Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mrneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Dodoma, Zuhura Aman amesema eneo la ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataaifa cha Msalato Dodoma linakabiliwa changamoto zinazochelewesha ujenzi.

Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi mbele ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma iliyofanya ziara baada ya kufanya ziara kiwanjani hapo, Zuhura amesema mradi huo unakabiliwa na changamoto ikiwemo mifugo kuchungiwa kwenye eneo hilo, wizi wa vifaa vya ujenzi na wananchi kupita bila kujali madhara yanayoweza kuwatokea na kuhatarisha afya zao.

“Kazi zinazoendelea kwenye mradi huu wa ujenzi wa uwanja tayari hatua zimeshafanyika ikiwemo ya kuwasiliana na uongozi wa serikali ya kata za Msalato na Nzuguni na maeneo mengine yaliyozunguka uwanja ya kutoa elimu kwa wanajamii ya kuwataka wasijihusishe na vitendo hivyo,” alisema Zuhura.

Aidha, aliwahimiza wakandarasi kujenga uzio kuzunguka eneo lote la uwanja utakapokamilika ili kuimarisha ulinzi ambao utakomeshwa na vitendo hivyo vikiwamo ya kuchungia mifugo,watu kupita na wizi wa vifaa ili kazi zikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donard Mejetii akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Dodoma akiomba serikali kuhakikisha inatoa ushirikiano wa kukomesha vitendo hivyo vinavyoathiri ujenzi wa kiwanja cha ndege.

“Haiwezekani … Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya maendeleo ya kila Mtanzania, halafu wanajitokeza watu wanahujumu fedha hizo kama vile wizi uliopo hapa wa kuiba vifaa vya ujenzi uanaendelea kuwepo na serikali imekaa kimya,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma John Kayombo alisema miradi saba iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma imekamilika kwa asilimia 99 na mingine ipo kwenye hatua za mwisho.

Kayombo amesema shilingi Bilioni 600.4 zimetolewa na serikali kwa ajili ya uwekezaji wa miradi mbalimbali ndani ya halmashauri ya jiji ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya, barabara za mzunguko, vituo vya maji,afya,majengo ya vyumba vya madarasa na kiwanja cha ndege cha Msalato .

Please follow and like us:
Pin Share