*Yaandika historia kwa kuvunja rekodi ya makusanyo miezi minane mfululizo
*Maboresho, uanzishwaji wa mifumo mipya ya TEHAMA yatajwa nyuma ya mafanikio
*Ukaribu kati ya watumishi wa TRA, wafanyabiashara waongeza mapato, kuaminiana
*Mwenda: Ifikapo Agosti mwaka huu mambo yatakuwa mazuri kupita mnavyofikiria
Na Joe Beda, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kero ya muda mrefu iliyokuwa ikimsononesha na kumkera Rais Samia Suluhu Hassan katika mifumo ya ukusanyaji kodi na mingineyo nchini, imepatiwa ufumbuzi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); JAMHURI linaripoti.
Rais Dk. Samia ambaye kesho Machi 19, 2025 anatimiza miaka minne tangu aingie madarakani, amekuwa akisononeshwa na mifumo duni ya TEHAMA inayotoa mwanya wa upotevu wa mapato ya serikali, hususan pale inaposhindwa kusomana.
Taarifa kutoka ndani ya TRA zinasema mifumo ya kikodi iliyoboreshwa, hasa ya TEHAMA, imechangia kwa sehemu kubwa kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato, na sasa makusanyo ya kodi yamepanda kwa asilimia 78 katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya TRA katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita jijini Dodoma, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema ndani ya kipindi hicho makusanyo yameongezeka kutoka Sh trilioni 11.92 mpaka Sh trilioni 21.20, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kwa TRA.
Lengo la TRA lilikuwa kukusanya Sh trilioni 20.42 ndani ya miezi minane iliyopita; ikiwa ni ukuaji wa asilimia 17 ukilinganisha na Sh trilioni 18.06 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24.
Mwenda amesema makusanyo hayo ni ongezeko la Sh trilioni 9.28 (ukuaji wa asilimia 78) kulinganisha na Sh trilioni 11.92 zilizokusanywa kati ya Julai 2020 mpaka Februari 2021, kabla Serikali ya Awamu ya Sita haijaingia madarakani.
Hii ni historia kwa TRA kuvunja rekodi ya makusanyo ya kodi kwa miezi minane mfululizo na Kamishna Mkuu anasema:
“Rais alitoa maagizo matatu makubwa kwa TRA; (kwanza) kuhakikisha mamlaka yanakusanya kodi kwa weledi, (pili) kupanua wigo wa ukusanyaji kodi na (tatu) kujenga uhusiano bora na walipakodi kwa kutumia 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya) kati ya TRA na walipakodi.”
Katika kutekeleza maagizo hayo TRA imeongeza makusanyo ya kodi na ulipaji kodi kwa hiyari; ikiwa ni sehemu ya mafanikio 10 waliyoyapata miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.

Mchango wa uboreshaji mifumo
Katika kuongeza mapato kupitia uboreshaji wa mifumo, taarifa zinasema kwamba Kampuni ya CUPIA kutoka Korea Kusini ndiyo iliyopewa jukumu hilo na sasa mifumo imeboreshwa na kusomana; huku mingine mipya ikianzishwa.
Miongoni mwa mifumo inayoboreshwa ni TANCIS (Tanzania Customs Integrated Sytem) na Mwenda anasema umekuwa na msaada mkubwa kwa TRA.
“TANCIS imeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali na wadau wanaohusika na utoaji wa mizigo bandarini, kwenye viwanja vya ndege na kwenye mipaka,” amesema.
Miongoni mwa wadau wanaosomana na TANCIS ni BRELA, TBS, NIDA na TASAC ambapo ssa mteja halazimiki kutembea na nyaraka na kubisha hodi ofisi moja hadi nyingine kutafuta huduma, kwa kuwa taasisi zote zinapata nyaraka na kuzifanyia kazi kwa kwa wakati mmoja.
Kamishna Mkuu anasema kupitia TANSIC mteja (mlipa kodi) anakuwa katika nafasi ya kuanza kushughulikia mzigo wake mara tu anapopata nyaraka kabla haujafika nchini.
TRA inao Mfumo wa Kodi za Ndani ambao ni mpya, inaofahamika kama IDRAS (Integrated Domestic Revenue Administration System).
Kwa upande mwingine, Mwenda anasema zipo ‘moduli’ mpya zimeanza kufanyakazi zinazolenga kuondoa usumbufu wa muda mrefu waliokuwa wakikumbana nao wateja.
Moduli ya kwanza ni ya ‘leseni za udereva’ ambapo sasa mwombaji atajaza kila kitu kwa njia ya mtandao.
“Anayeomba au anayebadili (kuhuisha) leseni hana sababu ya kuja ofisini. Hapa tunawaondoa ‘vishoka’ pamoja na kupunguza gharama zisizokuwa za lazima,” anasema.
Moduli itakuwa ikishughulika na usajili na umiliki wa magari; utakaokuwa ukifanyika kwa njia ya mtandao.
Kupitia moduli hiyo muuzaji wa gari ataingia wenye mfumo iwe kwa kompyuta au kwenye simu yake ya mkononi na baada ya malipo kukamilika, umiliki unabadilishwa mara moja kwenda kwa mnunuzi na kadi mpya ya gari inatolewa.
“Awali wamiliki wa mwanzo walijikuta kwenye matatizo wakati mnunuzi anapoacha kwa makusudi au kwa bahati mbaya kubadili umiliki kisha, kwa mfano, akakopa kwa dhamana ya kadi ya gari (ambayo haina jina lake) na kushindwa kurejesha mkopo. Sasa hilo limekwisha. Hata ukibadili rangi ya gari, unajaza tu kwenye mfumo kila kitu kinakamilika,” anasema.
Kufikia Agosti mwaka huu, kwa mujibu wa TRA, mifumo mingi mipya itakuwa imekamilika na au kuboreshwa kwa kiwango cha kisasa hivyo kuwapa ahueni si walipa kodi pekee, bali pia watumishi iwa TRA.
TRA, kama mdau wa kodi, wamekwishasiriki kutoa maoni katika Tume ya Rais ya Mapendekozo ya Ulipaji Kodi, wakitarajia kwamba ripoti ya tume itakapotoka itawasaidia sana kuimarisha maboresho wanayoendelea nayo kwenye mifumo ya kodi.
Kwanini uboreshaji huu
Kifupi Kamishna Mkuu Mwenda anasema uboreshaji uliofanyika na unaoendelea kufanyika ambao umechangia ufanisi wa utendaji kazi wa TRA, unafanywa kutokana na maoni ya wadau wao wakubwa; wafanyabiasahra na walipa kodi wote.
“Mapendekezo wanayotupa tunayachukulia kwa uzito na tumeona kuwa yana mashiko. Mifumo hii inatokana na mapendekezo yao na uboreshaji wake utaondoa usumbufu kwa raia wema waliokuwa wakikutana na ulaghai kutoka kwa raia wasio wema,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mwenda anaamini kuwa mikutano ya mara kwa mara inayofanyika kati ya makamishna na mameneja wa TRA imesaidia kuboresha makusanyo na kutengeneza utulivu ongoni mwao.
Tangu Rais Samia alipomteua Mwenda kushika nafasi ya Kamishna Mkuu wa TRA, mbali na ongezeko la makusanyo, utulivu miongomi mwa wafanyabishara umerejea hasa Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo ambao awali ulikuwa umegubikwa na migomo ya mara kwa mara.
Migomo hii huathiri shughuli za uzalishaji mali pamoja na ukusanyaji wa kodi huku pia ikitishia kusababisha uvunjifu wa amani.
Mameneja na makamishna wa TRA nchi nzima wameagizwa na Kamishna Mkuu kukutana na wafanyabiashara kila Alhamishi kusikiliza malalamiko na kero zai.
Tangu utaratibu huo uanze hakina hata Alhamamisi moja iliyopita bila ofisa husika kukutana na wafanyabishara na Mwenda anaasema:
“Wala hatutarajii kuruka hata Alhamisi moja. Hii ni programu ya kudumu. Lakini himaanisha kwamba ni Alhamisi peke yake, hapana. Wakati wowote mfanyabiashara anapokuwa na jambo, sisi tupo tayari kukutana na kuzungumza naye, na kulitatua papo hapo.”
Kamishna Mwenda na wasaidizi wake pamoja na mameneja wa TRA mikoani huwatembelea wafanyabisahra kwenye maeneo yao ya kazi na kuwasikiliza, ingawa pia wanaweza kuwasiliana na ye moja kwa moja kupitia SIKIKA App, maalumu kwa ajil iya kusikiliza kero zao au hata ushauri.
Uhusiano mzuri kati ya TRA na wafanyabiashara nchini ulijidhihirisha wakati wa janga la jengo lililopo Mtaa wa Kongo jijini Dar es Salaam kuporomoka, ambapo TRA walikuwa miongoni mwa taasisi za serikali zilizokwenda kutoa msaada.
Taarifa zinasema kwamba na wafanyabishara wa Kariakoo nao walijikusanya na kuwapa pole TRA wakati jengo lao lilipokumbwa na janga la moto; jambo ambalo lisingeweza kufikirika miaka michache iliyopita.
Katika kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, la kutaka Kariakoo kufanya biashara saa 24, ofisi mbili za TRA; Shauri Moyo na Gerezani, nazo zipo wazi kwa saa 24 kuwahudumia wateja.
Ujumbe kukumbusha kulipa kodi
Kuhusu wateja kupigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupo wa maandishi kuwakumbusha kulipa kodi, TRA inasema ni wajibu wake kufaya hivyo kwa kuwa lengo la mamlaka si kuona mteja anaingia gharama za kulipa faini au riba kwa kuwa tu amesahau kulipa kodi kwa mujibu wa sheria. “Riba na kodi si sehemu ya makadirio ya makusanyo yetu,” anasema.