Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Rushwa ni tatizo la kidunia lenye madhara makubwa kwa mtu, jamii, nchi na mataifa kwa ujumla. Rushwa imetumika kupoka haki za watu kwa kumnyanganya haki yeye aliyeistahili na kumpa yule asiyeistahili kwa sababu mwenye jukumu la kutoa haki amepokea hongo au kaahidiwa kupewa hongo ili apindishe sheria.
Ni kwa sababu ya rushwa wapo vijana wanaokosa fursa za masomo au za kupata mikopo ya kibiashara na wengine kupendelewa na kupewa fursa hizo japo hawana sifa kwa kuwa wametoa rushwa.
Rushwa imewanyima wananchi wengi hasa maskini fursa ya kupata huduma bora za kijamii kama vile majisafi na salama, elimu bora, afya, makazi au miundombinu bora ya barabara kwa fedha inayotengwa kuboresha huduma hizi kuhujumiwa na watendaji au watu wachache na kuitumia kwa maslahi binafsi.
Tumeshuhudia pia matukio ambayo vitendo vya rushwa vimetumika kuchepusha au kuvujisha mapato ya Serikali hivyo kuikosesha Serikali fedha ya kutoa au kuboresha huduma kwa umma.
Mapambano dhidi ya rushwa yametamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 9(h) ambapo Serikali na taasisi zake zimetakiwa kuhakikisha aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.
Ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Machi 19, 2021 siku ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuilinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yapo mengi ya kujivunia yaliyofanyika katika mapambano dhidi ya rushwa nchini katika kipindi hicho.
Alipohutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma, Rais Samia alieleza dhamira ya dhati ya Serikali ya kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutowaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma.
Tutaendeleza pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma, alisisitiza Rais Dkt Samia. Dhamira hii inadhihirika kwa matokeo yanayotokana na hatua zilizochukuliwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Mathalani, taarifa ya utafiti uliofanywa na Transparency International ya mwaka 2023 kuhusu Corruption Perception Index (CPI) inaonesha kuwa Tanzania imefanya vizuri na kupata alama 40 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti, ikilinganishwa na alama 38 ilizopata mwaka 2022 ambapo ilishika nafasi ya 94.
Tanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo, imeshika nafasi ya pili katika mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na nchi ya Rwanda.
Aidha, ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa hivyo kuhakikisha ustawi wa umma, Serikali imefanya maboresho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 ili iendane na mazingira ya sasa ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Muswada wa maboresho hayo ya Sheria upo katika hatua ya kuwasilishwa Bungeni. Hii ni hatua muhimu katika mapambano haya.
Pia, Serikali imeimarisha uwezo wa kiutendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuiwezesha kwa rasilimali watu, rasilimali fedha, vitendea kazi pamoja na mafunzo ya weledi kwa watumishi. Mapema mwaka huu 2024, Serikali imetoa kibali cha ajira za watumishi 350 hivyo kufanya idadi ya watumishi wapya wa TAKUKURU katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia kufikia 880.
Uimarishaji huu wa TAKUKURU umeifanya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Kutokana na uwezeshaji wa TAKUKURU uliofanywa na Serikali, kiasi cha Shilingi bilioni 201.72 imedhibitiwa na kurejeshwa Serikalini kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi wa tuhuma za rushwa pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo. Sehemu ya fedha hii imetumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo kama vile ujenzi wa vituo vya afya, manunuzi ya dawa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa shule na barabara ili kuleta ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Serikali pia imetaifisha mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.14 zikijumuisha nyumba, viwanja na magari. Aidha, miradi ya maendeleo 3,576 yenye thamani ya Shilingi trilioni 16.76 ilifuatiliwa kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa fedha hiyo inatumika kadiri ilivyokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Vilevile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, uchunguzi wa tuhuma za vitendo vya rushwa uliendelea na pale penye ushahidi na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kesi zilifunguliwa na kuendeshwa mahakamani. Jumla ya kesi 1,922 za rushwa ziliendeshwa mahakamani zikiwamo kesi 19 zilizofunguliwa katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mahakama ilitoa maamuzi katika kesi 1,303 za rushwa ambapo katika kesi 801 sawa na asilimia 61 Jamhuri ilishinda baada ya washtakiwa kupatikana na hatia ya kutenda makosa ya rushwa na kuhukumiwa kifungo jela au kulipa faini.
Serikali inayoongozwa na Rais Samia pia imeimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuipatia TAKUKURU fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi. Fedha hiyo imewezesha kuanzisha na kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za TAKUKURU za mikoa ya Kilimanjaro na Simiyu na kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za wilaya saba za Kilolo mkoani Iringa, Kongwa (Dodoma), Kiteto (Manyara), Mvomero (Mvomero), Liwale (Lindi), Nyasa (Ruvuma) na Momba (Songwe).
Vilevile, ujenzi wa jengo la Makao Makuu jijini Dodoma, majengo mawili ya mikoa ya Iringa na Shinyanga pamoja na majengo matano ya ofisi za wilaya za Nkasi (Rukwa), Nzega (Tabora), Kishapu (Shinyanga), Monduli (Arusha) na Rombo mkoani Klimanjaro unaendelea.
Serikali pia imeiwezesha TAKUKURU kwa fedha ya kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa na kuuhamasisha ushiriki katika mapambano dhidi ya adui rushwa. Hii ni sehemu ya jitihada za kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ambapo baadhi ya wadau wamehamasika na kuchangia kuzuia vitendo vya rushwa kwa kuacha kushiriki vitendo hivyo au kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa huku wengine wakipata ujasiri na kujitokeza kutoa ushahidi katika kesi za rushwa mahakamani.
Uelimishaji umma umefanyika kwa makundi mbalimbali katika jamii kuanzia vijijini hadi mijini kupitia mikutano, minada, magulio, midahalo, semina, warsha, mbio za Mwenge wa Uhuru, vipindi vya redio, vipindi vya televisheni, na machapisho mbalimbali. Pia, elimu kwa umma imetolewa kupitia maonesho ya kitaifa na kimataifa yanayofanyika kila mwaka nchini kama vile maonesho ya Wakulima (Nanenane) na Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Ili kuongeza ushiriki wa wadau katika kuzuia vitendo vya rushwa, Programu ya TAKUKURU – Rafiki ilizinduliwa 20 Disemba, 2022. Programu hii imelenga kushirikisha wadau kutatua kero katika utoaji wa huduma kwa umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo zikiachwa bila kutatuliwa zinaweza kusababisha kutokea kwa vitendo vya rushwa. Utekelezaji wa Programu hii umekuwa wenye mafanikio ambapo kero nyingi zilizoibuliwa zimetatuliwa hivyo kuzuia vitendo vya rushwa na kuboresha huduma zinazotolewa kwa umma.
Katika hatua nyingine, mwaka 2023, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 9-11, 2023. Hii ilikuwa heshima kubwa kwa Taifa na inayoashiria imani ya Mataifa mengine ya Afrika pamoja na Umoja wa Afrika kwa Tanzania katika suala la mapambano dhidi ya rushwa. Wadau mbalimbali wa mapambano haya kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwemo kutoka sekta ya umma, sekta binafsi na asasi za kiraia walishiriki maadhimisho hayo.
Akihutubia wadau hao siku ya kilele Julai 11, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia pamoja na mambo mengine aliwatahadharisha watu wanaojihusisha na rushwa kuhusu mienendo yao. “Walarushwa wanapaswa kufahamu kuwa nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na rushwa au kufuga walarushwa. Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika si salama kwa walarushwa na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya walarushwa”, alisisitiza Rais Samia.
Mheshimiwa Rais Samia hakuishia kutoa onyo hilo bali aliueleza ulimwengu mafanikio ya hatua zilizochukuliwa na Tanzania kuidhibiti rushwa, yaani kazi zilizofanyika kuzuia na kupambana na rushwa. Mathalani, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, kupitia mapambano dhidi ya rushwa Serikali iliokoa zaidi ya Shilingi bilioni 139 ya fedha ya umma. Fedha hizo ukinipa mimi sasa hivi nikifumba macho nakwambia nazipeleka kununua vifaa tiba, alisema Mhe. Dkt. Samia.
Rais Samia aliwaomba viongozi barani Afrika kushirikiana katika kupambana na vitendo vya rushwa na kusisitiza kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika ni janga la rushwa ambalo linadhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango na mikakati ya kujikomboa kiuchumi. Pia, alitumia jukwaa la maadhimisho hayo, pamoja na mambo mengine, kumtaka kila Mtanzania kujitathmini ni kwa namna gani anadhibiti rushwa huku akiirejea kaulimbiu ya TAKUKURU.
‘‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu ; Tutimize Wajibu Wetu. Ni kaulimbiu nzito na kaulimbiu inayotupa mtihani hasa sisi Watanzania, tujitizame sisi wenyewe mmojammoja, tunaendana na kaulimbiu hii ? alihoji Rais Samia.
”Nitasimama imara kwenye mapambano dhidi ya rushwa” hii ni ahadi aliyoitoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati anapokea taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Machi 28, 2021 katika Ikulu ya Chamwino ikiwa ni siku tisa tangu ale kiapo cha kuwa Rais. Tunawiwa kusema, ahadi hii ameitekeleza kwa vitendo na Watanzania hatuna budi kusimama imara na kuungana naye kwenye mapambano haya kwa kuizingatia kaulimbiu ”Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu;
Tutimize Wajibu Wetu.