📍 Mapato na Idadi ya Watalii Vyaongezeka

Na Beatus Maganja, JamhuriMedia, Mbeya

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, amesema kuwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta matokeo chanya katika kukuza sekta ya utalii nchini. Hali hiyo imeonekana kwa ongezeko la idadi ya watalii na mapato katika Hifadhi ya Mpanga/Kipengere, iliyopo katika mikoa ya Mbeya na Njombe.

Semfuko aliyasema hayo Machi 19, 2025, alipotembelea Hifadhi hiyo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujionea vivutio vya utalii na kukagua miradi ya kimkakati ya utalii inayotekelezwa katika hifadhi hiyo.

“Awali, Hifadhi hii haikuwa na watalii kabisa. Hata hivyo, mafanikio makubwa yalianza kuonekana kuanzia mwaka 2022, jambo ambalo linatokana na fedha zilizotolewa na Serikali yetu chini ya uongozi wa Mama Samia,” alisema Semfuko.

Aidha, Semfuko aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne, TAWA imefanikiwa kujenga miundombinu na kuweka vielelezo mbalimbali ambavyo vimesaidia kuvutia watalii katika eneo hilo.

Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko alieleza kuwa TAWA imetangaza fursa za uwekezaji katika hifadhi hiyo na matarajio yake ni kupata uwekezaji mkubwa katika sekta ya malazi na shughuli mbalimbali zitakazochochea utalii na kufanya hifadhi hiyo kuwa kitovu cha utalii katika ukanda wa nyanda za juu kusini.

Kwa upande wake, Kamanda wa Hifadhi ya Mpanga/Kipengere, CI Donacian Makoi, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka kwa kasi kubwa. Kwa sasa, kila mwezi hifadhi hiyo hupokea watalii kati ya 300 na 400, tofauti na awali ambapo walikuwa wakipokea watalii kati ya 100 na 200 kwa mwezi.

kuhusu mapato, katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 mpaka Februari 2025 hifadhi hiyo imeingiza kiasi cha shillingi Millioni 155 tofauti na awali kabla ya uboreshaji wa miundombinu ambapo hifadhi haikuweza kuingiza kiasi chochote cha fedha.

Makoi aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2024/2025, TAWA inaendelea na miradi miwili mikubwa ya kitalii ndani ya hifadhi hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa sehemu za wageni kupata vyakula na vinywaji, maarufu kama “Tourism Lounge,” na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 30 kuelekea ukanda wa juu wa hifadhi, hasa katika eneo la bustani ya dunia lenye spishi zaidi ya 400 za maua.

Naye, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Prof. Jafari Kideghesho, alitoa rai kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kuthamini vitu vyetu na kuwahamasisha kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini hususan Hifadhi ya Mpanga/Kipengere.