Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari, amesema kati ya Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu imesajili laini za simu milioni 7.3.

Amesema hayo alipozungumza na vyombo vya habari Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TCRA (2022- 2023) na Maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano.

Amesema kuwa kutokana na usajili huo umechangia laini za simu nchini kuongezeka kutoka milioni 57.6 hadi milioni 64.1 sawa na ongezeko la asilimia 13.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema katika kipindi hicho hicho miamala ya fedha imeongezeka kutoka Sh bilioni 3.7 hadi kufikia bilioni 4.6 sawa na ongezeko la asilimia 24.

Dk Bakari ametaja mikoa mitano inayoongoza kwa idadi kubwa ya laini za simu ni Dar es Salaam ina milioni 11.8, Mwanza milioni 4.25, Arusha milioni 3.8, Mbeya milioni 3.7 na Dodoma milioni 3.4.

“Hadi Julai 2022 kulikuwa miamala 3,767,732,264 na hadi Juni imeongezeka na kufikia miamala 4,670,491,000 sawa na ongezeko la asilimia 24,” alisema. Vivyo hivyo katika kipindi hicho tozo za miamala ya fedha kupitia simu za mikononi imepungua kutoka 19,225,082,685 hadi 14,805,512,341.

Amesema kupungua kwa tozo ya miamala ya fedha kumesababishwa na kupungua kwa viwango vya tozo ya miamala ya fedha iliyoanza kutumika Oktoba mwaka jana.

Dk Bakari amesema kumekuwa na ongezeko la watumiaji wa intaneti kwa asilimia 17 katika kipindi hicho kutoka watumiaji milioni 29.2 hadi watumiaji milioni 34.04.

Amesema TCRA imeendelea kutoa leseni na kusimamia masharti ya leseni kwa watoa huduma za mawasiliano nchini hadi kufikia Juni 2023 imetoa kwa watoa huduma 1,481 na imetoa jumla ya leseni 2,415. Dk Bakari alisema TCRA imekuwa ikipanga na kusimamia rasilimali mawasiliano kwa kugawa masafa, namba, vikoa na postikodi na anuani za makazi.

Amesema upangaji na usimamizi mzuri wa rasilimali mawasiliano (masafa na namba) ndio unaowezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano pamoja na huduma za fedha mtandao. “Jitihada hizi zitawezesha wananchi wengi kupata huduma za intaneti ya kasi ambayo ni muhimu sana wakati huu tukiwa kwenye uchumi wa kidijiti.

Malengo ya serikali ni kuhakikisha kuwa kufikia 2025 serikali inataka kuona asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za intaneti zenye kasi,” amesema Dk Bakari.