*Huduma za uokoaji zaimarishwa kukidhi idadi kubwa ya wageni

Na MwandishinWetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro


Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) imejiwekea mikakati ya kuboresha huduma kwa wageni wa ndani na nje; JAMHURI linaripoti.

Idadi ya watalii wanaopanda mlima huu mrefu na wa kipekee wenye kilele chenye barafu ukanda wa Ikweta, imekuwa ikipanda katika miaka ya karibuni; filamu ya ‘Tanzania the Royal Tour’ ikitajwa kuwa miongoni mwa machagizo makuu ya ongezeko hilo.

Filamu hiyo ilichukuliwa mwaka 2021 baada ya dunia kutoka katika janga la COVID 19 lililoelekea kuua kabisa sekta ya utalii, na kuzinduliwa mapema mwaka 2022; Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiwa mwigizaji (mwongoza watalii – guide) mkuu.

Kinapa ni hifadhi ya pili nchini katika kuingiza fedha na kuchangia pato la taifa ikiwa nyuma ya Hifadhi ya Taifa Serengeti (Senapa).

Akizungumza ofisi kwake katika lango la kupandia Mlima Kilimanjaro la Marangu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Kinapa, Angela Nyaki anasema:

“Tuna mikakati mbalimbali ya kuimarisha huduma hifadhini baada ya kuwapo ongezejo la idadi ya wageni. Tayari tumeimarisha miundombinu kwa kujenga malazi ya wageni 99 pale Horombo. Wageni maarufu (VIP) nao watakuwa na eneo lao la kulala.”

Horombo ni kituo cha pili kwa wapandaji wa Mlima Kilimanjaro wanaopitia Njia ya Marangu, kikiwa mita 3,720 kutoka usawa wa bahari.

Kingine kikubwa zaidi ambacho kinafanyika Kinapa kwa sasa ni kupandisha maji mlimani.

“Mlima huu una aina zote za hali ya hewa (weather). Huwezi kuamini, huko juu kuna eneo la jangwa kabisa! Na huko ndiko tunakutaka kupeleka maji,” anasema.

Tayari huduma ya mawasiliano ipo hadi kileleni mwa Mlima Kilimanjaro, kitu kinachoongeza fursa ya kutangazwa kwa mlima huu pale watalii wanapofanya ‘live streaming’ kuwapa nafasi ndugu na marafiki zao kokote walipo duniani kuwafuatilia, na Afande Angela anaongeza:

“Pia tunajadiliana na TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania) kutafuta njia bora za kupeleka umeme mlimani bila kuharibu mazingira asilia kuhakikisha kunakuwapo nishati (safi) ya uhakika.”

Afande Angela anasema wamelazimika kuyafanya yote hayo kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia katika kutangaza utalii na vivutio vyake vilivyopo nchini.

“Uamuzi wa Dk. Samia kuwa mwongoza watalii mkuu katika ile filamu (the Royal Tour) ulikuja wakati muafaka na umekuwa na manufaa makubwa katika sekta hii, hasa kwetu Kinapa,” anasema.

Rais Samia ni miongoni mwa wageni wenye hadhi ya juu (VVIP) wanaotembelea na kuitangaza Kinapa na kwa kupitia filamu aliyoiongoza, watalii wengi zaidi wamekuwa wakipanda mlima, kitendo kinachowafanya waliokasimishwa usimamizi wa hifadhi kuboresha zaidi huduma.

“Tanzania The Royal Tour, filamu iliyouonyesha mlima wetu, imeongeza hamasa kwa watu mashuhuri duniani kuja kujaribu kuupanda Mlima Kilimanjaro,” anasema Kamishna Angela.

Anasema awali kupanda mlima kulichukuliwa kama shughuli ngumu isiyokuwa na chembe ya burudani, lakini sasa hali inabadilika taratibu kuendana na wakati.

Katika kuwatoa hofu wapandaji wa milima duniani, Kinapa imeongeza na kuimarisha huduma za uokoaji na tayari kampuni mbili zinafanya kazi hiyo.

Tofauti na awali, sasa uokoaji Mlima Kilimanjaro unafanyika kwa kutumia vifaa vya kisasa zikiwamo helikopta.

Uimarishaji wa miundombinu ya Kinapa unatekelezwa kutokana na Sh milioni 800 zilizotolewa na Serikali ya Dk. Samia kukabiliana na majanga yaliyosababishwa na COVID-19.

Matunda ya Royal Tour

Takwimu zinaonyesha kwamba ndani ya miezi minane iliyopita; Julai 2024 hadi Februari 2025, zaidi ya watu 55,000 wamepanda Mlima Kilimanjaro na kuingiza Sh bilioni 92.

Kabla ya janga la COVID-19, Kinapa ilikuwa ikivutia wastani wa wapandaji mlima 49,000 kwa mwaka.

“Watalii wetu wengi wanaopanda mlima wanatoka Marekani (ambako the Royal Tour pia ilizinduliwa) na kuna uwezekano wa kufikia wageni 100,000 mwisho wa mwaka huu wa fedha,” anasema.

Shughuli za utalii zilidorora sana wakati wa janga la COVID-19 na kama si jitihada za Rais Samia hakuna anayejua sekta hiyo ingekuwa wapi kwa sasa.

Kuhusu umuhimu wa filamu na ‘documentaries’ mbalimbali, Kim Vertleyden, mtalii kutoka Uswisi aliyeshuka kutoka mlimani na kuzungumza na JAMHURI, anasema ametimiza ndoto yake ya tangu utotoni.

“Nilipokuwa mtoto niliona ‘documentary’ (makala ya filamu) ikiuelezea Mlima Kilimanjaro. Nikaweka nia (nadhiri) ya kuupanda mlima huu na leo nikiwa na umri wa miaka 45 sasa, nimetimiza ndoto yangu,” anasema.

Kauli yake inamaanisha kwamba matunda ya filamu ya the Royal Tour iwapo itatangazwa vyema ndani na nje ya nchi, yataendelea kupatikana hata miaka 50 ijayo.

Kim ameahidi kurejea tena Kilimanjaro Oktoba mwaka huu akiwa na rafiki zake kupanda mlima huo mrefu zaidi Afrika.Mwenyeji wa Kim, mwongoza watalii mzawa (guide), Benedict Mato, anaema alikichofanya Rais Samia ni mbegu kwa vijana wa sasa wanaoitazama filamu hiyo.
Ends