NA MICHAEL SARUNGI
Serikali inaandaa mikakati mahsusi ya kuhakikisha sekta ya michezo nchini inakuwa moja ya vyanzo vya ajira na mapato kwa vijana.
Akizungumza na JAMHURI baada ya kukabidhi bendera kwa Timu ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya riadha ya dunia nchini Uingereza, yatakayofanyika kuanzia Agosti 4 hadi 13, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha michezo inakuwa chanzo cha ajira nchini kuliko sekta nyingine.
Amesema katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Serikali itawekeza kwa nguvu katika sekta hiyo kuifanya kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mapato kwa wanamichezo.
Amesema historia ya mwisho ya kujivunia katika riadha ilikuwa mwaka 2006 wakati Samson Ramadhani aliposhinda medali ya dhahabu katika michezo iliyofanyika Melbourne nchini Australia, na tangu hapo riadha imeshuka kiasi cha kukatisha tamaa.
“Hebu nendeni mkaliwakilishe Taifa kwa kutuondolea aibu hii iliyodumu kwa miaka mingi kwa kuhakikisha mnarudi na medali ili tuweze kuirudisha heshima yetu iliyopotea katika riadha,” amesema Mwakyembe.
Amesema Serikali itazungumza na Watanzania wenye vituo vya kuendeleza michezo kikiwamo cha Filbert Bayi Sports Complex kuangalia namna ya kuwaandaa vijana.
Kwa upande wake, Rais wa Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, amesema mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na RT, bado zipo changamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu za pamoja kuhakikisha riadha inasonga mbele.
“Hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kupata mafanikio katika michezo bila ya uwepo wa mikono ya serikali ndani yake; tunachoomba ni ushirikiano wa hali na mali kutoka serikalini,” amesema Mtaka.
Naye Mkurugenzi wa MultiChoice, Maharage Chande, amesema kampuni yake ina dhamira endelevu ya kuinua na kuibua vipaji nchini na ndiyo maana wameamua kusaidia katika maandalizi ya timu.
“Hebu wadau wote wa michezo yote nchini tuungane kwa pamoja kuhakikisha jina la Tanzania linaanza kujulikana tena katika michezo ndani na nje ya nchi kama ilivyokuwa katika miaka ile ya 1974,” amesema Chande.
Amesema katika miaka ya 1974 Tanzania ilikuwa na jina kubwa katika michezo kuliko Kenya, Ethiopia, Uganda na nchi nyingine katika ulimwengu wa michezo, hali iliyoweza kuitangaza nchi kwa kiwango kikubwa duniani.
Amesema ni katika miaka hiyo ya 1974 huko Christchurch, New Zealand; Filbert Bayi Sanka akiwa na miaka 21 aliishangaza dunia, mbali ya kushinda Medali ya Dhahabu, lakini pia alivunja Rekodi ya Dunia ya mbio za mita 1,500 kwa muda wa 3.32.2.
Mara baada ya kukabidhiwa bendera, mmoja wa wanariadha hao, Alphonce Simbu, amesema wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanarudi na medali baada ya Tanzania kusindwa kuipata kwa zaidi ya miaka 10.
“Tunaelewa tuna deni kwa Watanzania kwani kwa mara ya mwisho Tanzania ilitwaa medali katika mashindano ya dunia mwaka 2005 yaliyofanyikia Helsinki, Finland wakati Christopher Isegwe alipotwaa medali ya fedha,” amesema Chande.
Amesema timu iko chini ya Kocha Mkuu, Zakaria Barie, na ina wachezaji wanane ambao ni Alphonce Simbu, Stephano Huche na Said Makula ambao watakimbia marathon wakati Gabrie Geay na Emmanuel Giniki watashiriki mbio za meta 5,000 huku Sara Ramadhani na Magdalena Shauri wakishiriki marathon kwa upande wa wanawake, na Failuna Abdi atashiriki meta 10,000.