Hifadhi ya Taifa ya Katavi iko hatarini kutoweka, kutokana na kuingizwa kwa maelfu ya mifugo.
Katavi ni Hafadhi ya Taifa ya tatu kwa ukubwa miongoni mwa hifadhi 16 hapa nchini. Hifadhi nyingine ni Serengeti, Ruaha, Mikumi, Milima ya Udzungwa, Milima ya Mahale, Milima ya Kitulo, Gombe, Arusha, Ziwa Manyara, Tarangire, Mlima Kilimanjaro, Mkomazi, Visiwa vya Rubondo, Saadani na Saanane.
Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Frederick Mofuru, ameiambia JAMHURI kuwa uhifadhi na ufugaji haviendi pamoja.
Anasema uingizaji mifugo hifadhini una athari mbalimbali, ikiwamo ya mifugo kuambukizwa magonjwa ya wanyamapori na hatimaye kuwapata binadamu wanapokula nyama.
“Katika Hifadhi hii tunayo changamoto kubwa sana ya mifugo kuingizwa kwenye hifadhi, tunajitahidi kufanya doria hapa kwa kutumia ndege ili kuhakikisha tunakamata mifugo. Machi mwaka huu tumekamata ng’ombe zaidi ya 4,000 waliokuwa wanachungwa katika hifadhi,” anasema Mofuru.
Takwimu zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina ng’ombe 87,928, mbuzi 44,348, na kondoo 8,712.
Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na uharibifu wa mazingira kutokana na mifugo ni Bonde la Mto Katuma ambao ni tegemeo kwa wakazi wa mkoa na Hifadhi ya Katavi ambayo wanyamapori hasa viboko na mamba hutegemea maji kutoka bonde hilo kabla ya kuingia Ziwa Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali (mstaafu) Raphael Muhuga, anasema vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo katika Hifadhi ya Katavi ni tishio kubwa kwa ustawi wa kukuza utalii mkoani humo na Taifa kwa ujumla.
Meja Jenerali Muhuga anasema uingizwaji wa mifugo unapeleka sura mbaya kwa mkoa, pia athari zake ni kubwa, si tu katika uharibifu wa mazingira bali hata mlipuko wa magonjwa katika hifadhi.
Kuhusu ujangili, Mofuru anasema tatizo hilo lipo pia katika hifadhi hiyo na kwamba linasababishwa na silaha zinazoingia nchini kupitia kambi mbili za wakimbizi za Katumba iliyoko Wilaya ya Nsimbo, na Mishamo iliyoko wilayani Mpanda. Kambi hizo zimekuwa zikipokea wakimbizi kutoka Burundi.
Serikali imetangaza kuanzishwa kwa Operesheni Taifisha Mifugo, iliyotangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, na kutiwa nguvu na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Operesheni hiyo ilipangwa kuanza Juni 15, mwaka huu katika mapori na hifadhi zote zilizovamiwa na mifugo.