Mikoa ya Katavi, Shinyanga na Tabora inaongoza nchini kwa kuwa nyuma katika kuwapatia chanjo watoto wenye umri chini ya miaka miwili.

Akizungumzia hali hiyo hivi karibuni mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Health Promotion Tanzania, Peter Bujari, amesema Mkoa wa Katavi umekuwa na kiwango cha asilimia 54.1 kwa watoto waliopata chanjo ya kinga; Shinyanga asilimia 55.5 na Tabora ikiwa na asilimia 58.9.

Lakini wakati mikoa hiyo ikiwa nyuma katika utoaji wa chanjo, mikoa iliyo mbele ni pamoja na Kilimanjaro unaoongoza kwa kutoa chanjo kwa watoto kwa asilimia 93, ukifuatiwa na Kagera asilimia 88, Njombe (87%), Dar es Salaam (86%) na Iringa (84%).

Kutokana na hali hiyo, mkurugenzi mtendaji huyo wa taasisi hiyo ya Health Promotion Tanzania inayojihusisha na maendeleo ya sekta ya afya nchini amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kupitia mkakati mahususi wa afya kwa wote, mkakati unaolenga kuhakikisha wote wanafikiwa na huduma husika za afya.

Amesema uzoefu unaonyesha kuwa moja ya vikwazo vikubwa kwa wananchi kupata huduma za afya ni pamoja na uwezo duni wa kiuchumi.

“Mara nyingi uwezo duni wa kiuchumi umekuwa kikwazo kwa watu wengi kupata huduma za afya, ikizingatiwa kuwa huduma ya bima ya afya haijawafikia wengi. Sasa mtu anaumwa, haendi hospitali leo kwa sababu hana pesa, anasubiri siku nyingine atakapopata pesa,” amesema na kufafanua kuwa, hata huduma za utoaji chanjo kwa ajili ya kinga kwa watoto wadogo huchangiwa na mtandao duni wa huduma za afya katika baadhi ya mikoa.

Amesema Health Promotion Tanzania imefanya juhudi mbalimbali ambazo ni pamoja na kukutana na wabunge wa maeneo ambayo takwimu zinabainisha utoaji chanjo umekuwa wa kiwango kisichoridhisha.

“Tumekutana na wabunge wa maeneo hayo ambako hali si nzuri, tumewaeleza umuhimu wa jambo hilo na wameonyesha utayari wa kuhamasisha jamii kuwapa chanjo watoto ili hatimaye jamii nzima iweze kulindwa.

“Unapokuwa na jamii ambayo sehemu kubwa imepata chanjo maana yake ni kwamba jamii hiyo imelindwa dhidi ya magonjwa, lakini inapotokea sehemu ndogo ya jamii hiyo ndiyo iliyopewa chanjo, ni dhahiri jamii hiyo kwa sehemu kubwa itakuwa haijakingwa,” amesema na kuongeza kuwa mkakati mahususi wa ‘afya kwa wote’ utalenga kuwafikia watoto 331,150 wenye umri chini ya miaka miwili.

“Inakadiriwa kuwa watoto 113,330 katika mikoa ya Katavi, Tabora na Shinyanga hawapati huduma ya chanjo kila mwaka,” ameeleza Bujari.

Ameeleza kwamba kumekuwa na tofauti ya asilimia 10 katika utoaji wa chanjo kati ya maeneo ya mijini na vijijini, na kwa hali hiyo, hakuna namna isipokuwa kutekeleza mkakati huo mahususi wa ‘afya kwa wote’ ili kuimarisha viwango vya utoaji chanjo maeneo yote, ikiwa ni pamoja na kuondoa tofauti hiyo ya asilimia 10 inayofanya maeneo ya mijini kuwa mbele ya vijijini.

Uchambuzi wa kitakwimu uliofanywa na Health Promotion Tanzania unabainisha kuwa nchini Tanzania, watu zaidi ya sita kati ya 10 hawana huduma ya bima ya afya.

Inaelezwa kuwa ni asilimia 33 tu ndiyo wenye huduma ya bima ya afya.