Migogoro ya ardhi nchini ni miongoni mwa masuala yanayolitia doa taifa huku ikisababisha chuki na uhasama kati ya jamii moja na nyingine au kati ya mtu na mtu.

Serikali iliunda kamati maalumu ya mawaziri wanane wa kisekta kutatua migogoro hiyo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, na kwa kiasi kikubwa kamati hiyo imejitahidi kutekeleza wajibu wake.

Kwa bahati mbaya thamani ya ardhi, ‘bidhaa’ isiyozalishwa, kuongezeka au kuongezwa kwa urahisi, hupanda siku hadi siku, hivyo kuchochea hamu ya umiliki wake.

Katika maeneo mengi nchini kumekuwapo ugomvi wa ardhi na aghalabu ugomvi huu hufikia hatua ya watu kuuana au wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo iliyopewa dhamana ya kusimamia masuala ya ardhi kwa niaba ya serikali, lakini wizara hii au maofisa wa wizara hii siku zote wamekuwa wakionekana kama chanzo cha migogoro ya ardhi badala ya kuwa suluhu ya migogoro hiyo.

Malalamiko yanayopelekwa wizarani hasa katika Ofisi ya Kamishna wa Ardhi huchelewa kupatiwa ufumbuzi na wakati mwingine yanapopatiwa ufumbuzi, huzusha hisia za upendeleo wa upande fulani, hasa iwapo upande mmoja una ukwasi kuliko upande mwingine.

Mfano mmojawapo ni habari tuliyoiandika katika Toleo Namba 528 la Gazeti la JAMHURI lililosambazwa Novemba 9, mwaka huu kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kijiji cha Lupunga na mwekezaji.

Mgogoro huo umetatuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha kwa kumpa haki mwekezaji huyo akidai kuwa amekuwa mmiliki halali wa shamba lenye ukubwa wa ekari 850 tangu mwaka 1983 wakati wa Nguvu Kazi.

Kwa vyovyote vile uamuzi huo hautarajiwi kupokewa kwa mikono miwili na makumi ya wananchi waliokuwa wakilitumia eneo hilo kwa shughuli zao za kiuchumi kwa miaka mingi iliyopita, hata kama mwekezaji atakuwa na nyaraka kutoka kwa Kamishna wa Ardhi.

Tunadhani kwamba ni vema kwa maofisa wanaomsaidia Kamishna wa Ardhi pamoja na Waziri wa Ardhi kutumia busara zaidi katika kufikia utatuzi wa migogoro inayohusisha mustakabali wa makumi kwa mamia ya wananchi, hasa walio maskini.

Ipo haja kwa maofisa hawa kuangalia namna stahiki ya kutoa haki kwa pande zote na kuwaacha wananchi wakiishi kwa amani na mwekezaji aliyechukua eneo la kijiji au kitongoji chao.

Lupunga ni mfano tu wa migogoro mingi inayoamuliwa ‘kisheria’ lakini inaacha manung’uniko ya muda mrefu kwa wananchi wengi, hivyo hata kuhatarisha shughuli za uwekezaji zinazokusudiwa katika eneo husika.