Jeshi la polisi nchini Kenya limesema kuwa miili ya wanawake 8 iliyokuwa kwenye dampo katika eneo moja la makazi duni imepatikana jijini Nairobi.
Jeshi hilo limeongeza kuwa kwa sasa linachunguza ili kupata uhusiano kati ya tukio hilo na masuala ya imani za kidini, wahalifu wanaofanya mauaji ya kupanga au watoa huduma za afya kinyume cha sheria.
Katika tukio hilo la kutisha, miili ya wanawake hao ilipatikana ikiwa imekatwa katwa na kufungwa kwenye mifuko ya plastiki kwenye sehemu iliyojaa takataka eneo la Mukuru, kusini mwa mji mkuu wa Nairobi.
Kaimu Mkuu wa jeshi la polisi la Kenya Douglas Kanja amesema kuwa miili sita ya kwanza ilipatikana Ijumaa, na miili mingine ilipatikana jana Jumamosi. Kanja ametoa wito kwa wananchi kuonesha ushirikiano ili kufanikisha kuwapata wahusika wa unyama huo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.