Na Baraka Jamali, JamburiMedia, Mtwara
Mikataba ya biashara na kodi kati ya nchi moja na nyingine inachukua nafasi muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
Kimsingi, mikataba hiyo ina lengo la kupunguza mzigo wa kodi kwa wawekezaji wa kigeni na kuhamasisha uwekezeji.
Kama nchi tumeingia mikataba na Canada (mwaka 1995), Denmark (mwaka 1976) na India (mwaka 1979).
Mikataba hiyo ni mifano halisi ya jinsi inavyosaidia kuimarisha rasilimali za ndani kupitia uhamasishaji wa uwekezaji na imeundwa ili kuzuia upotevu wa mapato na kuboresha mazingira huku ikiondoa tatizo la ushuru mara mbili kwa wawekezaji.
Mathalani, mwekezaji wa Canada anayewekeza Tanzania katika sekta za madini, kilimo na nishati anapata uhakika wa kulipa kodi moja pekee lakini si kwa pamoja.
Mei 24, mwaka huu alipofunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Uganda, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, anasema: Sote ni mashahidi kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuendelea kutekeleza agenda ya uchumi wa viwanda kwa kuwavuta wawekezaji kutoka nje na kuheshimu makubaliano na mikataba tuliyojiwekea.
Pamoja na mambo mengine, hatua hiyo inafanya wawekezaji waone wako salama zaidi na wanawekeza kwa kutoa uhakika wa kodi.
Takwimu zinaonyesha nchi zilizo na mikataba ya kodi ya kibiashara ya nchi mbili zinaweza kuvutia uwekezaji wa kigeni moja kwa moja kwa asilimia 30 na zaidi ikilinganishwa na nchi zisizo na mikataba kama hiyo.
Ukiangalia mikataba ya kikodi ya Tanzania na nchi mbalimbali ikiwamo Canada (Canada – Tanzania Income and Capital Tax Treaty-1995) ni kwamba inaazimia kuzuia ushuru mara mbili na kuweka viwango vya kodi kwa mapato na mtaji.
Uanzishwaji wa mkataba huu umesaidia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuongeza uwekezaji wa nchi hiyo na Tanzania hasa katika sekta za madini na nishati.
Mkataba huo unahakikisha raia wa Canada na Tanzania hawalipi ushuru mara mbili kwa mapato wanayopata katika nchi hizo.
Mkataba huo unasema: Kuwe na urekebishwaji viwango vya ushuru kwa aina mbalimbali za mapato, kama vile mapato ya faida, gawio na riba. Hii inatoa uwazi zaidi kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
“Katika kupunguza vikwazo vya ushuru, mkataba huu unaleta mazingira mazuri kwa wawekezaji wa Canada kuwekeza Tanzania na kinyume chake, hivyo kuchangia ukuaji wa kiuchumi.”
Mkataba huo unahamasisha ushirikiano kati ya mamlaka za nchi hizi na kusaidia kukabiliana na udanganyifu wa kifedha na kuhakikisha ushuru unakusanywa ipasavyo.
Ingawa mkataba unalenga kutoa mwongozo, bado kuna changamoto katika kutafsiri na kutekeleza masharti yake yanayoweza kuathiri wakandarasi na wafanyabiashara.
Mkataba mwingine ni ule wa ‘Denmark – Tanzania Income and Capital Tax Treaty (1976). Huu umesaidia kuboresha mazingira ya biashara kwa wawekezaji wa Denmark.
Serikali ya Denmark imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi na kifedha kwa Tanzania na kuwezesha miradi mingi ya maendeleo.
Sambamba na kuwa na faida chanya ila umekuwa na athari kadhaa kwa Tanzania.
Mathalani unaruhusu kampuni za Denmark kupata faida bila kulipa ushuru mkubwa hapa nchini na hatua hii inaweza kusababisha upungufu wa mapato ya serikali hasa katika sekta muhimu kama madini na kilimo.
Kwa kuwa baadhi ya wawekezaji wa kigeni wanapata manufaa zaidi kupitia mkataba huo, Tanzania inaweza kujiweka katika hali ya kuongeza ushuru kwa raia wake ili kufidia mapato yaliyopotea.
Julai 30, mwaka jana, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anasema ushirikiano na wawekezaji wa kigeni umesababisha hasara kubwa kutokana na serikali kutokuwa makini wakati wa makubaliano.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kabindi wilayani Biharamulo anasema na kuongeza: Mikataba mingi iliyoingiwa na serikali kipindi cha nyuma imelitia hasara taifa kutokana na kutokuwa makini na kufanya wageni kutajirika na rasilimali na wamekuwa kama tuna utaratibu wa kuvunja mikataba holela na kusababisha kupigwa faini.
Niliwahi kuzungumza bungeni mwaka 2017 nikiwa mbunge kuhusu hii mikataba na mataifa ya kigeni kuwa haina faida kwa nchi yetu bali itachangia hasara kubwa lakini niliishia kushambuliwa kwa maneno. Tangu nimezungumza hadi sasa tumelipishwa faini ya Dola 339,000,000 za Marekani kutokana na kutofuata sheria ya mikataba.
Katika hatua nyingine, utafiti wa jinsi rasilimali zinavyofaidisha nchi na mikataba tunayoingia uliofanywa mwaka 2016 na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Rosemary Mukama, unasema: Mwalimu Nyerere alionyesha umuhimu wa kuhakikisha kwamba mikataba inafaidisha pande zote, haswa nchi zinazoendelea kama Tanzania. Akasisitiza kampuni za kigeni zinapaswa kuchangia kwa usawa katika maendeleo ya nchi.”
Vilevile mkataba mwingine wa India – Tanzania Income Tax Treaty (1979) umeshuhudia ongezeko la biashara na uwekezaji.
India imewekeza katika sekta za kilimo, afya, na teknolojia na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania.
Kampuni za India zinaweza kutumia mikakati ya kisheria kuepuka kulipa ushuru wa juu na kuathiri mapato ya serikali ya Tanzania.
Ripoti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya mwaka 2021 kuhusu mikataba ya kodi inasisitiza umuhimu wa mikataba ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili katika kuhamasisha rasilimali za ndani.
Ripoti hiyo inasema: Ushirikiano kati ya mamlaka za ushuru za nchi husika ni muhimu katika kuboresha ukusanyaji wa ushuru na kufuatilia upatikanaji wa fedha za kigeni.”
Pia mikataba hiyo inaweza kusaidia biashara za ndani kwa kutoa fursa za kuungana na kampuni za kigeni na kuongeza ushindani na ufanisi.
Uwekezaji wa kigeni unapoingia nchini, huleta ajira mpya. Hiyo inasaidia kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira na kuboresha kipato cha kaya
Unaweza pia kusaidia kuimarisha ujasiriamali wa ndani. Kwa mfano, kampuni za kigeni zinaposhirikiana na wajasiriamali wa ndani, zinaweza kusaidia kuboresha ubora wa bidhaa na huduma na kuongeza ushindani wa soko.
Uwekezaji wa kigeni mara nyingi unahusisha ujenzi wa miundombinu kama vile barabara na reli. Hii inaongeza uwezo wa nchi kutoa huduma bora za kijamii kwa raia wake.
Makubaliano hayo ya kibiashara kati ya Tanzania, Canada, Denmark na India yana jukumu muhimu la kuboresha makusanyo na rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2020 kuhusu uwekezaji barani Afrika inasema: Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi kutokana na mikataba ya kibiashara ya kikodi pia ni njia mojawapo ya kuimarisha ushirikiano na kutoa faida kwa pande zote.
MWISHO