1-3Hatua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya kuwafikisha wabunge wanne mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mikopo waliyochukua wabunge kutoka benki mbalimbali nchini imegeuka mwiba kwao.

Taarifa za benki mbalimbali na ofisi za Bunge, zinaeleza kuwa wabunge walipofika Dodoma mwaka jana mara tu baada ya kuchaguliwa, walipata ushawishi kutoka kwa mawakala wa benki waliojikita katika viwanja vya Bunge wakaishia kuchukua mikopo inayozidi pato lao la mwezi.

Wabunge wengi wamechukua mikopo mikubwa kutoka benki za biashara nchini, na mikopo hiyo sasa imegeuka adhabu kwa wabunge hao.

Taarifa za uhakika zinaonesha wapo wabunge ambao wamekopa milioni 500 hadi bilioni moja, hali inayowafanya kukatwa fedha zote zinazoingizwa katika akaunti zao za benki.

“Hivi tunavyoongea kuna wabunge kila wakiingiziwa fedha kwenye akaunti zao zinakatwa zote hawapati kitu. Hawana pesa. Pesa zote zinakwenda kulipa madeni yao makubwa waliyoyachukua.

“Sasa wanahaha kutafuta njia mbadala  za kujiongezea kipato, maana hali ni mbaya,” anasema mtoa taarifa.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa katika kupambana na makato hayo makubwa ya posho na mishahara, wabunge wanaunda mkakati wa kuishauri Ofisi ya Bunge kuanza kutumia akaunti mbili tofauti.

Wabunge tayari wamewasiliana na ofisi za Bunge waruhusiwe kutoa akaunti zaidi ya moja na malipo yao yaingizwe katika akaunti hizo kudhibiti makato yanayofanywa na benki.

“Kimsingi wanachotaka kufanya sasa watazalisha tatizo kubwa kuliko walilolitengeneza. Wakiwa na akaunti mbili wakakwepa wajibu wa kulipa mikopo yao huu utakuwa utapeli na wataishia mahakamani vile vile,” anasema mtoa habari.

 

Ndugai alonga

 

Akizungumza na JAMHURI, Spika wa Bunge Job Ndugai, anasema suala la kukopa ni la mtu binafsi ambalo ofisi yake haiwezi kuingilia.

Ndugai anasema ni kawaida Bunge linapozinduliwa  mkoani Dodoma benki zinaweka kambi bungeni kwa ajili ya kutoa huduma kwa wabunge ikiwa ni pamoja na kupata wateja wapya, hivyo suala la kuwakopesha si jipya na anaamini kila aliyekopa ana uwezo wa kumudu mkopo wake kutokana na masharti ya mkopo aliochukua.

Suala la wabunge kutaka kutumia akaunti zaidi ya moja anasema yeye amesikia kitu kama hicho, lakini hawezi kulizungumzia maana bado halijafika mezani kwake.

“Zipo taratibu. Ni lazima zifuatwe, hivyo ni vyema ukanipa muda, pia nishirikiane na uongozi kuona kama inawezekana au la, ndipo naweza kulitolea ufafanuzi,” anasema Spika Ndugai.

 

Wabunge wanne kizimbani

 

Wiki iliyopita wabunge wanne walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kuomba rushwa kutoka katika mashirika wanayoyasimamia.

 Machi 31, Takukuru iliwapandisha kizimbani wabunge watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 30.

Wabunge waliopandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Maghela Ndimbo, ni Mbunge wa Mvomero, Ahmed Saddiq Murad (53), Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54) na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Ndimbo alisema washtakiwa walitenda kosa hilo Machi 15, mwaka huu kati ya saa mbili na saa nne usiku katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Masaki, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alisema washtakiwa wakiwa kama wajumbe wa Kamati ya Bunge ya LAAC, waliomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Mbwana Magotta.

Wabunge hao waliomba rushwa hiyo watoe upendeleo chanya kuhusiana na taarifa ya fedha ya wilaya hiyo ya mwaka wa fedha 2015/16.

Baada ya kusomewa, washtakiwa walikana, ambapo upande wa Jamhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo waliomba tarehe nyingine ya kutajwa kesi.

Hakimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuwapa washtakiwa masharti ya dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano.

Wabunge hao walitimiza masharti ya dhamana wakaachiwa huru, kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 14, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Aprili mosi, Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56), alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili ya kuomba rushwa ya milion 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanesco (Tanesco), Felchesmi Mramba.

Ndassa anadaiwa pia kumshinikiza Mramba kuwafungia umeme ndugu na rafiki zake. Akisomewa mashtaka hayo na wakili wa Serikali, Denis Lekayo, aliyedai mbele ya Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 13, mwaka huu Dar es Salaam kinyume cha kifungu cha 15(2) Sheria ya Takukuru.

Katika shtaka la kwanza, alisema siku ya tukio, Ndassa kwa nafasi yake ndani ya PIC, aliomba rushwa ya Sh 30 milioni kutoka kwa Mramba ili kamati hiyo iweze kutoa ripoti ‘nzuri’ya hesabu za mwaka 2015/2016 kwa shirika hilo.

Katika shtaka la pili, alisema Ndassa alimshinikiza Mramba kumpatia umeme ndugu yake aliyetajwa kwa jina la Matanga Mbushi na rafiki yake Lameck Mahewa. Mshtakiwa alikana mashtaka na wakili wa Serikali alieleza kuwa upelelezi unaendelea.

Wakili huyo alisema dhamana iko wazi ila aliiomba Mahakama iweke masharti magumu asiweze kuingilia uchunguzi unaoendelea kufanywa. Hata hivyo, Wakili Erasto Mgenge anayemtetea Ndassa aliiomba Mahakama itoe dhamana isiyo na mashari magumu kwa sababu ni haki yake.

Hakimu Mchauru alimtaka Ndassa kujidhamini mwenyewe na kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10, masharti ambayo aliyatimiza na kuachiwa huru kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 18 itakapotajwa tena.   

 

CCM yang’aka

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa tamko kwa wabunge wake kuwa hakitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Christopher ole Sendeka, kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki ilisemachama hicho kimesikitishwa na tuhuma za rushwa hasa zinapowahusu wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.

“CCM inaunga mkono jitihada za vyombo vya dola katika kutafuta ukweli wa tuhuma hizo. Lazima ifahamike vitendo vya rushwa havikubaliki kwa namna yoyote kwani vina madhara makubwa kwa Taifa.

“CCM inavishauri vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua stahiki wabunge wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya rushwa,” inasema taarifa hiyo.

 

Wabunge wengine kushitakiwa

 Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI na kuanza kuchapishwa wiki iliyopita, unaonesha kuwa kuna orodha ndefu ya wabunge wanaochunguzwa ambao wengi wanaweza kuishia mahakamani kama gazeti hili lilivyochapisha wiki iliyopita.

Gazeti hili lilichapisha habari za baadhi ya wabunge kuomba hadi Sh milioni 100 kutoka mashirika na taasisi za umma, huku wengine wakiomba wabadilishiwe chai na chakula kuwa posho.

Gazeti hili lilisema kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya wabunge, watakaobainika wanaweza kufikishwa mahakamani na adhabu ya rushwa kwa mbunge ni faini Sh 20,000 au kifungo jela miaka 3 au vyote viwili.

Hata hivyo, chini ya ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbunge akifungwa jela kwa zaidi ya miezi 6 anapoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge, suala ambalo wengi wanaamini hii ndiyo hatari kubwa inayowakabili wabunge wanaoendekeza rushwa.

 

Tetesi za kuomba rushwa

Kashfa ya wabunge kuomba na kupokea rushwa kutoka katika taasisi na mashirika wanayoyasimamia zimekuwa zikisikika mara kwa mara.

Hivi karibuni wabunge waliingia kwenye mvutano na Ofisi ya Bunge kuhusu fedha ambazo wanastahili kupewa kwa ajili ya ununuzi wa magari yao.

Mwaka 2010 wabunge walilipwa kiasi cha Sh milioni 90 kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser (Hardtop), ambayo ni vitendea kazi vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo huku nusu yake ikilipwa na Serikali.

Wakati Serikali ikipambana kubana matumizi na kuboresha maisha ya Watanzania, wabunge walikataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala yake wametaka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

 Wabunge wanataka walipwe Sh  milioni 130 ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya kupanda bei. Hata hivyo, ombi hilo limegonga mwamba.

Baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la 11, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alifanya kikao na wabunge wote kuwapa taratibu, lakini pia kuwafahamisha stahiki wanazopaswa kupata kama wabunge.

 Suala hilo liliibua mjadala na kuchangia wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la 11, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho hicho.

Kutokana na kupata fedha kidogo na kuchukua mikopo mikubwa wakawekeza katika miradi wasiyo na uzoefu nayo, wabunge wengi wameishiwa fedha kiasi cha kutotamani kufika majimboni kwao.

Hatua hii inaelezwa kuwa ndiyo inayowasukuma kulazimisha kupata fedha za ziada kwa nia ya kufukia mashimo pale walipopungukiwa.