneo yaliyotia fora kulalamikiwa ni la wingi wa kodi na urasimu kwa mambo mbalimbali.
Ilitolewa mifano ya utitiri wa kodi kwenye utalii na viwanda. Kuna malalamiko ya ukubwa wa
kodi na ushuru mbalimbali. Yote haya tunaamini yatapatiwa ufumbuzi ili kuwafanya walipa kodi
wawe wepesi na wafurahie kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
Mwisho, tunampongeza Rais Magufuli, kwa dhamira yake ya kulinda viwanda vya ndani.
Tulishanusa mpango haramu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na mawakala wao
kuhakikisha ushuru kwenye mafuta ya mawese kutoka ughaibuni unaondolewa. Rais
ametangaza msimamo mzuri wenye kuleta tija kwa wakulima wa alizeti na mbegu nyingine.
Hatua hiyo itakomboa maelfu ya wakulima walioitikia mwito wa kuzalisha mazao kwa wingi.
Tunamshauri Rais Magufuli na wasaidizi wake wadumishe utaratibu wa kukutana na wadau wa
sekta mbalimbali ili kuvitambua na kuvindoa vikwazo vinavyokwamisha ustawi wa uzalishaji
nchini mwetu. Mkutano huu umeleta faraja na kuwapa matumaini mema wawekezaji na
wakulima.