Miaka mitatu imetimia tangu mwanamuziki nguli, Papa Wemba, kufariki dunia.
Ilikuwa mithili ya simulizi za ‘Alinacha’ asubuhi ya Jumapili Aprili 24, mwaka 2016, kuzagaa kwa taarifa za kifo cha mtunzi na mwimbaji mkongwe, Papa Wemba, kwamba amefariki dunia.
Taarifa hizo zilieleza kwamba nguli huyo alianguka jukwaani akiwa anatumbuiza jijini Abidjan, nchini Ivory Coast katika tamasha la muziki la FEMUA.
Baadhi ya wanabendi wake waliokuwa jukwaani waliendelea kupiga muziki kabla ya mmoja wao kukimbia kumuokoa baada ya kuona amesalia chini kwa sekunde kadhaa akiwa anatetemeka kisha akazirai.
Msemaji wake, Henry Christmas Mbuta Vokia, alikaririwa akisema: “Marehemu Papa Wemba alikuwa ameingia muda mfupi tu jukwaani kisha akacheza wimbo wa kwanza, mashabiki wakamuomba awaimbie tena wimbo mwingine akakubali.
“Lakini dakika chache tu baada ya kuanza kupiga wimbo wake wa tatu Papa Wemba alianguka na kuzirai ghafla jukwaani.
“Watu wa Shirika la Msalaba Mwekundu walijaribu kumsaidia lakini hakuonyesha dalili nzuri, hivyo wakampeleka hospitalini, lakini baada ya dakika karibu thelathini hivi tukaambiwa kuwa Papa Wemba ametuacha.”
Watu walishuhudia kipande cha video kinachomuonyesha jamaa mmoja akichukua ‘microphone’, halafu akairudisha kwenye steji.
Baada ya Papa Wemba kuanguka, inadaiwa jamaa yuleyule badala ya kumsaidia alikimbilia kwenye ile ‘microphone’ ili isijulikane kwamba aliibadilisha.
Baadhi ya watu wakasambaza taarifa kwamba ‘microphone’ hiyo ilikuwa imewekwa sumu.
Taarifa za kifo chake ziliendelea kuwafikia watu mbalimbali akiwemo mwimbaji mkongwe wa Kongo DRC, Koffi Olomide, ambaye aliandika maneno machache kwenye ukurasa wake wa Instagram akisema: “…kwaheri kaka, asante,” na kuambatanisha picha yao ya pamoja ya siku nyingi kwenye hayo maneno.
Koffi Olomide amekuwa akitajwa kuwa mpiga gitaa wa zamani na mtunzi wa nyimbo kadhaa zilizoimbwa na Papa Wemba.
Baada ya miezi kadhaa kupita tangu mumewe afariki dunia, Marie Rose Lozolo, au kwa jina jingine Mama Amazone, mke wa marehemu Papa Wemba, alikutana na waandishi wa habari na kufunguka mengi kuhusu mpendwa wake huyo.
Alianza kwa kusema kuwa katika maisha yake ya miaka 45 ya ndoa na mumewe walipitia mambo mengi.
“Bado naona ugumu kuishi bila mume wangu kipenzi ambaye alikuwa mwanamuziki kamili, mpole sana. Awapo nyumbani ni nadra sana kumsikia akiongea ovyo, lakini awapo jukwaani ni mtu mwingine tofauti kabisa, kwani huko ndiko ilikuwa dunia yake…” alisema Marie Rose Lozolo.
Aliendelea kusimulia kuwa, sehemu nyingine ambayo alikuwa akionyesha uchangamfu wa hali ya juu ni pale anapokuwa na jamaa zake.
Mama Amazone alifahamiana na Papa Wemba akiwa na umri wa miaka 15 tu, wakati marehemu mumewe alikuwa na miaka 20.
Katika kipindi chote alichoishi na mumewe hakuwahi kujua kama mumewe alikuwa na hadhi kubwa hadi pale alipofariki dunia.
“Wakati akiwa hai alikuwa akipenda kunitania mara kwa mara, akisema siku atakayokufa ndiyo nitajua hadhi yake, pia aliniambia angependa kifo chake kimkute akiwa kazini (jukwaani ), kwa kweli utabiri wake ulitimia…” anasimulia Marie Rose Lozolo.
Alitamka kuwa hakuwahi kuambiwa na Papa kama ana mke mwingine au watoto zaidi ya binti mmoja ambaye alimlea yeye aitwaye Kukuna.
Mama Amazone alisema ataendelea kupigania hakimiliki ya marehemu mumewe, kwani ameacha kazi nyingi na kubwa.
“Mume wangu alikuwa na nyimbo nyingi sana, kuna nyingine alishawahi kunitungia akinitamkia maneno haya: “Nasali Nini Mpo, Nakoma Mopaya, Na Motema Nayo Yebisa Nga, Yebaka Bolingo Emata Nzete, Boni Lelo Tokomi Separer, Ngai Naleli Ngo, Show me the Way, Maboko Ezangi Amazone, Wemba Alingaka, Ngai Naleli, Maboko Ezangi Amazone, Jules Alingaka,” na nyingine nyingi.
Tafsiri yake: “Hebu niambie inakuwaje, najikuta kama mgeni moyoni mwako, fahamu kwamba penzi lina nguvu ya kuupanda mti hadi juu, vipi leo twafikia hadi kuachana! Nalia mie, nalia kweli nammiss Amazone nimpendaye, mie Wemba nalia mie Jules, naimiss mikono niipendayo ya Amazone.”
Marie Rose Lozolo alisema kabla ya kifo cha mumewe walikuwa jijini Paris nchini Ufaransa ambako alipatwa homa akalazwa hospitalini kwa muda wa siku 10.
Iligundulika kuwa alikuwa na malaria, baada ya kupata matibabu aliruhusiwa, lakini madaktari walimshauri apumzike kwa muda wa wiki nne.
Baada ya wiki nne kumalizika wakiwa Paris, waliamua kuongeza wiki mbili zaidi za mapumziko. Baadaye wakaingia studio kurekebisha kazi ya albamu yake mpya ambayo tayari imeshatoka, kisha kurejea jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC).