Watu waliomteka Mohammed Dewji, maarufu kama Mo, walidhani hawatafahamika ila inaonekana walikosea kusuka mpango wao wa utekaji na sasa mambo yameanza kuwatumbukia nyongo, JAMHURI limefahamu.
Vyanzo vya habari kutoka Uingereza, Afrika Kusini, Marekani na hapa nchini vimeliambia JAMHURI baada ya kuchapisha habari kuwa Mo ana microchip iliyorekodi tukio la kutekwa kwake, kuwa mataifa makubwa hayataki dunia irejee katika enzi za uharamia na utekaji wa watu, hivyo wameanzisha msako wa nchi hadi nchi kupata taarfia za wahusika na baadaye watakuwa wananyakua mtekaji mmoja baada ya mwingine kimyakimya.
Baada ya wiki iliyopita JAMHURI kuchapisha taarifa nyeti kuwa Mo ana microchip iliyokuwa inarekodi nyendo na mazungumzo ya watekaji, kabrasha zaidi limeanza kufunguliwa na sasa watekaji wameanza kufahamika.
“Nimeziona diplomatic cable (taarifa za kibalozi) zilizotumwa nchini kwao siku mbili baada ya tukio la Mo kutekwa. Nchi hizi zina kila kitu. Wanayo orodha ya watekaji, tena kwa majina na sasa wameamua kuwafanyia kazi kimyakimya,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:
“Si muda mrefu kuna majina yatatajwa watu watabaki vinywa wazi. Marekani kwa mfano imechukizwa mno na tukio hili lililokuja sambamba na mauaji ya Mwandishi wa Saudia, Jamal Khashoggi. Imesema ni jukumu la msingi la Umoja wa Mataifa na nchi wanachama kulinda maisha ya binadamu bila kujali anaishi Amerika, Ulaya, Afrika au bara jingine lolote lile.
“Sasa Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Ulaya wameamua kuanza kuwawekea vikwazo kwa njia ya smart sanction (vikwazo vinavyolenga mtu) kwa watekaji na watu wanaofanya mauaji ya kinyama duniani. Moto wanaoupitia maofisa wa Saudi Arabia waliohusika na mauaji ya Khashoggi utakuwa huo huo kwa watekaji hapa nchini.
“Hapa kwetu orodha waliyonayo, wanasema wataanza kuwanyima viza za kuingia katika nchi zao, na sasa wanaorodhesha mali walizonazo nje ya nchi au mali walizo na uhusiano nazo hawa watekaji kwa nia ya kuzitaifisha na kuwafilisi. Pia wanakusanya ushahidi wa kuwapeleka kuwashtaki kwenye Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) huko The Hague.
“Kwa hiyo si muda tutaanza kuona mtu amesafiri nje ya nchi, tunasikia amekamatwa huko ughaibuni, baadaye tunawaona the Hague… hii wameona ndiyo dawa pekee,” kimeongeza chanzo chetu.
Tulichochapisha wiki iliyopita
Wiki iliyopita gazeti hili lilichapisha taarifa kuwa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini na tajiri kijana barani Afrika, Mohamed Dewji, maarufu kama Mo, limewaumbua watekaji haijapata kutokea.
Wakati wakidhani Mo hakuwa na mlinzi, na baada ya kuvua saa na kuacha simu katika eneo la Colosseum Hotel Dar es Salaam walipomtekea, hivyo wakidhani hana mawasiliano yoyote, kumbe alikuwa na kifaa maalumu kilichomo mwilini mwake kinachorekodi kila walichofanya watekaji, JAMHURI limeambiwa.
“Kwa kweli Mo alifanya uwekezaji wa maana kuwekewa ‘microchip’ mwilini mwake. Wakati anaweka kifaa hicho miaka 10 iliyopita, hakujua kuwa kitakuwa na faida kwa kiwango hiki, ila kifaa hiki kimemwokoa kwani kimerekodi mazungumzo yote na wakati mwingine kupiga picha baadhi ya maeneo alikowekwa kulingana na positioning.
“Kifaa hiki kinaingizwa sehemu yoyote ya mwili unayotaka na hakina madhara. Ni kama kitendanishi cha mimba. Kinaungwa kwenye satellite, kisha kulingana na kiasi ulicholipa, kinakuwa na uwezo wa kutuma sauti, picha, kinaeleza hali yako kiafya, joto la mwili wako, aina ya ugonjwa ulionao au kama ugonjwa umeanza na katika mazingira ya utekaji kama haya, kinakusaidia kufahamisha mitambo kilipounganishwa uko wapi na unafanyiwa tukio lipi,” kimesema chanzo chetu kutoka London na kuongeza:
“Kimsingi hapo Tanzania wapo matajiri zaidi ya 35 ninaofahamu kuwa wamefungwa kifaa hicho. Zilipoanza vurugu za ugaidi na utekaji mwanzoni mwa miaka ya 2000 matajiri wengi Afrika walianza kujilinda kidijitali na hii ni salama zaidi kuliko kulindwa hata na mtu mwenye bunduki, maana anaweza kukugeuka yeye.”
Chanzo hiki kimelieleza JAMHURI kuwa taarifa zilizorekodiwa zipo London – Uingereza, New York – Marekani na Johannesburg – Afrika Kusini katika mitambo ya kuhifadhia kumbukumbu (servers).
Mtaalamu wa mawimbi ya satellite aliyepo nchini Afrika Kusini ameliambia JAMHURI kuwa teknolojia ya microchip inatumia satellite badala ya GPS (Global Positioning System) kuepusha aliye na microchip asipoteze mawasiliano muda wote. “GPS ukiwa sehemu isiyo na internet inapotea, lakini satellite hata ukitumbukia majini inaendelea kuona,” amesema mtaalamu huyo.
Kifaa hicho ni kidogo sawa na punje ya mchele na kinaingizwa mwilini kwa kutumia bomba la sindano. Kimehifadhiwa ndani ya plastiki na kina uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu miaka milioni moja. Kifaa hiki kinachoitwa kwa kifupi RFID kinampa aliyekiweka namba ya utambuzi, kinatunza kumbukumbu zake na mawasiliano yake anayofanya kwa muda wote wa maisha yake.
Baadhi ya kampuni zinazotoa huduma hii zinampa mhusika fursa ya kuchagua watu watatu wa kupata taarifa zake iwapo litamtokea jambo lolote lisilo la kawaida, liwe la kiusalama au vinginevyo.
Teknolojia ya microchip hapa nchini imekuwa ikitumika kulinda wanyama walioko katika hatari ya kutoweka wakiwamo faru, ambao kimsingi walikuwa wanawindwa na majangili kwa kiasi cha kutisha.
JAMHURI limekwenda nyumbani kwa Mo kupata ufafanuzi wa taarifa hizi kuwa ana microchip iliyorekodi taarifa zake zote, ila walinzi wakawaambia waandishi wetu: “Tumeambiwa hakuna mwandishi anayeruhusiwa kuingia ndani.”
Hata hivyo, JAMHURI limezungumza na baba mzazi wa Mo, Gullam Dewji na kumweleza kuwa Mo anayo microchip iliyorekodi tukio lote la utekwaji wake, naye akasema: “Wewe umeambiwa na nani? Sasa utaleta matatizo. Mo hana hiyo chip,” amesema na kukata simu.
Kutoka Afrika Kusini
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka Johannesburg, Afrika Kusini, Mpho Mandla, anasema taasisi za ulinzi na usalama nchini humo bado zimeelekeza macho na masikio yake Dar es Salaam, Tanzania.
Mandla anasema taarifa za kuhusishwa kwa raia wa Afrika Kusini ziliwafikia kwa njia ya mitandao ya kijamii, huku shauku kubwa ikiwa ni kuwafahamu wahusika wa tukio la utekwaji wa Mo Dewji.
“Unajua Tanzania na Afrika Kusini ni nchi zenye historia ya udugu, Tanzania imesaidia sana wakati wa mapambano ya ubaguzi wa rangi hapa kwetu…ninyi mnabaki kuwa ndugu zetu sana kuliko mataifa mengine yanatotuzunguka.
“Tuliposikia kwamba kuna mfanyabiashara Mtanzania ametekwa, kwanza nilisikitika kwamba matendo ya utekaji sasa yamehamia Tanzania… siku chache baadaye tukasikia kupitia kwa ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi kwamba waliomteka mfanyabiashara huyo walikuwa wanaongea lugha ya Kizulu,” anasema Mandla.
Mandla ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama hasa kwenye forensic ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba baada ya kusikia kuhusu raia wa Afrika Kusini kuhusishwa na tukio hilo, alitamani kusikia majina yao pamoja na kufahamu kama wamo katika orodha ya wahalifu wanaotafutwa kimataifa.
Taaluma ya forensic aliyonayo Mandla, kimsingi inahusu kukusanya na kuchambua masuala yote yanayohusisha matukio yanayohusiana na jinai, ushahidi unaoshikika ili kupata suluhisho kuhusu mtuhumiwa wa uhalifu.
Katika hali kama hiyo wachunguzi huchunguza vitu kama damu, vimiminika, alama za vidole, hard drives, kompyuta pamoja na teknolojia kubaini namna uhalifu ulivyotendeka.
Mandla ametoa ushauri kwamba, katika dunia ya sasa ambapo uhalifu unazidi kuongezeka kwa kasi huku ukisaidiwa na teknolojia, ni vema wananchi wakachukua tahadhari zaidi kuliko kutegemea msaada wa polisi kwa asilimia 100.
“Umefika wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama barani Afrika kutoa elimu kwa wananchi wake namna ya kujilinda… maana dunia ya leo imekuwa si sehemu salama sasa. Tusisubiri majanga yatufike,” anasema Mandla.
Makachero wa Marekani wanavyofuatilia
Mtandao wa www.kenyainsights.com, umeripoti kuwa Shirika la Kijasusi la American Intelligence Group (AGI) limeamua kushirikiana na CIA kuchunguza kwa kina kadhia ya Mohammed Dewji kutekwa. Shirika hili linasema limewaona watu wenye bunduki wakiingia Colosseum Hotel Dar es Salaam na kwamba inaelekea ni mpango uliokuwa umesukwa kitambo.
Katika mtandao huo wamechapisha picha muhimu za watu wanaodhaniwa kuwa watekaji wakiwa kwenye vikao, wengine wakijifanya wanakunywa bia, wakiwa wamevalia suti na kuonekana kama wateja. Yupo mmoja aliyevaa T-shirt na jeans, vyote vya bluu, waliokuwa wanafuatilia nyendo za Mo siku chache kabla ya kutekwa kwake.
Pia ipo siku ambayo zinaonekana pikipiki tatu zimeegeshwa nje ya hoteli, huku wengine wakifuatilia mfumo wa CCTV camera. Taarifa zinaonyesha kuwa kuna watalii waliokuwapo hotelini hapo na walipiga picha kadhaa za watekaji, ambazo mtandao huo umeanza kuzisambaza.
Mashirika ya kikachero ya Marekani yanasema siku alipotekwa Mo, wameangalia video za CCTV hakuna mtumishi yeyote wa hoteli aliyekuwapo kuangalia usalama wa wateja kama inavyotakiwa, ila zinaonyesha vijana wawili wanaoonekana kwa wajihi kuwa ni watu wa mazoezi, wakiwa wanasubiria ‘kwa machale’ nje ya hoteli. Picha hiyo nayo wameichapisha.
Afafanua utata wa microchip kupiga picha
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, mmoja wa wataalamu wa Kampuni ya Microchip International, ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, amesema microchip zinatumika kwa matumizi mbalimbali kama ilivyo simu ya mkononi, huku akiwashangaa wanaoibeza teknolojia hiyo.
Amesema kifaa hicho, microchip, kinaweza kutumika kufungua milango, kupata taarifa za kiafya, kuwasha kompyuta kwa kutunza nywira (password), kuzima taa nyumbani ukiwa nje ya nyumba yako, kuwasha gari, kulipa nauli za ndege, mabasi, kutunza akaunti yako ya benki na matumizi mengine mengi kutegemeana na mhusika anahitaji nini. Teknolojia hii sasa inatumiwa na kampuni kubwa za kimataifa (multinational companies) kurahisisha utendaji na kuangalia nyendo za wafanyakazi wao.
“Anayehoji kuhusu teknolojia ya microchip kwamba haiwezi kusafirisha mawimbi, nadhani bado ana ufahamu mdogo kuhusu teknolojia ya microchip. Anawaza microchip ya mwaka 1998… leo teknolojia imekua sana na inaweza kufanya mambo makubwa kulingana na mhusika anavyotaka kuitumia.
“Nimeona maswali yako kuhusu teknolojia hiyo kutobainisha alipo Mohamed Dewji (Mo), mpaka baada ya siku tisa. Kwanza unapaswa kuelewa kwamba kunakuwa na makubaliano baina ya kampuni na mteja, jambo ambalo linabaki kuwa siri kubwa baina ya wawili hao.
“Ili uweze kutoa taarifa za mteja inabidi kuwepo na ridhaa yake… sasa huwezi kusema kwamba kwa kuwa limetokea tatizo basi unapeleka taarifa kwa yeyote awaye, hapana. Japokuwa tulikuwa tunapata signals vizuri, lakini haikuwa sahihi kuzisambaza kwa watu bila ridhaa ya mteja,” anasema mtaalamu huyo.
Amesema gharama za kuweka kifaa hicho zinatofautiana kulingana na matumizi halisi ya kifaa chenyewe, vinavyofungwa kwa wanyama walioko hatarini kutoweka na kile kinachofungwa kwa watu ambao wanahisi hatari katika maisha yao ni tofauti kubwa.
“Ndiyo maana katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara wapo matajiri wachache ambao wamemudu kufunga microchip, maana zinakuwa aghali kulingana na matumizi husika… kuna tofauti kati ya microchip ya kufungulia mlango na ile ambayo inapeleka mawimbi yake katika satellite, hili ni jambo muhimu sana kulielewa.
“Teknolojia hii ni pana sana, mtu anaweza kuifananisha na simu ya mkononi. Kuna tofauti kubwa kati ya smart phone na simu ya kitochi. Jiulize unaweza kuingia WhatsApp kwa kutumia Nokia 3310? Lakini hilo bado haliifanyi simu hiyo kutoitwa simu, hata gharama yake [Nokia 3310] na iPhone X ni tofauti kama mbingu na ardhi.
“Microchip inaanzia dola za Marekani 50 (Sh 112,500) hadi dola za Marekani 700,000 (Sh bilioni 1.57)… hivyo si sahihi kwamba teknolojia ya microchip inafanana,” anasema mtaalamu huyo.
Vyanzo vingine vimeongeza kuwa watekaji walianza kushtuka baada ya kuona Mo anawapa simu ya baba yao wawasiliane naye kuomba fedha bila kuonyesha wasiwasi mkubwa, hivyo hilo likawashitua kuwa huenda ana “ulinzi wa ziada”. Pia wameongeza kuwa watekaji walipopata habari zilizochapishwa katika mtandao wa www.kenyainsights.com, waliona taarifa zao zimekwisha kufahamika hivyo salama yao ni kumwachia huru.
Sweden, Ujerumani, Afrika Kusini watumia microchip
Nchini Sweden, ambako zimeanza kutumika mwaka 2015, matumizi ya microchip yanaongezeka mwaka hadi mwaka na sasa wanasema watu zaidi ya 30,000 wanazo microchip. Ulrika Celsing (28), ni mmoja kati ya Waswisi 3,000 walioweka microchip na anasema anatumia microchip kuingia kazini kwa kupunga mkono kwenye kifaa kilichopo mlangoni na mlango unafunguka.
“Ni ajabu kujaribu jambo jipya na kuona jinsi gani unaweza kuitumia kurahisisha maisha siku za usoni,” amesema. Microchip imegeuzwa kama begi la mkononi, ambapo sasa inaondoa kadi za kuingia kwenye vyumba vya kufanyia mazoezi, kupanda mabasi na kazi nyingine nyingi zilizokuwa zinafanywa na kadi za benki.
Shirika la Reli la Sweden tayari linao wateja 130 ambao wanalipa nauli zao kwa kutumia microchip. Wanachofanya makondakta wa treni wanawapa wahusika kifaa cha kusoma mionzi ya microchip kinakata nauli ya mhusika kutoka benki moja kwa moja.
Seven Becker aliyeanzisha Kampuni ya ‘I am Robot’ inayouza microchip nchini Ujerumani, ambaye ni muuzaji pekee wa microchip nchini Ujerumani hadi sasa, anasema tangu amefungua kampuni yake mwaka 2015 ameuza kati ya microchip 2,000 na 3,000 kwa Wajerumani, lakini anaamini wapo Wajerumani wengi wenye microchip wanaozinunua kutoka nje ya nchi hiyo.
Serikali ya Marekani mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati wa utawala wa Rais George Bush iliwekeza zaidi ya dola milioni 300 katika teknolojia hii ya microchip na inaamini zinazidi kuimarisha usalama.
Taarifa zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa matajiri wengi nchini Afrika Kusini na watoto wao wamefunga microchip kuepusha utekaji uliokuwa unafanyika kwa wingi. “Kwa sasa akitekwa mtoto au tajiri kama ana microchip inaonyesha yuko wapi na ndani ya muda mfupi wahusika wanakamatwa. Sasa watekaji wanaogopa kuteka nchini hapa,” kimesema chanzo chetu.
Wanasiasa wataka microchip
Tangu JAMHURI lichapishe taarifa za Mo kuwa na microchip mwilini, limekuwapo wimbi kubwa la wafanyabiashara, wanasiasa na hata viongozi wa dini kutaka kufahamu microchip zinapatikana wapi ili nao waziweke.
“Ninachokwambia hata kama Mo hana microchip, kwa jinsi Gazeti la JAMHURI lilivyoeleza, kwa sasa Mo ana ulinzi wa kutosha. Kila mtu anamwogopa. Anaona akimvamia taarifa zake zitakuwa hadharani. Mimi ni kiongozi wa dini sawa, lakini kama Papa analindwa na makomandoo, sasa mimi ni nani nisitamani kuweka hii microchip ikanilinda mimi, familia yangu na waumini wangu watakaopenda kuiweka.
“Nifahamishe zinakopatikana, nitachunguza na kuona kama uwezo utaruhusu, hiki ni kifaa muhimu kuwa nacho mara moja,” amesema kiongozi mwandamizi wa dini (tunahifadhi madhehebu yake).
Baada ya maombi kuwa mengi, Jamhuri limefanya mawasiliano na kampuni kadhaa zinazozalisha hizo microchip ambazo zimesema bei inaanzia dola 50 hadi dola 700,000 kulingana na mahitaji ya mteja. “Haturuhusiwi kutangaza biashara. Tupo kwenye mtandao kutoa huduma hii muhimu na mtu anayetuhitaji akiingia kwenye mtandao wetu ataona huduma tunayoitoa.
“Akipenda atawasiliana na sisi, nasi tutamshauri aina ya microchip inayomfaa kwa matumizi yake. Kama ni kurekodi sauti, kutuma signals, kupima joto la mwili au anataka iliyoboreshwa kurekodi hadi video, teknolojia haishindwi kitu, isipokuwa uwezo wake wa kulipia gharama husika. Kwa sasa hatuna malipo ya mwezi, wala mwaka baada ya kuweka microchip, ila ukitaka taarifa zetu utagharimia kidogo huduma ya posta kukutumia taarifa hizo kwa njia utakayoichagua, vinginevyo, unaingia mwenyewe kwenye kompyuta na kutoa taarifa zako,” amesema mtaalamu kutoka kampuni moja ya Marekani.
JAMHURI limebaini kwenye mtandao zipo kampuni kama ‘I am Robot’ ya nchini Ujerumani, wao wanauza maelfu ya microchip duniani kote. Wanapatikana kwa www.chip-implants.com.
JAMHURI limefanya juhudi kubwa kuwasiliana na vyombo vya dola kufahamu hatua iliyofikiwa katika kuwasaka watekaji wa Mo, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda kwani polisi wanarushiana mpira na hawataki tena kulizungumzia suala la Mo kwa sasa. Ijumaa iliyopita Mo alikwenda kuswali katika Msikiti wa Shia Ithnasheri uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuzungumza maneno machache.
Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi Jumamosi, Mo alisema wakati ametekwa hakukuwapo chochote cha kusaidia zaidi ya Mungu na akawashukuru viongozi wa dini, Watanzania, ndugu na marafiki zake kwa kumwombea wakati akiwa mateka.
“Wazazi wangu najua Mungu alikuwa amewapa mtihani mkubwa sana,” amekaririwa Mo na Gazeti la Mwananchi akisema na kuongeza:
“Naahidi kuwa nitaendelea kuwa mwanadamu mzuri, kumwabudu Mungu zaidi, kuwa msaada kwenye jamii, kushirikiana bega kwa bega na Watanzania kwa kuwasaidia maskini, yatima na mambo yanayoleta maendeleo kwa nchi yetu.”
Mo (43) anakadiriwa kuwa na utajiri wa Sh trilioni 3.5 na ndiye tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.