Ijumaa iliyopita Oktoba 24, mwaka huu ulimwengu uliadhimisha miaka 69 tangu kuanzishwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York nchini Marekani. Ilikuwa ni baada ya Vita Kuu vya Pili ya Dunia kumalizika (1939-1945).
Umoja huu ulioanza na nchi wanachama 50, leo una nchi wanachama 193; hii ni hatua moja kubwa ambayo haina budi kupokewa kwa shangwe, wakati nchi hizo zinakaa pamoja katika mazungumzo na mijadala ya kujenga umoja na uelewano katika dunia yetu.
Nia na shabaha kuu ya Umoja wa Mataifa ni kujenga na kustawisha haki za msingi za binadamu. Hii ina maana kuwa malengo ya umoja huo ni kuifanya dunia kutawaliwa na mambo mawili — amani na usalama.
Leo tunapoadhimisha miaka 69 ya uhai wa Umoja wa Mataifa, kuna maswali na maelezo mengi ya kina yanayohitaji majibu na ufafanuzi sahihi kuhusu hiyo shabaha kuu ya “Haki za msingi za binadamu”.
Maswali na maelezo ya kina hayatoki mbali wala hayahitaji mwenye macho na masikio kuhoji au kueleza tu, bali hata asiye na macho na masikio wanaona na kusikia mambo na shughuli zinazofanwa na Jumuiya hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Kabla sijazungumzia kile ninachokusudia, napenda kuungana na binadamu wenzangu duniani, kuupa hongera Umoja wa Mataifa kufikisha umri wa miaka 69. Hapana shaka Umoja huo umeona na kupambana na misukosuko mingi yenye utata, vitisho, vita na mauaji ya aina aina.
Si hivyo tu, hata mambo ya heri, upendo, furaha, utulivu na amani za hapa na pale zimeonwa na kupita mikononi mwa umoja huo kwa nia kuu ya kutaka kujenga na kuimarisha amani na usalama duniani. Hongera UN.
Nianze kwa kusema na kutoa shukrani kwa Umoja huo kuikubali nchi yetu kuwa mwanachama tangu mwaka 1961 hadi leo na kuweza kuithamini, kuijali katika nyanja mbalilmbali za maendeleo ya binadamu.
Ninashuhudia baadhi ya wananchi wenzetu wanapewa kazi na madaraka ya juu katika umoja huo. Nchi yetu kupewa misaada ya hali na mali na heshima mbele ya mataifa mengine duniani na kuchochea harakati za maendeleo ya nchi.
Kutambua na kupokea shughuli zetu za ustawi wa jamii katika utoaji elimu, matibabu, ajira, utamaduni bila kusahau masuala ya ufundi, sayansi na teknolojia. Uboreshaji wa makazi mijini na kilimo bora huko vijijini.
Shughuli hizo kwangu ni tamu kama asali na ni nzuri kama waridi. Hapa natoa kongole kwa wajumbe na wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa. Kama wahenga wasemavyo, kila jambo lina ncha mbili, basi na umoja huo hali kadhalika.
Ncha hii ya pili kwangu ni chungu kama shubiri na ni mbaya kama dharau. Nimesema hivyo kwa sababu ile shabaha kuu ya Haki za msingi za binadamu na Malengo makuu mawili; amani na salama ni mgogoro duniani hadi leo.
Vita na mapigano kati ya nchi na nchi; na kundi moja na jingine ndani ya nchi vinaendelea huko Iran, Iraq, Libya, Somalia, Nigeria, Israel na kadhalika. Vita hii misingi yake ni kukosekana haki; haki katika maisha, dini na utaifa.
Ndani ya Umoja huu kuna baadhi ya mataifa ndiyo yenye kauli ya uamuzi kama vile Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, (akina NATO) wakiamua lao lazima liwe hata kama haki, amani na usalama unavunjwa.
Leo Wapalestina wanaporwa nchi yao na Marekani kupitia mgongo wa Waisraeli, ambao ni vibaraka wao. Ukiangalia ramani ya nchi ya Wapalestina robo tatu imenyakulliwa na kukaliwa na Waisraeli. UN iko wapi?
Nchini Iran kuna vita ya madhehebu ya dini moja ya Kiislamu, Marekani ndiyo kichecheo kikubwa na Umoja wa Mataifa haina kauli mbele ya Marekani. Sawa hiyo? Vipi UN inakuwa na kigugumizi! Haki iko wapi?
Baadhi ya viongozi wa Afrika wanaotuhumiwa katika mauaji ya kimbari haraka wanafikishwa Mahakama ya Kimataifa, lakini baadhi ya viongozi wa Marekani wanaotuhumiwa kuua viongozi wa Uarabuni na Afrika hawaguswi.
Umoja wa Mataifa wanaona, wala hawatoi amri ya kukamatwa viongozi hao. Hii dhamira ya kuanzisha Umoja wa Mataifa iko wapi? Kweli amani na usalama vitapatikana duniani wakati baadhi ya mataifa ni madikteta ndani ya Umoja huo? Hawaguswi wala kukemewa.
Ni busara Umoja wa Mataifa kuwa na fikra za ukombozi na kimapinduzi kuokoa mataifa yanayoendelea. Hebu mthubutu kuziambia nchi zilizoendelea, hasa Marekani na wenzake kuacha ubabe na uuaji wa binadamu wasio na hatia. DUNIA SALAMA INAWEZEKANA, TIMIZENI WAJIBU WENU.