Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imekwisha kutoa awamu mbili za mikopo kwa baadhi ya wanafunzi walioomba.

Mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 Sh bilioni 450 zimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza na wanaoendelea.

Pamoja na juhudi kubwa za serikali katika kuhakikisha wanaostahili mikopo hii wanapata na kuanza masomo, hali bado si nzuri kwa baadhi ya waombaji. Hadi mwishoni mwa wiki, maelfu ya wanafunzi walikuwa hawajapata mikopo hiyo.

Hali hiyo imezua taharuki na simanzi miongoni mwao, hasa kwa wale wanaotoka kwenye familia maskini.

Pamoja na kupongeza kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Bodi ya Mikopo, bado tunaona kuna umuhimu wa kuhakikisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi unafanywa kwa kasi na weledi ili kutenda haki.

Tunao ushahidi wa baadhi ya watoto wanaotoka kwenye familia duni ambao hadi leo wanahangaika kupata mikopo. Tunashauri upembuzi wa waombaji uwe unafanywa mapema na kwa umakini ili kuondoa kero hizi.

Mkopo ni mkopo, na tafsiri ya mkopo ni kwamba anayekopa hutakiwa alipe mkopo huo. Kwa maana hiyo mkopo si zawadi wala si hisani. Mkopo ni haki ya kila mwanafunzi mwenye sifa kwa sababu unatolewa kisheria.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, alieleza kwa uchungu mkubwa shida wanazopata wanafunzi wa elimu ya juu pindi wanapohitaji mikopo.

Aliahidi kufanya kila analoweza ili kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi mwenye sifa anapata mkopo bila mizengwe. Kweli, muda mfupi baada ya kuingia madarakani alihakikisha anafanya mapinduzi makubwa yakiwamo mabadiliko ya kimfumo na kiuongozi kwenye Bodi ya Mikopo.

Hakuishia hapo, alikwenda mbali kwa kuhakikisha fedha za mikopo zinaongezeka hadi Sh bilioni 450 kwa mwaka 2019/2020. Fedha hizi ni nyingi, na kwa kweli kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa taifa linaonja mafanikio ya juhudi hizi.

Pamoja na lawama zinazoelekezwa HESLB, upande mwingine wenye kasoro ni wa wanafunzi wanaoomba mikopo. Mara kadhaa imebainika kuwa taarifa za baadhi yao huwa, ama zinakosewa wakati wa kujaza fomu za maoni, au zinaghushiwa. Kasoro hizo zimesababisha wengi wakose mikopo.

Tunaomba pande zote zinazohusika kwenye mikopo hii kuketi na kuangalia namna ya kuondoa dosari hizo ili azima njema ya serikali kuwakopesha wanafunzi iweze kutimia.