Hatimaye Mashindano ya Ligi Kuu ya Vodaco Tanzania Bara yamemalizika huku Klabu ya Simba ikiambulia kushika nafasi ya tatu, huku mtani wao wa jadi, Yanga ikitwaa ubingwa wa ligi hiyo, ikifuatiwa Azam FC iliyoshika nafasi ya pili.

Klabu ya Simba iliyokuwa mtetezi wa ubingwa wa ligi hiyo, ilianza vizuri katika mashindando hayo lakini baadaye ilianza kunyong’onyea kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele.

 

Hadi mashindano hayo yanahitimishwa Jumamosi iliyopita, Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mtani wake wa jadi, Yanga katika mtanange uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

 

Wachezaji, viongozi, wapenzi na mashabiki wa Simba waliondoka uwanjani wakiwa wamenyong’onyea, baadhi wakiwa midomo wazi, wakiwa wamejitwisha mikono vichwani na wengine wakiwa wameinamisha vichwa chini na kushika viuno kwa kutoamini kilichotokea.

 

Ilikuwa ni Jumamosi ya shangwe, nderemo, vifijo na vigelegele kwa Yanga, na wakati huo huo, siku ya huzuni, masikitiko na hata vilio kwa Simba. Mambo ya mpira wa miguu hayo, ni dakika 90.

 

Wachambuzi na wadadisi wa masuala ya soka wanasema matatizo yaliyosababisha Simba kupoteza uelekeo sahihi katika Mashindano ya Ligi Kuu ya Vadacom Tanzania Bara mwaka huu yanaweza yakajirudia msimu ujao ikiwa viongozi husika hawatachukua hatua madhubuti kuyakabili mapema.

Simba ilianza kupepesuka mapema katika michuano hiyo baada ya kukumbwa na migogoro mbalimbali ukiwamo wa wachezaji wake, ingawa uongozi wa timu hiyo umekuwa ukipinga ukweli huo wa mambo.

Mgogoro kati ya wachezaji wa timu hiyo ulitokana na Simba kuvunja mkataba na kocha Milovan Circovic, uliositishwa mwishoni mwa mwaka 2012.

Kocha huyo alieleza kusikitika kuwa uongozi wa Simba umefanya kosa kuharibu mipango aliyokuwa amejiwekea kuwezesha ufanisi wa timu hiyo, na matokeo yake hali iliendelea kuwa mbaya zaidi ya alivyoiacha.

 

Suala la ukata nalo linatajwa kuchangia kuyumba kwa soka la Singa, ingawa uongozi wa timu hiyo pia uliweza kukanusha madai hayo.  Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala, alisema madeni yanayoisumbua klabu hiyo yanatokana na kutolipwa na wadai wake.

 

Pia kitendo cha Simba SC kiungo wake, kumuuza Emmanuel Okwi nacho kinatajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za kuidhoofisha timu hiyo.

 

Lakini pia Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amekuwa akilalamikiwa kuwa ameshindwa kuhimili wadhifa huo, hususan katika kushughulikia matatizo ya klabu hiyo.

 

Tatizo jingine ni kusigana kwa Kocha Mkuu wa Simba, Partick Liewig na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio,’ hali inayoelezwa kukwaza kwa kiasi kikubwa morali wa wachezaji wa timu hiyo katika mashindano hayo.

 

Kuna wakati pia viongozi wa Simba waligawanyika kuhusu suala la kumrejesha kikosini beki wa timu hiyo, Amir Maftah. Baadhi ya viongozi walishinikiza beki huyo arejeshwe Simba lakini wengine walisisitiza aachwe kwanza ajifunze kutokana na kuonesha tabia ya mgomo.

 

Kwa upande mwingine, Yanga imeweza kutumia migogoro na madhaifu ya Simba kujijenga katika mashindano hayo na hivyo, kudhihirisha ubabe wake katika tasnia ya soka hapa nchini.

 

Kipigo kilichotolewa na Yanga kwa Simba Jumamosi iliyopita, kimechangia kudhoofisha matumaini ya wapenzi na mashabiki wa wekundu hao wa Msimbazi juu ya kuhuisha kiwango chake msimu ujao.

 

Matatizo yaliyoiyumbisha Simba kiasi cha kupoteza uelekeo sahihi katika mashindano ya mwaka huu, bila shaka yatatoa fundisho kwa timu nyingine zenye uelekeo wa kukaribisha migogoro isiyo na tija.

 

Yango imedhihirisha ujogoo wake kwa Simba msimu huu, lakini pia Azam FC nayo imeonesha kuwa tishio kwa watani hao wa jadi na kwamba inaweza kufanya vizuri zaidi katika msimu ujao kiasi cha kuibuka na ubingwa wa kishindo.